Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limewateua Watanzania watatu kuwa maofisa waandamizi wa kusimamia mchezo wa kundi A kati ya Ghana na Gabon wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 utakaofanyika Uwanja wa Port Gentil utakaofanyika kesho Mei 17, 2017.
Watanzania hao ni Mwesigwa Selestine atakayekuwa Kamishna wa mchezo huo wakati Frank John Komba atakuwa mwamuzi msaidizi na katika kitengo cha kitaalamu cha uchunguzi kwa wachezaji wanaotumia dawa za kusisimua misuli atakuwa Dk. Paul Gasper Marealle.
Hii ni fahari kwa nchi yetu Tanzania kwa viongozi wake kuthaminiwa na kuaminika katika nyanja za kimataifa.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawapongeza viongozi hao na inawatakia kila la kheri katika kutimiza majukumu waliyopangiwa kesho na baadaye hasa ikizingatiwa kuwa fainali zijazo za vijana kama hizi, zitafanyika Tanzania mwaka 2019.
No comments:
Post a Comment