LEO katika uwanja wa Eden Arena jijini Prague,
Jamhuri ya Czech, kutakuwa na pambano kali la kuwania taji la UEFA Super Cup
kati ya Chelsea na Bayern Munich.
Kitu kikubwa kinachozungumzwa sana kuhusiana na
pambano hilo, ni kufufuka kwa bifu kati ya kocha wa Chelsea, Jose Mourinho na
yule wa Bayern, Pep Guardiola.
Wote wawili hawakuwa na timu hizo zilipokutana
katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 na Chelsea kuibuka kidedea,
pia Guardiola hakuwa na Bayern ilipochukua ubingwa wa Ulaya Juni mwaka huu, na
wala Mourinho hakuwa Chelsea walipobeba taji la Europa League, lakini uwepo wao
sasa unaongeza utamu wa mechi hiyo.
Guardiola na Mourinho walikuwa na upinzani mkubwa
sana kati ya mwaka 2010 na 2012, wakati wakiziongoza Barcelona na Real Madrid,
na Guardiola ndiye alikuwa mbabe zaidi kutokana na kushinda mataji 14 na Barca
kati ya mwaka 2008 na 2012.
Sasa hivi yuko Bayern ambako anawakati mgumu sana wa
kuvaa viatu vya Jupp Heynckes, ambaye msimu uliopita aliipa klabu hiyo mataji
matatu; Bundesliga, Kombe la Ujerumani na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mourinho alinukuliwa na mtandao wa Ujerumani wa Bild
akidai kwamba, hana uhakika iwapo Bayern hii ya Guardiola itakuwa kali kama ile
ya Heynckes iliyochukua taji la Ligi ya Mabingwa.
Jumanne hii, Guardiola alipoteza pointi yake ya
kwanza kwenye Bundesliga baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Freiburg.
Katika pambano hilo Mhispaniola huyo alipumzisha wachezaji saba na Xherdan
Shaqiri ndiye alifunga bao la Munich 1-0.
Lakini kwenye mechi ya leo, Guardiola ataingiza
uwanjani kikosi chake kamili, lakini yuko njia panda juu ya nani ampange kama
kiungo mkabaji. Thiago Alcantara na Javi Martinez wanamajeruhi na Bastian
Schweinsteiger, alitoka uwanjani akichechemea katika pambano dhidi ya Freiburg baada
ya kuumia enka hivyo yuko hatihati kucheza leo.
Mourinho, ambaye amewahi kushinda taji la ligi ya
mabingwa akiwa na Porto na Inter Milan, amekaribishwa kwa mikono miwili baada
ya kurudi Chelsea, ambako aliifundisha kati ya mwaka 2004-2007.
Chelsea ambayo Jumatatu hii nayo ilipata sare ya 0-0
dhidi ya Manchester United kwenye Ligi Kuu England, kocha wake Mourinho anaamini
kwamba timu hiyo itatumia mechi hiyo kama kipimo tosha cha kujiandaa na Ligi ya
Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Chelsea wamewahi kushinda taji la UEFA Super Cup
mwaka 1998, wakati Bayern hawajawahi kubeba taji hilo ambalo halina mashiko
sana kulinganisha na mataji mengine.
Winga wa Bayern, Arjen Robben, ambaye alifunga bao
la ushindi kwenye fainali ya ligi ya mabingwa na kuipa timu yake ushindi wa
mabao 2-1 dhidi ya Borussia Dortmund, anadai kwamba watafurahi kuchukua taji
hilo kwa mara ya kwanza.
Kumbukumbu
Guardiola na Mourinho wamewahi kukutana mara 11
wakati wakizinoa Barcelona na Madrid, Guardiola ameshinda mara tano na Mourinho
mara mbili. Chini ya Guardiola, Barca imewahi kuipiga Madrid ya Mourinho kwa
mabao 5-0 katika uwanja wa Camp Nou, Novemba 29, 2010 na mechi hii ndiyo
ilikuwa ya kwanza kwa wawili hao kukutana.
Wakiwa
Hispania
Kikosi cha Mourinho cha Inter Milan, kiliitoa
Barcelona ya Guardiola kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 kwenye nusu fainali ya
Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2009-2010.
Robben amewahi kuichezea Chelsea kati ya mwaka 2004 na
2007, alishinda mataji mawili ya Kombe la FA, na alifunga mabao 15 katika mechi
67 za ligi akiwa Stamford Bridge chini ya Mourinho.
Andre Schurrle, ambaye ametua wakati huu wa kiangazi,
anaijua vizuri Bayern Munich kutokana na kucheza Bundesliga kwa muda mrefu
akichezea klabu za Bayer Leverkusen na Mainz, mshkaji wake alipokuwa Mainz, Jan
Kirchhoff kwa sasa anakipiga Mainz.
Kevin De Bruyne naye anaijua Bayern kwa sababu
alitumia msimu wa 2012/13 kwa mkopo katika klabu ya Werder Bremen ya Ujerumani
na akiwa huko walipigwa mechi zote mbili na Bayern, lakini yeye alifungwa siku
timu yake ilipopigwa 6-1 na Munich.
Historia
Mara ya mwisho Chelsea na Bayern kukutana ilikuwa
kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 na Chelsea waliibuka
kidedea kwa mikwaju 4-3, baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1
wafungaji wakiwa Didier Drogba kwa Chelsea na Thomas Muller kwa Bayern.
Baada ya kufungwa kwenye fainali hiyo msimu
uliofuata Bayern wakachukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya
kuifunga Borussia Dortmund kwa mabao 2-1 katika uwanja wa Wembley, mabao ya
Bayern yalifungwa na Mario Mandzukic (60) na Arjen Robben (89).
Chelsea kwa upande wao walichukua ubingwa wa Europa
League kwa kuibuka na ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Benfica, bao la Chelsea
liliwekwa kimiani na Branislav Ivanovic, pambano hilo lilipigwa kwenye uwanja
wa Amsterdam Arena.
Klabu zote mbili zimewahi kufungwa kwenye michuano
ya UEFA Super Cup; Chelsea mabingwa wa mwaka 1998, mwaka jana walipigwa 4-1 na
Atletico Madrid katika pambano lililopigwa jijini Monaco.
Wakati kwa upande wao, Bayern hawajawahi kubeba taji
hilo wamewahi kufungwa na Dynamo Kyiv mwaka 1975, Anderlecht mwaka 1976 na
mwaka 2001 walipigwa na Liverpool. Wao ndio timu pekee kufungwa mara tatu
kwenye mechi hiyo bila kushinda.
Dakika 90, wakitoka sare zinaongezwa dakika 30,
ikishindikana matuta na wachezaji saba saba ndiyo watakuwa benchi na
watakaoruhusiwa kuingia ni watatu tu.
Uwanja:
Eden Arena
Prague, Jamhuri ya Czech
Mwamuzi:
Jonas Eriksson (Sweden)
Waamuzi
wasaidizi: Mathias Klasenius (Sweden) Daniel Wärnmark (Sweden)
Mwamuzi
wa akiba: Stefan Wittberg (Sweden)
No comments:
Post a Comment