Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, October 7, 2015

TAIFA STARS YATAKATA TAIFA YAIFUNGA MALAWI 2-0









TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo imetakata baada ya kuifunga Malawi `The Flames kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mabao ya Taifa Stars yalifungwa na wachezaji wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Mabao yote ya Taifa Stars yalifungwa katika kipindi cha kwanza huku Samatta akiwa wa kwanza kuwainua wapenzi wa soka nchini kwa bao lake katika dakika ya 18 akipokea pasi safi kutoka kwa Ulimwengu.
Ulimwengu alifunga la pili katika dakika ya 20, baada ya kipa wa Malawi, Simplex Nthala kutema mkwaju wa krosi wa Haji Mwinyi na Ulimwengu akauwahi mpira huo na kuusukumia kimiani na kuihakikishia Taifa Stars ushindi.
Mechi ilikuwa ni ngumu kwa kila upande, Malawi ndiyo waliopeleka mashambulizi mengi zaidi ya Taifa Stars hasa kataika dakika 15 za mwanzo.
Lakini kuanzia dakika 20 hadi 35, Stars walionekana kuutawala mpira zaidi lakini Malawi hawakuwa wamelala, kwani nao walifanya mashambulizi ya kushtukiza.

Ushindi wa Taifa Stars ni faraja kubwa kwao, ambayo mara mbili ilicheza na Malawi katika mechi za kimataifa za kirafiki, Mwanza na Mbeya kwa nyakati tofauti na kutoka sare ya kufunga 1-1, na ile ya suluhu.
Pia ni furaha iliyoje kwa kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa ambaye juzi tu aliingia mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo baada ya awali kuwa na mkataba wa miezi mitatu kama kocha wa muda.
Mkwasa alipewa mikoba ya kuifundisha Taifa Stars kwa muda baada ya kutimuliwa kwa kocha Mholanzi Mart Nooij baada ya timu hiyo kufanya vibaya katika michezo mingi ikiwemo ya kimashindano na kirafiki.
Mbali na Mkwasa, Hemed Morocco naye alilamba mkataba kama msaidizi wa Mkwasa kwa kipindi hicho cha mwaka mmoja na nusu.
Tangu Mkwasa aanze kuifundisha timu hiyo imeshapata sare mbili dhidi ya Uganda katika mashindano ya Kombe la Chan ya mabao ya 1-1 na dhidi ya Nigeria ya 0-0 katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).
Samatta amekuwa msaada mkubwa kwa TP Mazembe baada ya hivi karibuni kuiwezesha timu hiyo kutinga fainali ya Ligi ya Mabigwa wa Afrika baada ya kufunga mabao mawili wakati wakishinda 3-0.
TP Mazembe katika mchezo wa awali ilifungwa mabao 2-1 na kuifanya kutinga fainali kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-2, ambapo sasa itacheza na USM Alger ya Algeria.
Fainali hiyo itapigwa kati ya Oktoba 30 na Novemba mosi wakati ule wa marudiano utafanyika kati ya Novemba 6 na 8.

No comments:

Post a Comment