WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mjini Morogoro, juzi
wameibuka mabingwa wa mashindano ya pool yanayoshirikisha Vyuo vya Elimu ya Juu
na kudhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Safari
Lager, baada ya kuifunga Chuo cha Ardhi magoli 13-9 kwenye Ukumbi wa Vijana.
Kwa ushindi huo, Mzumbe walijinyakulia Sh 500,000 huku Ardhi
wakipata Sh 300,000 kwa kuwa mshindi wapili na Chuo cha Uandishi wa Habari
Morogoro (MSJ), kikishika nafasi ya tatu na kupata Sh 200,000, Chuo cha SUA
wakishika nafasi ya nne na kupata Sh 100,000.
Kwa Upande wa nafasi ya mtu mmoja mmoja wanaume, George Tito
kutoka SUA aliibuka kidedea na kutwaa
nafasi ya ubingwa wa mkoa baada ya kumshinda mpinzani wake Kiloya Kafuna
kutoka Chuo cha Mzumbe kwa magoli 3-2 na kujipatia Sh 150,000.
Kwa upande wa wanawake Salome Eliudi, kutoka Chuo cha
Mzumbe alishiaka nafasi ya kwanza na kupata Sh 100,000 baada ya kuwashinda
wenzake wawili aliokuwa akichuana nao.
Hivyo mshindi wa kwanza wa timu katika shindano hilo,
atapata fursa ya kushiriki mashindano hayo ngazi ya Taifa na mtu mmoja
mmoja upande wa wanaume atauwakilisha mkoa kwenye michuano hiyo inayotarajia
kufanyika mwezi ujao ujao jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa mashindano hayo, Naibu Meya wa
Manispaa ya Morogoro, Lidya Mbiaji, aliwataka wanafunzi hao kuzingatia masomo
kwanza ndiyo michezo ifuate.
Aliwataka viongozi wa mchezo huo mkoani hapa na maeneo
mengine, kutenga muda maalumu wa kucheza mchezo huo, ili kutoa nafasi ya
kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo, badala ya kuundesha kwa nyakati
zote kama ilivyo sasa.
No comments:
Post a Comment