BUCHAREST, Romania
KOCHA, Jose Mourinho ameshikwa na kigugumizi kwenye mkutano na
waandishi wa habari, baada ya kutupiwa swali kuhusu kutomchezesha nyota wake, Kevin
de Bruyne ambaye anadai kuwa anaona amekuwa akichukuliwa kama mtoto mdogo.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Star, kocha huyo wa
Chelsea alibwatuka usiku wa kuamkia jana katika mkutano na waandishi wa habari wakati akizungumza
kuhusu mechi ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya timu ya Steaua
Bucharest, baada ya kutwangwa swali hilo kuhusu nyota huyo raia wa Ubelgiji.
Kwa sasa, De Bruyne anafanya mazoezi na timu ya watoto
wakati kikosi cha timu ya wakubwa kikiwa safarini nchini Romania na kuna
taarifa zinazoeleza kwamba, yupo tayari kuondoka wakati wa usajili wa dirisha
dogo litakapofunguliwa mapema Januari,
baada ya kukwaruzana na Mourinho.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vilivyopo karibu na
mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, nyota huyo kwa sasa haridhishwi na jinsi
anavyochukuliwa na anajihisi kama anafanywa kama mtoto.
De Bruyne anakuwa mchezaji mpya kukwaruzana na
Mourinho, ambaye msimu huu amekuwa akimsugulisha benchi, Juan Mata na
alipohojiwa kuhusu mchezaji huyo juzi kocha huyo alibwatuka na kuondoka kwenye
mkutano wa waandishi wa habari.
“Kevin hayupo mahali hapa na ni uamuzi wangu na
mtazamo wangu,” alisema kocha huyo huku akionekana kuchukizwa na swali hilo.
“Hii ni ajabu kwani hakuna hata mtu mmoja ambaye
anauliza kuhusu Mata. Wiki tatu zilizopita, mlikuwa mkizungumza kuhusu Mata,
lakini kwa sasa mmegeukia kuhusu Kevin,” aliongeza kocha huyo.
Alisema kuwa anawashangaa kuona wakizungumzia kuhusu
mchezaji ambaye hachezi ama kuchaguliwa ndani ya timu na akasema kuwa huo ni
uamuzi wake, kwani kwenye timu ana wachezaji 11 ambao wanaweza wakacheza na
amekuwa akiwateua kwa kuangalia kile ambacho wanakifanya uwanjani na mazoezini.
Katika usajili wa majira haya ya joto, De Bruyne alikuwa
anawindwa na timu za Bayer Leverkusen, Schalke na Borussia Dortmund lakini akawekewa
ngumu na baba mzazi wa nyota huyo, Herwig De Bruyne alisema usiku wa kuamkia jana
kuwa watalipatia ufumbuzi suala hilo wakati wa usajili wa dirisha dogo
litakapofunguliwa mapema Januari mwakani.
@@@@@@@@@@@@@@@
Benitez amfagilia Wenger
LONDON, England
KOCHA Rafa Benitez amemmwagia sifa
kocha wa Arsenal, Arsene Wenger akisema kuwa ndiye kocha bora kuliko wote
wanaofundisha kwenye michuano ya Ligi Kuu ya England.
Benitez alitoa kauli hiyo mapema
jana, wakati timu yake ya Napoli ikijiandaa kuivaa klabu hiyo ya Emirates
katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
Katika mkutano na waandishi wa
habari wa kuzungumzia mtanange huo uliopigwa usiku wa kuamkia leo, Benitez
alimpotezea Kocha wa Chelsea, Jose
Mourinho akisema kuwa kocha mkuu huyo wa Arsenal ndiye kinara kwenye soka la
Uingereza.
"Wenger ni kocha mkubwa, ni mtu
mashuhuri na ni mmoja kati ya watu wanaolifahamu soka la Uingereza.
"Ana uzoefu mkubwa Ulaya kwani
Arsenal mara zote imekuwa kati ya timu nne bora na amekuwa akifanya kazi kubwa
na huku akisajili wachezaji wazuri. Kwa hatua hii kila kitu kwake kimekuwa kikienda
sawa,” aliongeza kocha huyo.
No comments:
Post a Comment