Halila
Tongolanga amefariki jana usiku katika hospitali ya Muhimbili. Alikuwa
mwanamuziki wa siku nyingi na alifahamika kwanza kwa wengi baada ya kuanza kusikika kibao chake cha lugha ya Kimakonde cha Kila munu ave na kwao, chenye
tafsiri ya ‘Kila mtu ana kwao’ ambacho alikirekodi akiwa bendi ya jeshi ya CTU
Monduli, iliyojulikana kama Les
Mwenge. Kwa kifupi ni kuwa baada ya hapo aliitwa kujiunga na bendi iliyokuwa
mali ya Dr Alex Khalid, iliyokuwa ikiitwa Makondeko Six. Wakati huo Dr Khalid
alikuwa na sehemu kubwa ya burudani iliyokuwa pia na ukumbi na ilikuwa inaitwa
Makondeko ikawa na bendi ya watu sita hivyo bendi hiyo ikaitwa Makondeko Six.
Bendi hii awali ilikuwa ikipiga muziki kwa kufuata nyayo za bendi ya Tatu Nane,
lakini Dr Khalid baada ya kuona bendi haina umaarufu kutokana na aina ya muziki iliyokuwa ikipiga, ndipo alipomuita
Halila Tongolanga nae akaja na baadhi ya wanamuziki wakajiunga na kuanzisha kundi
lililoendelea kutumia jina la Makondeko Six japo wanamuziki walikuwa wengi zaidi
ya sita. Na ndipo katika kundi hili lilikuwa na wanamuziki wengine kama
Innocent Nganyagwa, Anna mwaole wakaweza kurekodi tena wimbo wa Kila Munu Ave
na kwao na kundi kupata umaarufu mkubwa mpaka baada ya kusambaratika kwa Makondeko baada ya kifo cha Dr Alex Khalid, lakini Tongolanga aliendelea
kutumia jina la Makondeko.
|
Baadhi ya wanamuziki waliowahi kufanya kazi na Tongolanga katika kundi la makondeko Six, wakiwa wanasubiri kusafirisha mwili wa mpendwa wao.Toka kushoto, Innocent Nganyagwa, Meneja wa bendi, mpiga solo, Waninga |
|
Tongolanga amefanya kazi nyingi za muziki ikiwemo
kuwa mmoja wa kundi lililoundwa na wanamuziki wengine mahiri kama Moshi William, Muhidin Mwalim, Huluka Uvuruge, Kandaya na wengine lililojulikana
kama Bana mwambe, ambapo waliweza kutoka nyimbo nyingi nzuri sana wakati
biashara ya kuuza album ilipokuwa ina faida. Tongolanga ameagwa na wapenzi wa
muziki ndugu na marafiki, lakini kulikuwa na uhaba mkubwa wa wanamuziki wenzie katika
kundi lililokuja kumuaga mwanamuziki huyu. Waliojitokeza hasa ni wanamuziki wale tu
ambao waliwahi kupiga nae katika kundi la Makondeko na Bana Mwambe na wanamuziki wengine wachache wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Muziki John Kitime, Katibu Mkuu wa Chamudara Hassan Msumari. Serikali iliwakilishwa na Katibu Mtendaji wa BASATA. Katika jambo moja kubwa lililotokea
wakati wa kuaga mwili ni kujitokeza kwa balozi wa Msumbiiji Bi Monica Patricio
Clemente aliyefika Muhimbili kuaga mwili wa Tongolanga akiwa amesindikizwa na maafisa wengine, na pia Balozi huo alitoa
rambirambi zake kama Balozi na alitoa rambirambi kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa
Msumbiji. Hili lilikumbusha usemi wa wahenga ‘Nabii hathaminiwi kwao.’ Taarifa
zilizopatikana pale ni kuwa Tongolanga alikuwa mtu maarufu sana nchini
Msumbiji, na aliyekuwa ni msanii muhimu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini
humo.
|
Balozi wa Msumbiji Bi Monica Patricio
Clemente akiaga sanduku lililokuwa na mwili wa Halila Tongolanga |
Nilipokutana
nae kwa mara ya mwisho akiwa kitandani Tongolanda kwa sauti ya uchovu alinambia
alikuwa na mengi ya kunambia, wakati tunasubiri taratib kukamilika za kuanza
kusafirisha mwili, Innocent Nganyagwa ambaye alikuwa mmoja ya wanamuziki
waliotengeneza kundi la Makondeko Six alinambia Tongolanga alikuwa amepanga
kufanya onyesho la ‘Usiku wa Makondeko’ na alikuwa na mipango mingine mikubwa
ya kufanya kupitia kipaji chake. Pengine ndiyo hayo aliyotaka kunambia Mungu
pekee anajua.
Shukrani za pekee zimfikie Mbunge wa Tandahimba Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, kwani kwa juhudi zake Tongolanga alisafirishwa akiwa hai kutoka Ndanda hadi Dar es Salaam kwa matibabu, na pia ndie aliyeusafirisha mwili wa mwanamuziki huyu kwenda Mchichila kwa ajili ya mazishi.
|
Toka kushoto Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Nyangamale, Balozi wa Msumbiji nchini, Katibu Mtendaji wa BASATA, Mbunge wa Tandahimba Mhe Katani Katani, afisa wa Ubalozi wa Msumbiji |
Tongolanga
anategemewa kuzikwa kijijini kwao Mchichila kesho Junanne 6 Juni 2017.
Mungu
Amlaze Pema Halila Tongolanga
|
Mpiga Kinanda Geophrey Kumburu, Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza, Katibu Mkuu wa CHAMUDATA Hassan Msumari |
|
John Kitime, wanamuziki wa Makondeko Six, Mngereza, KumburuAdd caption |
|
Sanduku alilolazwa Halila Tongolanga likitayarishwa kuingizwa kwenye gari la kusafirisha kuelekea Mcjichila |
|
Sanduku likiingizwa kwenye gari |
Imetayarishwa na John Kitime wa www.tanzaniarhumba.blogspot.com
No comments:
Post a Comment