*Baada ya
kukosoa sasa ni wakati wake wa kufanya kwa vitendo
Na Rahel Pallangyo
BAADA ya muda mrefu kuwa na kiu ya kuona Tanzania
inafanya vizuri katika michezo, hususani ule wa riadha, Wilhelm
Gidabuday amekuwa Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT).
Sasa amevaa viatu vilivyoachwa na Suleiman Nyambui
ambaye alikiacha kiti hicho cha ukatibu mkuu baada ya kupata nafasi ya kuwa
kocha wa timu ya taifa ya Brunei.
Mkutano Mkuu wa uchaguzi Mkuu wa RT uliofanyika Jumamosi
iliopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wajumbe wa mkutano huo
walimchagua Gidabuday kuwa Katibu Mkuu kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Baada ya kuondoka kwa Nyambui, nafasi hiyo ilikuwa
ikikaimiwa na Ombeni Zavalla ambaye alikuwa katibu msaidizi.
Gidabuday siyo jina geni masikioni mwa wengi kwa jinsi
ambavyo alivyokuwa akipigania maendeleo ya mchezo huo kwa kuwa mstari wa mbele
kuwakosoa viongozi wa michezo.
Alikuwa
mstari wa mbele kuosoa
Hakuna chombo cha habari kisichomjua Kidabuday kwanza
kutokana na jina lake kuwa la kipekee
kuwa na kipaji kikubwa cha kuongea kwa mpangilio.
Kidabuday lianza kukosoa kuanzia RT hadi Kamati ya
Olimpiki Tanzania (TOC) akisema wameshindwa kuiwezesha Tanzania kupata medali.
Kuna wakati aliingia katika mgogoro mkubwa na TOC hasa
katibu wake Filbert Bayi pale alipodaikuwa yuko tayari kuchoma vyeti vyake
uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kama timu ya Tanzania
iliyoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola Glascow, Scotland ingerudi na medali.
Timu hiyo haikurudi na medali na Gidabuday aliendelea
kuchonga na kuzidi kujizolea umaarufu, lakini hakujua kuwa TOC haikuwa na
wachezaji na jukumu la kuandaa timu liko kwa vyama vya michezo.
Gidabuday alitakiwa kuvisaka vyama vya michezo na sio
TOC, ambayo haina wachezaji na haikuwa na fungu la kuvifaidia vyaka kuziandaa
timu zao.
Mchawi mpe
mwao amlee.
Kuna usemi wa Kiswahili usemao kuwa, mchawi mpe mwanao
amlee kwani kufanya hivyo kutamzuia kumuua mtoto huyo kwani ataogopa akifanya
hivyo atajulikana kuwa ni yeye aliyehusika na mauaji hayo.
Watu wa riadha hawakukosea kabisa kumpa Gidabuday kazi
ya kuiongoza RT kwani baada ya kuongea mengi mazuri na mipango mingi ya
kuuendeleza mchezo huo, sasa ni wakati wake wa kuyafanya kwa vitendo.
Yale ambayo aliweza kuyakosoa kwa muda mrefu, sasa wakati
umefika wa kuyaweka katika vitendo, ili Tanzania iweze kupiga hatua kubwa
katika mchezo wa riadha.
Malengo yake
makubwa
Gidabuday anasema ili kuinua riadha hakuna budi
kuimarisha vyama vya mikoa kwa kuvipatia vifaa kama ofisi, usafiri pamoja na
komputa.
Katibu Gidabuday anasema kwa kushirikiana na makatibu
tawala wa mikoa watahakikisha kila mkoa unapata ofisi, usafiri pamoja na
komputa ili kuwarahisishia viongozi wa mikoa kwenye utendaji wao wa majukumu.
"Riadha Taifa haiwezi kuona vipaji vilivyopo
mikoani ila vyama vya mikoa ndivyo vye uwezo wa kuvifikia vipaji hivyo
vilivyopo wilayani hadi vijijini kinachotakiwa ni kuwawezesha tu, “ anasema.
Anasema kuwa wakifanikiwa kuwasaidia viongozi wa mikoa
hakuna wasiwasi kuwa riadha itarejeakatikammstari kama ilivyokuwa miaka ya
nyuma ya 1970 hadi 1990.
Gidabuday anasema viongozi wa vyama vya mikoa
walifanywa kama kiungo wakati wa mkutano mkuu kwa sababu ni wapiga kura tu
lakini wakati wa maendeleo wamekuwa wakitengwa.
Kituo cha
kuendeleza riadha
Ili kuendeleza na kukuza vipaji vinavyopatikana kwenye
mashindano mbalimbali, Gidabuday anasema wanatarajia kuanzisha kituo cha kukuza
na kuendeleza vipaji.
"Kuna mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Msingi
Tanzania (UMISHUMTA), na ile ya Sekondari (UMISSETA) na mashindano ya bingwa wa
taifa, hivyo washindi wanaopatikana tutakuwa tunawaweka kwenye kituo,"
alisema.
