Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Thursday, October 6, 2016

POSI AKUNWA NA SERENGETI BOYS











NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Kazi Vijana na Walemavu Abdallah Possi amekiri kufurahishwa na mafanikio ya timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Boys licha ya kutolewa katika hatua ya mwisho ya kufuzu michuano ya vijana Oktoba 2 na wenyeji Congo Brazzaville.

Possi aliyasema hayo kwenye hafla ya chakula cha mchana na timu hiyo iliyofanyika kwenye ofisi za TFF zilizopo Ilala jijini Dar es Salaam ikiwa na maana ya kuwatia nguvu kwa kazi kubwa waliyoifanya pamoja na kushindwa kufuzu katika michuano hiyo.

Waziri Possi alisema kuwa Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri licha ya kukumbana na changamoto nyingi za uendeshaji lakini wamepanga kuwapiga jeki ili kuinua soka la vijana.

Aidha Possi aliwapongeza pia vijana hao kwa kujituma na kuweka utaifa mbele na kupambana kuhakikisha wanashinda ili kufuzu kwenye michuano hiyo itakayofanyika mwakani nchini Madagascar lakini bahati haikuwa upande wao.

"Nawapongeza vijana kwa kupambana hadi tone la mwisho wameonyesha uzalendo mkubwa kwa nchi yao, pia nawapongeza TFF kwa kuwatunza kwakuwa Serikali haiwezi kufanya kila kitu kutokana na majukumu iliyokuwa nayo," alisema Possi.

Rais wa TFF Jamal Malinzi alisema katika kipindi chake chote cha miaka 20 alichodumu katika medani ya soka hajawahi kuwa kwenye wakati mgumu kama Oktoba 2 ambapo alishuhudia timu ya Serengeti ikishindwa kufuzu kwa kutolewa kwa faida ya goli la ugenini na wenyeji Congo kwavile aliamini kulikuwa na nafasi ya vijana hao kusonga mbele.

Malinzi alisema mwezi ujao vijana hao wataenda Korea Kusini kwa ajili ya michuano itakayoshirikisha nchi sita ambayo itawaongezea uwezo wa kujiamini kucheza mechi za ugenini kwani ndiyo wanaandaliwa kuwa Ngorongoro Heroes kabla ya kuwa Taifa Stars siku za usoni.

No comments:

Post a Comment