Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, May 23, 2016

RAIS WA FIFA GIANNI INFANTINO AIPONGEZA YANGA, JUMA ABDUL MCHEZAJI BORA APRILI

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ameipongeza timu ya soka Young Africans ya Dar es Salaam, kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2015/16.
Young Africans imetwaa ubingwa huo kwa msimu wa pili mfululizo, lakini ikiwa ni mara ya 26 tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara mwaka 1965.
Katika salamu zake, kupitia barua yake ya Mei 18, 2016 kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi, Infantino ameelezea ubingwa wa Young Africans kwamba umetokana na kazi kubwa inayofanywa na uongozi wa timu hiyo, makocha, wachezaji pamoja na mashabiki.
“Yanga ndiyo mabingwa wa Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Young Africans na timu nzima isiyoshindika kwa mafanikio haya makubwa. Taji la Young Africans ni matokeo ya mshikamano ulioko ndani ya Young Africans,” amesema Infantino katika barua hiyo yenye kichwa cha habari kinachosema: Salamu za Pongezi kwa Young Africans.
Amesema pongezi zake ziende kwa uongozi wa klabu, makocha na benchi nzima la ufundi, wachezaji, madaktari pamoja na mashabiki wote wa Young Africans.
“Kwa niaba ya familia ya soka, napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Young Africans na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa jinsi mnavyopeleka ujumbe chanya wa soka kwa jamii ya michezo,” alisema Infantino katika barua hiyo iliyotua TFF Mei 21, mwaka huu.
Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikwisha kuipongeza Yanga ambayo imepewa Kombe na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji na kwa sasa wanasubiri zawadi ya fedha Sh 81,345,723. 





JUMA ABDUL MCHEZAJI BORA APRILI VPL
Beki wa kulia wa timu ya soka ya Young African ya Dar es Salaam, Juma Abdul ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Aprili, 2016 baada ya kura zake kuwashinda Donald Ngoma ambaye pia anakipiga Young Africans na Hassan Dilunga wa JKT Ruvu ya Pwani.
Katika rekodi za Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) iliyoketi Jumamosi Iliyopita, imeonesha kwamba Abdul alicheza mechi zote tano za Ligi Kuu kwa mwezi Aprili ambapo pia aliifungia timu yake bao katika harakati za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/16.
Rekodi hizo pia zinaonyesha kwamba beki huyo hakuonyeshwa kadi hata moja katika michezo hiyo mitano sambamba na kutoa mchango mkubwa katika michezo aliyoshiriki kwa mwezi Aprili, 2016. Abdul atazawadiwa fedha Sh. 1,000,000 (milioni moja) na wadhamini wa Ligi hiyo, Kampuni ya mahiri ya simu za mkononi ya Vodacom.
Uwezo aliouonyesha Abdul ulisababisha Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kumjumuisha katika kikosi chake kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Harambee Stars ya Kenya kadhalika Mapharao wa Misri katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Juni 4, mwaka huu.
Wachezaji bora wa miezi minne iliyopita ni kiungo Thaban Kamusoko wa Young Africans (Desemba 2015), beki Shomari Kapombe wa Azam (Januari 2016), Mshambuliaji Mohamed Mkopi wa Tanzania Prisons (Februari 2016) na Shiza Ramadhani Kichuya wa Mtibwa Sugar (Machi 2016).
IMETOLEWA NA TFF

No comments:

Post a Comment