Pia Gidabuday anasema angependa kituo hicho kijengwe
kati ya mikoa ya Kanda za Juu Kusini kwa sababu maeneo hayo hali ya hewa ni
nzuri kufanyia mazoezi kuliko mikoa yenye joto.
Gidabuday anasema kuwa na kituo kunaweza kurudisha
riadha kwani kipindi ambacho michezo ilisimama shuleni ilisababisha michezo
kudorora kwa ujumla.
Pia Gidabuday anasema kuwa wanatarajia kuhamasisha
mchezo wa riadha kwa mikoa ya Kusini kwani anaamini wanaweza kupata wanariadha
wazuri tatizo hawajapata watu wa kuwahamasisha kupenda mchezo huo kama ilivyo
kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Kati.
Wataalamu wa
riadha
Katika kuendeleza riadha Gidabuday anasema
watahakkikisha wanawatumia wataalamu waliopo na kutoa mafunzo kwa wataalamu ili
wale wanaowafundisha wanariadha wawe na elimu sahihi.
"Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha
(IAAF) linatoa kozi mbalimbali, hivyo ni jukumu la RT kuhakikisha linapeleka watu
kwenda kusoma au unaweza kuomba mtaalamu aje kufundisha hapa nchini hivyo
tutahakikisha tunatoa fursa za kuendeleza makocha," alisema.
Gidabuday anasema yeye kama mtendaji atakuwa makini
kufuatilia ratiba ya IAAF kuona fursa zilizopo na kuzitumia, kwani RT walipoteza uaminifu kwa IAAF
Pia alisema RT inajivunia kuwa na wataalamu kama Samuweli
Tupa, Robert Kaliyahe na wengine wingi, ambapo ameahidi kuwatumia.
Nafasi za
Mafunzo Marekani
Gidabuday anasema Tanzania ilikuwa inapata nafasi za
masomo na mafunzo kwenye vyuo vikuu nchini Marekani, lakini nafasi hizo
zilikoma kutolewa 1993 baada ya kuona viongozi wa RT (zamani TAAA) walikuwa
wanapeleka watoto wao ama ndugu zao ambao siyo wanariadha.
"National College Athletics Association (NCAA) ya
Marekani ilikuwa inatoa nafasi 25 kila mwaka, lakini tulikuja kukosa nafasi
hizo baada ya baadhi ya viongozi kupeleka watoto wao ambao hawakuwa wanariadha,
“alisema na kuongeza:
“Mimi ni nmoja na wanafunzi wa mwisho kwenda Marekani
hivyo tutafanya mazungumzo na NCAA kuona kama tunapata tena hizo nafasi,"
anasema Gibabuday.
Gidabuday anasema kuwa wanafunzi wanariadha walikuwa
wanalipiwa kila kitu na vyuo hivyo na vyuo vilikuwa vinaona fahari pale
wanafunzi hao walipokuwa wakifanya vizuri kwenye michezo kwani ilisaidia
kukitangaza chuo.
Wanariadha ambao wamesoma kupitia mpango huo ni yeye
mwenyewe Gidabuday, Bayi, Mwinga Mwanjala, Makene, Suleiman Nyambui, Shahanga
na wengine wengi.
Gidabuday anasema wana imani kupata hizo nafasi za
masomo kwa sababu NCAA ilisema endapo Tanzania itapata viongozi wapya ambao
watathibitisha kupeleka walengwa watarudisha.
"Tunaamini tutapata hizo nafasi hivyo na sisi
itabidi tuingie makubaliano na wale ambao tutawapeleka kuwa sharti ni kurudi
nyumbani kusaidia michezo baada ya kuhitimu na siyo kuzamia," anasema.
Mashindano
ya Kimataifa
Tanzania ilikuwa ikipata mialiko mingi ya kushiriki mashindano
ya kimataifa, lakini ilipungua baada ya kuwa wanaopelekwa hawafanyi vizuri kwa
sababu waliokuwa wanakwenda walikuwa hawana sifa.
Gidabuday anasema IAAF ikitoa nafasi ya kushiriki
halafu ukafanya vibaya unapunguzwa maksi, lakini ukifanya vizuri pointi
zinaongezeka, hivyo kwa sababu Tanzania ilikuwa ikifanya vibaya nafasi
zilipungua.
Pia anasema kutopeleka wanariadha kwenye mashindano
pia kulisababisha kukosa pointi na kulazimika kulipa faini ambazo zilikatwa
kutoka kwenye mgao unaotoka IAAF.
"IAAF ilikuwa inatuma tiketi za ndege ambazo
hazijaandikwa majina, hivyo RT ilitumia mwanya huo kuweka watu wao hali
iliyosababisha kutofanya vizuri na nafasi zetu ziliongezewa Kenya hivyo tutahakikisha
tunawaandaa wanariadha wetu ili wakafanye vizuri, " anasema Gidabuday.
Kuna nafasi za wanawake, wanaume na walemavu, ambazo
Tanzania inatakiwa kupeleka wawakilishi au washiriki kwenye mashindano, lakini
tumeshindwa kuzitumia.
