MARA ZOTE TUMEKUA TUKIONA HAIWEZEKANI MPAKA PALE
TUNAPOONA WENGINE WAMEFANYA NA IMEWEZEKANA.
Ziara ya kutembelea kiwanda nchini CHINA kwa ajili ya kukubaliana utaratibu wa uzalishaji-Oct 2013
Hyasintha B.
Ntuyeko managing director of Kasole Secrets
company ltd, leo akisheherekea miaka 3 ya biashara yake.
Nilianza
biashara 6 Dec 2010 kwa mtaji wa
shilling 60,000/= ambao nilipatiwa
na Aunt yangu (Victoria Isangu) Mara
tuu baada ya kumaliza chuo.
Huu ndo ulikua mwanzo wa biashara, nilianza kufuata mzigo
mwenyewe Mombasa- 2011
Ni kweli kabisa
baada ya masomo ya chuo nilitumia muda wangu mwingi kuangalia series (kipindi
kile ilikua prison break) huku nikisubiri muda ufike nirudi nyumbani kusubiria
ajira.
Kwa kweli
sikuwahi kuota kufanya biashara, ndoto zangu zilikua kufanya kazi katika makampuni
makubwa ya mawasiliano huku nikiwa nimeshajipangia kiasi cha mshahara ambao
ningelipwa. Sasa hili wazo la biashara nililopewa na Aunt Vicky sikujua jinsi ya kulianza.
Aunt Vicky aliniambia
badala ya kukaa bure unaonaje kama ukiwa unauza hizi bidhaa ukajipatia hela
kidogo za matumizi? Ni kamuuliza sasa hii biashara inafanywaje? Akaniambia Ongea
na kila mtu unayekutana nae, hao ndo wateja wenyewe. Nikakubaliana nae,
akanilipia 60,000/= nikachukua pads( hizi
pads zilikua zikitengenezwa na mmea unaitwa leonorus) na vipodozi vingine vya gharama hiyo, Nikaondoka kuelekea
nyumbani (nilikua nikikaa na rafiki yangu kipindi hicho wakati nasubiria kurudi
nyumbani).
Hii ndio ofisi niliyoifungua na kuachana na biashara za kuzunguka
barabarani- July 2011
Hiyo siku
nilirudi nyumbani nikamuonyesha rafiki yangu akaniambia fanya ni kitu kizuri,
kesho yake nilikaa tuu nyumbani sikwenda popote, siku inayofuata nikaamua
kutoka kujaribu kuuza bidhaa zangu, nilianza na mwenge na nilitembea kwenye
maframe ya mwenge na kuongea hata na wapita njia, siku hiyo nilipata tsh
20,000/= Kwa kweli nilifurahi mnoo, kwanza nilishangaa inawezekanaje siku moja
tuu niweze kuzalisha tsh 20,000/=? Wakati nilikua na 20,000/= nimeihifadhi kwa
muda wa mwezi mzima kwa ajili ya kuitumia kama nauli muda utakapofika wa kurudi
nyumbani, sio siri nilikua siwezi hata kutoa sadaka kanisani nikihofia ikipugua
sitaweza kuongezea. Leo siku moja tuu nimepata 20,000/=? yaani nilijiona tajiri
sana. Sasa Nguvu ya kuifanya hii biashara ikapatikana.
muonekano mpya wa ofisi yangu July 2012
Watu
walioniagiza niwaletee bidhaa kesho yake walikua wengi hivyo nikampigia Aunt
Yangu kumueleza kua nina oda za watu na hela iliyopo mkononi haitatosha,
akaniongezea tsh 90,000/= nikafuata kununua mzigo kwa rafiki yake (Mama Mbise) kisha nikaendelea na
biashara, kwa kweli ilikua nzuri sana, nilizidi kutembea na kuziuza vyuoni pia.
Nilipata wateja wengi sana kiasi Mama
Mbise (rafiki yake aunt yangu) hakuweza tena kuniuzia mzigo, akanielekeza
niwe ninaufuata mwenyewe Mombasa-Kenya.
