LONDON, England
BAYERN Munich imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwa mara ya tano katika historia yake, baada ya Jumamosi iliyopita kuinyuka Borussia Dortmund 2-1, katika mechi iliyojaa burudani kubwa kwenye dimba la Wembley.
Fainali hiyo, ambayo ilikutanisha timu mbili za Ujerumani, ilikuwa ya vuta nikuvute kwa muda wote na mashabiki wake kushuhudia mechi safi kabisa kuanzia mwanzo hadi filimbi ya mwisho.
Vitu vichache sana vilizitofautisha timu hizo mbili, ambazo zilikwenda sambamba kwa 0-0 kwa muda mrefu, kisha 1-1 kabla ya dakika tisa ambazo ndizo zilizoweka tofauti hiyo.
Na mwisho wa mechi, kikosi cha Jupp Heynckes - Bayern ndicho kilichokuwa kimechanga vyema karata zake kwa kukichapa kikosi cha Jurgen Klopp, Dortmund. Na hapa, tofauti na mafanikio ya Bayern, hayo yalitokana na maarifa mazuri ya kiufundi ya kocha Heynckes, ambayo aliyafanya huku mechi ikiwa inaendelea.
Mechi ilianza kama Klopp alivyotarajia, ambapo kikosi chake cha Dortmund kilionekana kikitawala mchezo katika dakika 20 za kwanza, ambapo kiungo wa Bayern, Bastian Schweinsteiger alilazimishwa kurudi nyuma hadi kwa mabeki wa kati kutokana na Dortmund kumiliki kwenye sehemu ya kati.
Kutokana na Schweinsteiger kushuka nyuma, jambo hilo liliwafanya Dortmund kucheza kwa nafasi katika sehemu hiyo ya katikati ya uwanja.
Waliweza pia kupanga mashambulizi ya kushitukiza na kumiliki mpira, huku kiungo wao, Ilkay Gundogan, akiwa ndiye aliyekuwa akiamrisha aina ya mchezo unaopaswa kuchezwa kwenye sehemu hiyo ya kati.
Vita ya jino kwa jino baina ya viungo Gundogan na Javi Martinez ilikuwa ni burudani kubwa na kwenye jambo hilo lilifanya kuwapo kwa burudani kubwa katika sehemu hiyo ya katikati ya uwanja.
Kwenye dakika hizo za kwanza, Dortmund ilikuwa na nafasi kubwa. Dakika zilivyosonga mbele, kiungo Mhispania, Martinez, alijiweka sawa mwenyewe na sasa Bayern ikaanza kupata faida ya kujibadilisha kwake.
Nguvu ya Bayern ipo pembeni kwenye kushambulia, lakini wanapokuja kwenye suala la kuzuia, mhimili wao mkubwa upo katikati ya uwanja.
Wakati Martinez na Schweinsteiger walianza kutulia na kutumia nguvu zao kama ilivyokuwa katika mechi dhidi ya Barcelona na Juventus—jambo hilo lilianza kuwa shubiri kwa wapinzani wao.
Walianza kunyang'anya mipira na kufanya kazi kuwa rahisi kwa wachezaji wao wa mbele na mabeki wao, kitu ambacho ndicho kilichoifanya Bayern kuitambia timu hiyo.
Wakati Marco Reus alipopokea mipira nje ya eneo la Bayern, viungo hao wakabaji walimkimbiza kumzuia, huku mabeki wao wakiwa na kazi rahisi ya kuondoa mipira isiyokuwa na madhara.
Jambo hilo walilifanya kwa umakini mkubwa na kwamba Bayern isiponyang'anya mipira, basi viungo hao walisababisha faulo. Kuwabana na kuwazidi nguvu wachezaji wa BVB kuliwafanya waishiwe nguvu na Bayern kuanza kutawala katika sehemu hiyo.
Reus hakupata muda kabisa wa kuweza kuwakimbiza mabeki wa Bayern kama ilivyo kawaida yake ya kuwasumbua mabeki wa timu pinzani aliowahi kucheza nao.
Dortmund walijikuta sasa wanacheza mipira ya juu, kuwapigia washambuliaji wao Reus na Robert Lewandowski, jambo ambalo lilifanya kazi kuwa ngumu zaidi kwa sababu Bayern ilikuwa na wachezaji warefu kwenye safu yake ya ulinzi, Dante na Jerome Boateng.
Reus, ambaye anaonekana kama hana nguvu sana, ushindani wa kupambana kwenye mipira ya juu tena dhidi ya mabeki ambao wana uzito mkubwa kuliko yeye, hilo lilikuwa tatizo kwake na kwa Dortmund.
Na Schweinsteiger anapopata nafasi ya kutawala kiungo, basi siku zote Bayern wamekuwa wakishinda mechi zake kwa sababu uchezaji wake umekuwa ukiwaruhusu mawinga wao kucheza kwa kushambulia zaidi, huku Martinez akicheza kwa tahadhari kuwalinda mabeki.
Franck Ribery hakuwa kwenye ubora wake sana, lakini Arjen Robben alikuwa mtu hatari zaidi kwa upande wa Bavarians. Mdachi huyo, Robben angeweza kufunga mabao mengi tu katika kipindi cha kwanza, lakini alibadilisha mambo kwenye kipindi cha pili kwa kutengeneza bao la Mario Mandzukic, lililokuwa la kwanza kwa Bayern, kabla ya yeye mwenyewe kufunga la ushindi ikiwa imebaki dakika moja kufikia filimbi ya mwisho.
Ribery, Robben na Thomas Muller mara kadha walionekana wakibadilishana nafasi, na mabadiliko hayo ya mawinga hao, Mfaransa na Mdachi ndiyo yaliyozaa matunda.
Ribery alipiga pasi kwa Robben, ambaye aliambaa na mpira upande wa kushoto kabla ya kupiga pasi kwa mfungaji wa bao la kwanza, lakini baadaye, mkali wa zamani wa Marseille, Ribery, alitumia ujanja mkubwa kumtengenezea mpira Robben kufunga bao la ushindi.
Mabadiliko hayo kwenye safu ya ushambuliaji ya Bayern iliwapa shida mabeki wa Dortmund na hivyo kuonekana kama wana matatizo katika kuzuia.
Bao lao la pili walilifunga baada ya Ribery—kuingia kati na kucheza kama mshambuliaji wa kati, ambaye uwezo wake wa kumiliki mipira ulimsaidia kuuweka kwenye himaya yake mpira mrefu kabla ya kupiga kisigino kwa Robben aliyepita mbio kwenye eneo hilo la kati.
Mshambuliaji halisi mwenye namba yake inayomruhusu kucheza kwenye nafasi hiyo, Mandzukic, alikuwa mbali kabisa na tukio hilo.
Ni makosa machache sana ndiyo yaliyoweza kutoa mshindi wa mchezo huo, lakini kubadilika mbinu ndani ya uwanja kwa kocha wa Bayern ndicho kitu kilichoifanya timu yake imbwage Klopp.
No comments:
Post a Comment