MBAO imetia ‘mdudu’
sherehe za ubingwa za Yanga baada ya kuifunga bao 1-0 katika mechi ya kufunga pazi la
Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.
Ushindi huo umeifanya Mbao kukwepa kushuka daraja,
na sasa inabaki Ligi Kuu huku timu nyingine kutoka mkoani Mwanza, Toto Africans na
African Lyon ya Dar es Salaam zikiunganana JKT Ruvu ya Pwani kushuka daraja.
Aidha, mahasimu wa jadi wa Yanga, Simba walishinda mabao
2-1 dhidi ya Mwadui kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam, na kufikisha pointi 68
sawa naYanga lakini ikikosa ubingwa kwa mwaka wa tano kwa vile imezidiwa kwa uwiano mzuri wa mabao.
Katika mechi ya Kirumba, Mbao ilipata bao katika dakika ya
22 likifungwa na Habib Haji kwa shuti kali lililomzidi mlinda mlango wa Yanga Beno Kakolanya na kujaa wavuni.
Timu zilishambuliana kwa zamu katika mechi hiyo iliyojaa ubabe hasa dakika ya
79 pale wachezaji waYanga walipomsukuma mwamuzi Ludovick Charles
na kumwangusha chini wakidai kunyimwa penalti.
Aidha, mechi hiyo ililazimika kusimama katika dakika ya 56
pale wachezaji wa Yanga wakiongozwa na nahodha wao Nadir Haroub ‘Canavaro’,
Geofrey Mwashiuya na Simon Msuva kwenda kufukua kwenye goli la
Mbao wakidai kuna vitu vimefukiwa.
Kwenye uwanja waTaifa, Dar es Salaam, Simba ilipata bao
la kuongoza katika dakika ya 17 likifungwa na Shiza Kichuya kwa mkwaju wa Penalti iliyotolewa na mwamuzi
Erick Onoka waArusha baada ya Kichuya kukwatuliwa eneo la
hatari na kipa wa Mwadui Shaaban Kado.
Dakika ya 23 Ibrahim Ajibu aliifungia Simba bao la
pili baada ya kuunganisha vema pasi ya Juma Luizio kabla ya kuujaza mpira wavuni.
Dakika tatu kabla ya kwenda Mapumziko,
Mwadui ilipata bao kupitia kwa Paul Nonga aliyeunganisha pasi ya Hassan Kabunda.
Simba ilitawala vipindi vyote vya mechi hiyo hali iliyowafanya Mwadui muda mwingi kucheza kwa kujilinda.
Aidha, baada ya mechi hiyo wachezaji wa Simba na viongozi
wake hawakupanda jukwaani kupokea zawadi yao ya mshindi wa pili kwa madai bingwa bado hajaamuliwa kwa
vile rufaa yao bado haijarudi Fifa.
Simba imekata rufaa Fifa ikipinga maamuzi ya kamati ya Sheria na hadhi kwa wachezaji kuwapokwa pointi
3 na mabao mawili waliyopewa na kamati ya saa 72 baada ya kuikatia rufaa Kagera Sugar
ikidai kumtumia mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano katika mechi dhidi yao iliyochezwa Aprili mwaka huu.
Aidha,
katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Majimaji Songea,
wenyeji Majimaji wamebaki Ligi Kuu baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1.
Majimaji ilikuwa ikihitaji ushindi kwa udi na uvumba kubaki kwenye ligi baada ya kuwa na mwenendo mbaya katika mechi zake za raundi ya pili.
Timu nyingine iliyonusurika kushuka ilikuwa Ndanda ya Mtwara ambayo ilitumia vizuri uwanja
wake wa nyumbani wa Nangwanda Sijaona kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT
Ruvu ambayo ilishashuka daraja muda mrefu.
Toto Africans
ilishindwa kujinusuru baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 ugenini Manungu,
Turiani dhidi ya Mtibwa Sugar.
Aidha, African Lyon iliyopanda daraja msimu huu,
imerudi ilipotoka baada ya kutoka suluhu na Prisons na hivyo pointi hazikutosha kumbakiza Ligi Kuu ya msimu ujao.
Kagera Sugar
imemaliza nafasi ya tatu baada ya kuifunga Azam bao 1-0 nyumbani kwake Azam Complex
Chamazi.
Baada ya matokeo hayo,
timu zilizobaki kwenye Ligi Kuu ni Yanga, Simba, Kagera Sugar, Azam, Mtibwa Sugar,
Ruvu Shooting, Mwadui, Stand United, Majimaji, Prisons, Mbeya City, Ndanda,
Mbao ambazo zitaungana na timu zilizopanda msimu huu, Njombe Mji ya Njombe,
Lipuli ya Iringa na Singida United ya Singida kucheza LigiKuu.
Kwa upande wa wafungaji bora
wachezaji Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting na Simon Msuva wa Yanga wamefungana wote wakiwa na mabao
14, hivyo inabidi iangaliwe aina ya mabao aliyofunga kila mchezaji ndipo iamuliwe mshindi.
No comments:
Post a Comment