VIKWAZO
Binafsi hua
ninavichukulia Vikwazo/changamoto kama ni shule pekee ya mjasiliamali, hakuna
njia nyingine yeyote ambayo mjasiliamali anaweza kuongeza ujuzi na uzoefu kama
hata kumbana na vikwazo vyovyote katika biashara yake.
Kikwazo cha
awali nilichokumbana nacho ni kutoka kwenye kikundi cha sala (fellowship)
nilichokua ninasali , ninapenda kusali hivyo hua ninajishughulisha na shughuli
zozote zinazonifanya niwe karibu na Mungu.
Niliwashirikisha
biashara baadhi ya marafiki zangu niliokua ninasali nao kikundini, walivutiwa
na wenyewe wakawa watumiaji, muda mchache nikaona wameacha kutumia na kila
nikiwauliza hawakunipa majibu ya moja kwa moja, siku moja mmoja wa niliowapa
bidhaa zangu akaniambia, unajua Hyasintha tumeacha kutumia bidhaa zako
kwasababu zinahusiana na FREEMANSON, eeeh! Nilishangaaa sana, nikamuuliza ili
anieleweshe, akanipa Maelezo ambayo kichwani kwangu hayakukubalika hata kidogo,
nikamwambia sawa, we acha kutumia na kuifanya hii biashara ila acha mi niifanye
siku moja mtanitumia mimi kama mfano.
Siku chache
baadae viongozi kadhaa wa fellowship waliniita kunikanya kuhusu hii biashara
yangu na kunitaka nimuombe Mungu anitafutie kazi nzuri, kwa kweli sikuwaelewa
kabisa nikaamua kuendelea na biashara kwani niliamini kama mimi pia ninasali
basi ninauwezo wa kugundua la Mungu na la shetani.
Nikiwa chuo
nakumbuka kuna mgomo wa wafanyakazi uliwahi kutokea, RAIS alihutubia akasema
“ AKILI ZA MGAYA CHANGANYA NA ZA KWAKO” huu msemo niliupenda sana, hivyo hata katika kikwazo hiki ulikua
ukinifariji mno. Ni kweli kama nisingeamua kwa busara, ndoto yangu ingezimikia
pale.
Baada ya kunogewa na biashara nilisahau kabisa
swala la kutuma barua za maombi ya kazi, hivyo kujikuta ninaingia matatani na
familia, Ndugu na jamaa walinilaumu kwa kutotafuta kazi na kufanya biashara
isiyoeleweka, nina mshukuru sana Mama
Mbise (Rafiki wa Aunt Yangu) ambaye yeye alikua ni mshauri wangu mkuu na alinitia
moyo mno nikaweza kuishinda hii changamoto. Hivyo katika biashara yoyote tunahitaji
mshauri ambaye ataweza kutuelekeza njia na kutushika mkono, ni vyema kuchagua
mshauri sahihi, si kila mtu anaweza kukushauri katika biashara yako, wengine
wanaweza kukufanya ukate tamaa kabisa na kupoteza mwelekeo.
Biashara yangu
ilienda vizuri sana na ilipanuka, nikatoka hatua moja kwenda nyingine, kutoka mmachinga hadi kufungua ofisi na kukaa
mahali pamoja sasa.