Gidabuday anasema April 2017 watapeleka wanariadha
nane nchini Uganda kwa ajili ya mashindano ya dunia ya mbio za Nyika.
Ufadhili wa
Riadha
Gidabuday anasema kwa kushirikiana na serikali
wanaamini watapata wafadhili kila mashindano kuanzia ngazi ya mkoa hadi Taifa.
"Kwa kushirikiana na makatibu tawala wa mikoa
tuna imani tutapata wafadhili kwenye mashindano mbalimbali hali itakayosaidia
kuinua riadha," anasema Gidabuday.
Pia Gidabuday anasema watamtumia balozi wa kampuni ya
vifaa vya michezo ya ASICS nchini, Juma Ikangaa kuomba ufadhili wa vifaa vya
michezo kwa wanariadha wa Tanzania.
"Tuna bahati Ikangaa ni balozi wa ASICS tangu
1984, hivyo tutaandika pendekezo letu kuomba kampuni hiyo itasaidie vifaa na
naamini tutapata kwa heshima ya Ikangaa," alisema Gidabuday.
Pia alisema pendekezo lao watalipeleka kwenye
makampuni mbalimbali hapa nchini na kwa kuwa anaaminika anaamini watapata
wafadhili kwa sababu tutajitahidi pia kuwapa elimu ya faida ya kufadhili
riadha.
"Wanariadha wanaweza kutangaza raslimali za nchi
hii kimataifa hata bidhaa za makampuni yetu hivyo elimu inahitajika kwa wadau
kufahamu faida zake," alisema Gidabuday.
Zawadi nono
imeua mbio fupi
Gidabuday anasema wanariadha wengi wameacha mbio fupi
na kukimbilia mbio ndefu kutokana na zawadi zinazotolewa kwenye mbio ndefu kuwa
na mvuto.
"Mbio fupi zimekosa washiriki kwa sababu wengi
wamekimbilia mbio ndefu kutokana na ubora wa zawadi zinazotolewa kwa washindi
na makocha kuhamasisha wanariadha kucheza mbio ndefu kwa kuangalia maslahi
kuliko kuendeleza vipaji," anasema Gidabuday.
Gidabuday anasema watajitahidi kuhamasisha mbio fupi
kwa wanariadha wachanga ili wasiogope mchezo huo na kuwapa faida za kuanza na
mbio fupi kwani miili yao inakuwa haijazoea shuruba.
Mikoa kupewa
kipaumbele
Gidabuday anasema RT itatoa kipaumbele kwa mikoa
inayotoa asilimia kubwa ya wanariadha wanaowakilisha nchi kimataifa huku
akitolea mfano mkoa wa Singida ambao umetoa wanariadha watatu walioshiriki
mashindano ya Olympiki iliyopita.
Anasema kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza ushindani
wa mikoa kutoa wanariadha bora.
Anasemaje
kuhusu safu mpya?
Gidabuday anasema uongozi mpya wa RT ni alama ya kuiondoa riadha hapa ilipo na kuipeleka
sehemu nyingine kwa sababu Mwenyekiti wao Anthony Mtaka ni kiongozi wa mfano.
"Mtaka amesaidia riadha hata nafasi ya tano
aliyopata mwanariadha wa Tanzania Alphonce Simbu katika Olimpiki ya Rio 2016 ni
juhudi zake, hivyo kwa kushirikiana na mimi naamini tutaipeleka riadha mahali, ambapo bendera ya Tanzania itaonekana,"anasema.
Gidabuday anasema Mtaka ni kiongozi mzalendo ambaye
anapenda michezo kutoka ndani ya moyo wake, hivyo kwa dhamira hiyo anaamini
riadha itarudi kama ilivyokuwa enzi za Filbert Bayi na Juma Ikangaa.
Gidabuday ni
nani?
Gidabuday ni mwanariadha wa zamani mwenye taaluma ya
elimu ya viungo kutoka Chuo Kikuu cha Life University, Atlanta, USA,1995/98
Elimu kidato cha tano na sita
alisoma Riverside California, USA. 1993/95.
Wakati elimu ya msingi
alisoma shule ya Msingi Nangwa 1980-1986 na kidato cha kwanza hadi cha nne
alipata shule ya Balang'da Lalu, Hanang 1988-1991
Gidabuday 1993/1994 California State Champion
in X/Country USA, 1994 alishiriki California
State meta 5,000 na meta 10,000 Champ USA, 1995 NCCA Runner-Up Milwaukee State
USA, Winner of 1998 Los Angeles Super Bowl 10k USA
Pia ni mshindi wa kwanza kwa
niaka mitatu mfululizo 2001/2002/2003 wa Los Angeles Revlon kilometa tano,
mshindi wa NIKE Run Los Angeles 2004.
Gidabuday kijana mwenye miaka
42, mzaliwa wa mkoa wa Manyara kutoka kijiji cha Dirma, Hanang ana mikakati
mizito ya kuhakikisha RT inasonga mbele hapa nyumba na kimataifa.
No comments:
Post a Comment