Shirikisho liko kwenye hatua za mwisho za mchakato wa
Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 26/27 Oktoba 2013 hapa jijini Dar es
salaam.
Hivi sasa, wagombea
wanasubiri vyombo vya juu vya uamuzi kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mwisho kabla
ya kuanza kampeni na hatimaye uchaguzi.
Hata hivyo, baada ya Kamati
ya Maadili kufanya uamuzi dhidi ya kesi nane zilizowasilishwa mbele yake,
Sekretarieti imeona kuwepo kwa ukakasi katika utekelezaji wa uamuzi huo
kutokana na ukweli kuwa kuna baadhi ya mambo yanaonekana kuwa na ugumu katika
kuyatekeleza.
Sekretarieti si chombo
chenya mamlaka ya kutafsiri uamuzi wa vyombo huru vya Shirikisho, kazi yake
kubwa ni kupokea uamuzi na kuutekeleza, hivyo kwa kuwa kuna ukakasi huo imeamua
kuwasilisha uamuzi huo kwenye Kamati ya Rufani ya Maadili kwa ajili ya
kuufanyia mapitio (revision) na pia kutoa mwongozo kabla ya kurejesha uamuzi
huo kwenye Kamati ya Uchaguzi kwa ajili ya kuendelea na mchakato.
Sekretarieti imefanya hivyo
kwa lengo la kusaidia wagombea ambao wengi wanaonekana kuwa njia panda baada ya
kupokea uamuzi wa Kamati ya Maadili na kuiuliza Sekretarieti kuwa inakuwaje
Kamati ya Maadili iwaone hawana hatia, lakini hapo hapo ikubaliane na uamuzi wa
kuwaengua, jambo ambalo kwa kweli limetufanya tukose majibu sahihi na hivyo
kuamua kuomba revision na mwongozo.
Pia mwongozo utakaotolewa na
Kamati ya Rufani ya Maadili utasaidia kuweka mwelekeo mzuri wa masuala ya
Maadili katika siku zijazo.
Miongoni mwa mambo
yanayoonekana kuwa na ukakasi ni kuwaona watu wote ambao kesi zao
ziliwasilishwa kwenye Kamati ya Maadili hawana hatia, lakini hapo hapo
kukubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi wa kuwaengua baadhi yao kwa sababu
za kinidhamu ikisema haiwezi kuwahukumu mara mbili kwa kuwa wameshaadhibiwa kwa
kuenguliwa kwenye uchaguzi.
Ili haki itendeke na ionekane inatendeka, Sekretarieti
imeona ni vizuri masuala hayo yakafanyiwa revision (mapitio) na kutolewa
mwongozo ili kuondoa ukakasi uliojitokeza miongoni mwa wagombea, Shirikisho na
wadau na hivyo kujenga hisia kuwa kuna mbinu zimefanyika dhidi ya baadhi ya
wagombea.
Uamuzi huu haumaaniishi kuwa
Sekretarieti inapingana na uamuzi wa Kamati ya Maadili, bali ni utaratibu wa
Sekretarieti kuomba ufafanuzi au mwongozo kutoka vyombo husika pindi inapotokea
ukakasi katika utekelezaji wa uamuzi wa vyombo vya uamuzi vya Shirikisho.
Sekretarieti imeshamwandikia
Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani za Maadili ili aitishe kikao kwa manajiri ya
kufanya mapitio na kutoa mwongozo ambao utasaidia Shirikisho kuendelea na
uchaguzi bila ya ukakasi.
No comments:
Post a Comment