nikiwa Nairobi kukubaliana na hiyo kampuni kuhusu kupata mzigo moja kwa
moja Tanzania, dada aliyevaa hijabu ni rafiki yangu, waliobaki ni
administration ya hiyo kampuni. NAIROBI-KENYA 2011
Hapa sasa
nikapambana na changamoto nyingine, kampuni iliyokua ikiniuzia bidhaa kutoka
Nairobi wakaanza usumbufu wa kutoleta bidhaa, wanaweza chelewesha bidhaa kwa
zaidi ya miezi mitatu hadi minne na mimi ninawateja na sina biashara nyingine
ninafanya hapa mjini ni hiyo tuu. Nikaanza kuingia ugomvi na wateja kwa
kushindwa kuwapa bidhaa kwa wakati. Niliudhika sana, Changamoto hii ilinifanya
nikae chini nifikirie na mimi kua na kitu changu mwenyewe na si kutegemea watu
wengine ambao sijui ghala lao lina ukubwa gani. Hapo ndipo wazo la pads za mkaa wa mianzi lilipozaliwa,
Nilitumia muda
wangu mwingi kusoma na kutafuta kwa kina kuhusu mkaa wa muanzi na vipi
unahusika na afya ya uzazi ya mwanamke, nilipanda milima na mabonde kuhusiana
na jambo hili bila
kukata tamaa
kamwe. Baada ya kujiridhisha nilifungua kampuni yangu ya KASOLE
SECRETS, 18TH Feb 2013.
Kasole ni jina
langu nililopatiwa na Baba yangu likiwa na maana ya “kitu kizuri” na niliweka neno “Secrets”
likiwa na maana ya siri, Neno Siri linatokana na historia yangu hasa jinsi
nilivyoanza kufanya biashara, hivyo “Kasole
secrets” Inatafsiriwa kama “SIRI
NZURI” Siri zilizopo katika kujiamini, kua na msimamo, kuthubutu kufanya
jambo bila kusita, kujituma, kutodharau fursa na kutokata tamaa.
Hapa nikiwa katika moja ya supermarket nikizinadi pads
zangu, sikua bado na uwezo wa kutengeneza sare yangu, lakini sikukata tamaa
Glory Girl pads
ni pad bora ya afya iliyowekwa mkaa wa muanzi wenye kufyonza sumu, kuimarisha
kinga ya kizazi na mzunguko wa hedhi, kukuondolea maumivu makali ya tumbo na
viungo kabla na wakati wa hedhi.
nikiwa kwenye maonyesho ya sabasaba JULY-2013
Mpaka sasa nimeweza
kusambaza zaidi ya sehemu 40 jijini Dar na hata nje ya Dar kwa mikoa kama
KILIMANJARO, ARUSHA, MWANZA, MBEYA NA DODOMA.
Hapa nikiwa ninafundisha kina mama juu ya pads za muanzi. FEB 2013
picha baada ya kufundisha kikundi cha wajasiliamali juu
ya pads za Muanzi, MARCH 2013
Tembelea page yetu ya facebook ya Amani bamboo uweze
kupata taarifa zaidi
NINAPOKUA NIKIADHIMISHA MIAKA HII 3, NINAPENDA
KUSEMA..........
Kila kitu
kinawezekana kufanyika kama kweli tukiweka nia, Hatukuamini kama South Afrika
ingeweza kutawaliwa na waafrika wenyewe, lakini NELSON MANDELA alituaminisha kua inawezekana baada ya yeye
kuitawala South Afrika, Hatukuamini kama Rais mwenye asili ya Kiafrika angeweza kuingoza Marekani mpaka OBAMA aliposhinda Urais, pengine
hatuamini vitu vingi kama sisi binafsi tunaweza kufanya na hivyo kutothubutu kujaribu
kabisa.
Tunaweza kuleta
mabadiliko na kufanya maajabu, tunaweza kuishi maisha yoyote tunayoyataka,
tunaweza kua wafanya biashara wakubwa hapa Duniani, njia rahisi nikufikiria
nini Ufanye na ukifanye vipi, swala la mtaji
utalifikiria baadae baada ya kupata majibu ya nini ufanye na ukifanye
vipi.
Binafsi ninawaahidi
kipindi kingine nitakapokua ninasheherekea miaka kadhaa ya Glory Pads nitakua
nimeweza kuifanya glory pads kua international brand..........
nikiwa nimevalia vizuri kabisa tayari kuingia ndani kabisa katika
mitambo yao ya uzalishaji ili kuweza kuona ni jinsi gani wanafanya kazi- CHINA
NOV 2013
INAWEZEKANA
JAMANI..... Tembelea ukurasa wetu wa facebook uitwao amani bamboo
No comments:
Post a Comment