Kocha msaidizi wa Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Salum Mayanga, (kushoto) akiongea na wandishi wa habari leo. Katikati ni kocha Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Mart Nooij na kulia ni kocha msaidizi wa Taifa stars, Mecky Mexime.
KOCHA wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Mart Nooij, amesema atatumia kambi ya Ethiopia kujiandaa na mchezo wa Misri kwani vijana wapo katika hali nzuri na wameahidi kupambana kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo.
Mart Nooij aliyasema hayo leo wakati ametangaza kikosi cha wachezaji 23 walioondoka jana jioni kuelekea Addis Ababa nchini Ethiopia kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri
“Nitatumia kambi ya Ethiopia kujiandaa na mchezo wa Misri, kwani wachezaji wapo katika hali nzuri na wameahidi kupambana kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo na baadae kufuzu katika fainali za Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2017”, alisema Nooij
Mchezo kati ya Misri na Tanzania wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2017unatarajiwa kuchezwa Juni 14, katika uwanja wa Borg El Arab jijini Alexandria.
Kikosi cha Stars kiliondoka jana saa 11 jioni kwa Shirika la ndege la Ethiopia ambapo kitawasili jiji la Addis Ababa majira ya saa 1 jioni kwa saa za Afrika Mashariki kina wachezaji 23, benchi la ufundi la watu wanne na wajumbe wawili wa kamati ya Utendaji ya TFF ambao ni Vedastus Lufano na Geofrey Irick Nyange “Kaburu”.
Wachezaji hao ni Deogratias Munish, Aishi Manula, Mwadini Ali, walinzi Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Aggrey Morris, Mwinyi Haji, Salum Mbonde na Juma Abdul.
Wengine ni Mwinyi Kazimoto, Abdi Banda, Salum Telela, Frank Domayo, Jonas Mkude, Said Ndemla, washambuliaji Saimon Msuva, John Bocco, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta,Mrisho Ngasa na Juma Liuzio
Naye mjumbe wa kamati ya Utendaji ya TFF Vedastus Lufano amesema timu inakwenda kuweka kambi Ethiopia kwa ajili ya kupambana katika mchezo dhidi ya Misri kujiandaa vema ili wafanye vizuri kwani watanzania wameanza kupoteza imani na timu yao.
Wakati huo huo kikosi kingine cha timu ya Taifa kitaondoka nchini siku ya jumamosi kuelekea nchini Rwanda kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya Rwanda wa kuadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya Kimbali.
Kikosi kitakachoondoka kwenda Rwanza kitakuwa na wachezaji 18 na kitakuwa na kocha Salum Mayanga, akisaidiwa na kocha Bakari Shime
Wachezaji watakaondoka ni Peter Manyika, Said Mohamed, Emmanuel Semwanda, Joram Mgeveke, Hassan Isihaka, Gadiel Michael, Hassan Dilunga, Rashid Mandawa, Atupele Green, Kelvin Friday, Hassan Kessy, Ibrahim Hajibu, Malimi Busungu, Mudathir Yahya, Deus Kaseke, Andre Vicent, Amri Kiemba na Mohamed Hussein.
No comments:
Post a Comment