MUNICH, Ujerumani
ILIKUWA bonge la mechi. Ilikuwa fainali iliyostahili. Mechi iliyoshirikisha kizazi cha dhahabu ambacho kilikuwa kinahenyeka kusaka mafanikio wanayopaswa kufikiwa nayo.
Kizazi hicho cha aina yake, kilipambwa na kocha mwenye mafanikio na ujuzi wa aina yake katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Hiki ni kizazi cha Bayern Munich, mabingwa wapya wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Tangazo la Pep Guardiola kuwa kocha mpya wa Bayern lililotolewa Januari, kilikuwa ni kipande cha habari ambacho kilishitua wengi, lakini kubwa ni namna gani ataweza kukihimili kibarua chake hicho kipya.
Tangu Januari alipotangazwa Pep Guardiola kuwa atakuwa kocha mpya wa kikosi hicho, ndani ya miezi minne wababe hao wa Ujerumani, wameiteka Ulaya chini ya kocha anayemaliza muda wake, Jupp Heynckes, kitu kinachomweka pabaya Guardiola katika kutetea mafanikio hayo.
Bayern imetwaa ubingwa wa Bundesliga kwa tofauti ya pointi 25, watanyakua ubingwa wa Kombe la Ujerumani na sasa ni wafalme wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa mafanikio hayo, kutwaa mataji matatu makubwa kwa msimu mmoja, hilo linafanya suala la kurithi mikoba ya Heynckes kuwa ngumu katika kikosi hicho cha Bayern.
Bayern ilifungwa mara mbili kati ya fainali tatu za Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, ilizofanikiwa kutinga miaka ya hivi karibuni na wachezaji iliyokuwa nao wapo kwenye kiwango bora na muda ulianza kuwatupa mkono.
Msimu uliopita ilipopoteza fainali mbele ya Chelsea, tena iliyofanyika kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Allianz Arena, uliibua shaka juu ya nguvu ya kiakili ya nyota wa kikosi hicho na kitendo cha mara mbili mfululizo kupokwa taji la Bundesliga na wapinzani wao, Borussia Dortmund, ilikuwa ni kama kupaka chumvi kwenye vidonda.
Kuhusu Guardiola, wakati wanamsajili, walisema kwamba anayafahamu hayo yote. Lakini, sasa Bayern imeweza kumaliza tatizo lao hata bila ya msaada wa Guardiola.
Kiwango chenye ubora mkubwa kilichoonyeshwa na Bavarians katika msimu huu wa 2012-13 kilikuwa cha daraja la peke yake, kutokana na vichapo ilivyokuwa ikivitoa kwa wapinzani wao.
Vichapo vya mabao kama 9-2, 6-1 na 5-0 ilivyovitoa nyumbani na ugenini na matokeo mengine ya aina hiyo, vilitosha kuonyesha kwamba Bayern kwa msimu huu walikuwa kwenye anga jingine.
Kwenye Ligi ya Mabingwa, ushindi wa jumla wa mabao 7-0 dhidi ya Barcelona (timu iliyojengwa na Pep) kuliibua madai kwamba zama za Wacatalunya hao zimefika mwisho na sasa ni zamu ya Wadachi.
Pep, ambaye mwanzoni alihisiwa kwamba angetoa msaada wa namna ya kuifunga Barca baada ya kupangwa na kikosi chake kipya cha Bayern, alitazama mechi hizo baina ya timu hizo akiwa jijini New York, Marekani.
Na tangu hapo, jambo hilo limemfanya kukosa raha kabisa, kwa sababu ukweli wa mambo ni kwamba kibarua chake atakachokirithi kutoka kwa Heynckes si rahisi tena.
Guardiola hana furaha tena, anafahamu kibarua kinachomkabili ni kigumu, kwa sababu si kazi rahisi tena kuona kiwango cha sasa cha Bayern ikacheza kwa kiwango kingine cha juu zaidi ya hicho au hata kupata matokeo mengine yaliyobora zaidi ya iliyopata msimu huu.
Sawa, Bayern ilipoteza mipira mara nyingi sana kwenye mechi yake dhidi ya Dortmund kwenye fainali na kucheza chini ya ubora wake katika dakika 25, lakini hadi filimbi ya mwisho inapulizwa, wababe hao maarufu kama Bavarian walikuwa wakimiliki kwa asilimia 61, kitu ambacho kinafanana na Barca ilivyokuwa chini ya Guardiola, ambapo aliinoa timu hiyo kwa mechi 247.
Na kiwango hicho cha kumiliki mpira kwa asilimia nyingi walikifanya wakiwa na timu inayowafahamu vilivyo. Fainali ya mwaka huu ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ilikuwa ni 'German Clasico'.
Falsafa za Guardiola ni kufundisha mpira wa pasi zaidi na kwamba jambo hilo atalifanya kwenye kikosi chake cha Bayern, lakini timu yenyewe tayari ipo vizuri kiufundi na inaweza kupiga pasi zenye ubora kabisa, licha ya kutokuwa na mchezaji mwenye kariba ya Lionel Messi.
Kwa ukweli uliopo kwa kipindi hiki, hakuna timu nyingine iliyobora kuliko kikosi hiki cha Bayern Munich. Kwenye hilo kama unataka kumpa alama Guardiola kwa uchaguzi wake, ni wazi anapata 100% ya kuchagua timu sahihi.
Uteuzi wake kama kocha mpya wa Bayern, jambo hilo liliwapa morali wa timu hiyo na kutaka kuonyesha bosi wao mpya kile kitu wanachoweza kukifanya. Kiwango hicho cha wachezaji, ikiwamo kilichoonyeshwa na shujaa wa Wembley, Arjen Robben, ambaye ni wazi kabisa anaweza kuwa mchezaji wa kwanza kuonyeshwa mlango wa kutokea wakati Guardiola atakapowasili.
Na kama Bayern watatwaa DFB Pokal kwa kuinyuka Stuttgart, Juni Mosi (kitu ambacho wanatarajia kukifanya), Guardiola hapo atakuwa yupo kwenye kibarua kigumu zaidi ndani ya timu hii.
Mario Gotze atajiunga na timu hiyo akitokea Dortmund mwishoni mwa msimu huu, wakati huo fungu kubwa la usajili likimsubiri kocha mpya awasili. Na jambo hilo, pamoja na umaarufu wa timu, kocha huyo wa Catalan anatarajiwa kuifanya Bayern kuwa bora zaidi.
Alianza kuinoa Barca, alirithi timu ambayo ilikuwa haina kitu na ilikuwa haina vigezo vya kuwa timu ya ushindi, tofauti na atakavyorithi Bayern - timu ambayo imesheheni wachezaji washindi. Na sasa Guardiola atalazimika kuendeleza utawala wa timu hiyo - bila ya kujali changamoto gani atakumbana nazo. Huu ni mtihani mkubwa kwake.
No comments:
Post a Comment