ANTONIO
Conte ni kocha mahiri na mwenye raha sana, miongoni mwa makocha wa klabu za
Ligi Kuu ya England (EPL), kwa sababu amefanikiwa kutwaa ubingwa katika msimu
wake wa kwanza Chelsea na England kwa ujumla.
Mtaliano
huyu mwenye umri wa miaka 47, baada ya kupata mafanikio hayo, na pia kuingia
kwenye fainali ya Kombe la FA itakayopigwa baadaye Uwanja wa Taifa wa England –
Wembley, anatazamwa sasa na wadau mbalimbali, kuona iwapo maendeleo yenyewe
yatakuwa endelevu.
Kuanzia wiki
mbili zilizopita kumekuwapo tetesi kwamba huenda akaondoka, na kwamba Barcelona
walikuwa wanatumia kila mbinu kumchukua, ili akazibe nafasi inayoachwa wazi na
kocha wao, Luis Enrique aliyeamua kupumzika mwishoni mwa msimu huu.
Chelsea,
wawe au wasiwe na Conte, wana mtihani Ulaya, kwani baada ya kuwa nje ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya (UCL) wanarejea kwa kishindo msimu ujao, lakini pia mtihani
mwingine ni kutetea ubingwa, jambo ambalo siku zote limekuwa gumu kwa timu
nyingi, mfano wa karibu kabisa ukiwa ni wa Leicester waliotwaa pasipo
kutarajiwa msimu uliopita na kulitema mapema msimu huu kwa kufungwa mfululizo
hadi wakamfukuza kocha aliyewapa mafanikio hayo, Claudio Ranieri.
Baada ya
kujihakikishia ubingwa, Conte alisema kwamba hiyo ilikuwa ndio mwanzo wake tu
hapo Chelsea na kwamba mengi yalikuwa yanakuja, lakini mitaani watu wanasema
akiisha kupata taji hilo anataka kwenda kwingine kukabiliana na changamoto
mpya.
Wachezaji wa
zamani wa Chelsea na waliokuwa na umaarufu kwenye maeneo tofauti, Ruud Gullit,
Pat Nevin, Chris Sutton, Graeme le Saux na Mark Schwarzer wameitazama klabu yao
ya zamani na wana maoni mbalimbali, ikiwa ni juu ya Conte na mengine jinsi
klabu inavyoweza kujiimarisha ili kukabiliana na changamoto zilizo mbele yake.
Je, Conte
atabaki? Taarifa kutoka nyumbani kwake, Italia, zinasema kwamba klabu ya Inter
Milan, inayomwagiwa fedha nyingi na wafanyabiashara wa China, ipo tayari
kumchukua Conte na kumpa mshahara wa pauni 250,000 kwa wiki – na hicho kinaweza
kuwa kichochea cha yeye kuondoka Stamford Bridge iwapo Roman Abramovich
hataangalia hilo.
Kuhusishwa
kwake na kwenda Italia kunaangaliwa pia na ukweli kwamba mkewe na binti yao
mwenye umri wa miaka tisa wamebaki huko baada ya Conte kuhamia jijini hapa
mwaka jana. Ruud Gullit aliyecheza Chelsea na pia kuwa kocha kati ya 1995-98
ana maoni hapa:
“Nikizungumza
kwa mtazamo wa kisoka, ni wazi kwamba atabaki. Changamoto yake ijayo ni kutwaa
ubingwa wa UCL na anaweza kufanya hivyo na Chelsea. Ikiwa anahisi anayo timu
inayoweza kushinda, kwa nini aondoke akaanze tena upya kabisa kwingineko?
“Hata hivyo
ni jambo tofauti ikiwa ni uamuzi juu ya familia yake. Masuala yake binafsi ni
muhimu pia. Familia yake hawapo London, na hii kidogo si kawaida kwa sababu
nadhani hili ndilo jiji zuri zaidi ya yote duniani, sasa kwa nini hawaji? Hata
hivyo, ingeeleweka ikiwa watu wanazifuata sana mila na dsturi zao. Na ikiwa
wanafamilia wake wanataka kubaki Italia, basi ni uamuzi rahisi tu kwake
kufanya.”
Pat Nevin
aliyecheza mechi 250 akiwa na Chelsea kati ya 1983 na 1988 anasema kwamba baada
ya kuzungumza na Conte kwa saa kadhaa wiki chache ilizopita, atashangaa iwapo
ataondoka.
“Yaani hiyo
itakuwa ofa isiyo ya kawaida kuweza kumwondosha Chelsea lakini kitu ambacho kwa
kawaida huwafanya makocha wakaondoka kwenye nafasi kama yake ni pale wanapokuwa
hawana uamuzi au wanaingiliwa kwenye mambo yao.
“Sidhani
kwamba suala la fedha linaweza kumfanya aondoke na aliniambia kwamba anafurahia
maisha ya London sasa. Kitu kingine cha kufikiria ni pale unaposimama Stamford
Bridge na kusikia washabiki wakiimba 'Antonio, Antonio' ndipo unatambua kula
mmoja anakuenzi. Kwenye hali kama hiyo ni ngumu kocha kuondoka,” anasema Nevin.
Chris Sutton
aliyevunja rekodi ya Chelsea kwa kusajiliwa kwa pauni milioni 10 mwaka 1999 anasema
kitu pekee anachoona kinaweza kumwondosha Conte Chelsea ni iwapo hatapewa fungu
na kupata wachezaji anaowataka. Kwamba hadhani atatoa kipaumbele sana kwa UCL,
maana atakuwa anataka kuchukua makombe yote ya nyumbani.
Conte
alitwaa ubingwa wa Serie A – Ligi Kuu ya Italia mara tatu mfululizo kuanzia
2012, lakini hana rekodi nzuri kwenye UCL, kwani Juve walipigwa 4-0 kwa ujumla
kwenye mechi za robo fainali msimu wa 2012/13 na msimu uliopita wakakwamia
kwenye hatua ya makundi.
Graeme le
Saux aliyecheza mechi zaidi ya 300 Chelsea kwa vipindi viwili tofauti vya kati
ya 1987-1993 kisha 1997-2003 anasema endelevu wowote katika mafanikio
unategemea na wafanyakazi, na kwamba iwapo Chelsea wataweza kubaki na wachezaji
wenye kiwango, basi hawana tatizo.
"Eden
Hazard na N'Golo Kante kila mmoja ana umri wa miaka 26 na huo ni umri mdogo,
lakini kwa nguvu zao wana uwezo mkubwa wa kuwafanya Chelsea kuwa imara
wakisonga mbele. Diego Costa amehusishwa na kwenda China lakini ni muhimu kwa
Chelsea kubakisha kundi hili la wachezaji. Wakifanya hivyo, wataingia msimu
ujao wakipewa nafasi kubwa ya kutetea ubingwa huu,” anasema Le Saux.
Mark
Schwarzer aliyekuwa kwenye kikosi cha Chelsea 2014/15 anaona kwamba kuna
uwezekano mkubwa kwa Chelsea kutwaa tena ubingwa wa EPL msimu ujao lakini pia
ule wa UCL. Kuna wachezaji kadhaa kwenye kikosi hicho waliocheza mechi za UCL
kwa mafanikio.
No comments:
Post a Comment