Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, February 12, 2013

WAMBURA, MALINZI NJE KWENYE KINYANGANYIRO CHA UCHAGUZI WA TFF

Mwenyekiti wa kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF Iddi Mtingijola akitoa maamuzi ya kamati yake baada ya kupitia rufaa mbalimbali zilizowasilishwa mbele ya kamati yake baada ya kamati ya uchaguzi ya TFF kuwaengua baadhi ya wagombea lakini pia rufaa nyingine za wadau mbalimbali waliopinga kamati ya uchaguzi kuwapisha baadhi ya wagombea.

Waandishi wa habari wakifuatilia maamuzi ya kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF yaklisomwa na mwenyikiti wa kamati hiyo Iddi Mtinginjola.
Wajumbe wa kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF wakifuatialia kwa makini maamuzi ya kamati yao toka kwa mwenyekiti wao.
 
BAADA ya kuketi kwa siku mbili kupitia na kusikiliza rufaa mbalimbali zilizo katwa kwenye kamati ya rufaa ya uchaguzi ya shirikisho la soka nchini TFF, hatimaye kamati hiyo imetoa maamuzi yake.

Kabla ya kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF kuketi kwa siku mbili, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua waombaji kumi na mbili wa uongozi kwenye nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo utakaofanyika Februari 24 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa kutokidhi matakwa ya kikatiba. 
 Waombaji hao waliochujwa ni Omari Mussa Nkwarulo aliyeomba kuwania urais na Michael Richard Wambura aliyejitosa katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Makamu wa Rais.
Wengine waliochujwa wakiomba kugombea nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Abdallah Hussein Musa, Mbasha Matutu, Charles Mugondo, Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja, Eliud Peter Mvella, Farid Nahdi, Omari Isack Abdulkadir na Shafii Kajuna Dauda.

Kwa upande wa uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu aliyechujwa ni Christopher Peter Lunkombe aliyekuwa akiomba nafasi ya ujumbe katika Kamati ya Uendeshaji.

Hata hivyo baadaye kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF ilipokea rufaa mbalimbali kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuhusiana na uchaguzi utakaofanyika Februari 22 na 24 mwaka huu.
 
Waliowasilisha rufani mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Iddi Mtiginjola ni pamoja na waombaji uongozi saba walioenguliwa katika kinyang’anyiro hicho. Warufani hao ni Omari Mussa Nkwarulo na Michael Richard Wambura walioomba kugombea urais na umakamu wa rais.

Wengine ambao waliomba ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda mbalimbali ni Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Omari Isack Abdulkadir (Dar es Salaam), Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya) na Shaffih Kajuna Dauda (Dar es Salaam).

Warufani wengine ni wadau ambao waliweka pingamizi dhidi ya baadhi ya waombaji uongozi katika TPL Board na TFF, pingamizi ambazo zilitupwa mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa sababu za kiufundi.

Wadau hao waliokata rufani ni Agape Fue dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Jamal Malinzi kugombea urais, Medard Justinian dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Athuman Nyamlani kugombea urais, na Frank Mchaki dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Hamad Yahya kugombea uenyekiti wa TPL Board.

Majibu ya kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF chini ya mwenyekiti wa Iddi Mtingijola yaliyotolewa mbele ya waandishi wa habari usiku ni kama ifuatavyo.
Kanda ya Dar es Salaam rufaa ya Shafii Dauda imeshinda na hivyo basi jina lake limerudishwa katika kinyanyiro cha uchaguzi na kwamba maamuzi ya kamati ya uchaguzi yametengeluliwa.
Kanda ya Dar es Salaam, Omari Abdulkadiri rufaa ya yake imeshindwa na hivyo maamuzi ya kamati ya uchaguzi yamebaki kama yalivyo.
Faridi Mbaraka Salim Nahdi rufaa yake imeshindwa kwa kushindwa kutofautisha miaka yake ya kuzaliwa kati 1966 na kuonekana amezaliwa 1972 .
 
Eliudi Peter Mvela rufaa yake imeshindwa kwasababu ya kutokuwajibika kwenye kamati ya utendaji akiwa mjumbe wa kamati ya utendaji alipashwa kutetea kile walicho kubaliana ndani ya kamati ya utendaji lakini alikwenda kinyume na kile walichokubaliana ndani ya kamati ya utendaji kwa mujibu wa ibara 36(3) ya katiba ya tff na ibara ya 12(1)(b)(d).

Kanda ya Shinyanga Mbasha Matutu rufaa yake imeshindwa kwa kuingilia mchakato wa uchaguzi kushiriki kuandaa pingamizi dhidi ya mgombea mwenzake kwani imethibitika alishiriki kutaka wenzake washindwe, hivyo alikosa uadilifu kwa mujibu wa kifungu namba 9(7) cha katiba ya TFF.
 
Mwenyekiti wa bodi Ahmed Yahya aliwekewa pingamizi kuwa yeye si mwenyikiti halali wa Mtibwa Sports klabu , kamati imeaangalia katiba ya Mtibwa imeonekana kuwa mwenyekiti aliaacha madaraka yake na madaraka yake yakaenda kwa makamu mwenyekiti ambaye alikuwa na mamlaka ya kuitisha mkutano ambao ndio ungemchagua mwenyekiti na kuendelea mpaka mkutano mwingine.
Kwa mujibu wa katiba ya Mtibwa makamu mwenyekiti alitakiwa kuitisha mkutano wa kumchagua lakini badala yake alikwenda kwenye bodi na kumkasimu madaraka ya mwenyekiti jambo ambalo si halali kwa mujibu wa katiba ya Mtibwa, hivyo kamati imebaini kuwa si mwenyekiti wa halali wa Mtibwa.

 Kwa upande wa rufaa ya Michael Richard Wambura ambaye anawania nafasi ya makamu wa Rais imeshindwa kwasababu hana sifa ya uadilifu.

Mtiginjola amesema amri iliyotolewa na kamati ya rufaa ya jaji Mkwawa haijabadilishwa mpaka sasa na kwamba maamuzi ya kamati ya jaji Mkwawa kwamba Wambura hana uadilifu yako palepale.

Mtiginjola amesema Wambura alitakiwa kudai haki yake kupitia mahakama ya michezo ya kimataifa (CAS), kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya kamati ya jaji Mkwawa.
Katika nafasi ya Rais, mkata rufaa Omari Mussa Mkwaruro, rufaa yake imeshindwa kutokana na kuonekana hana upeo wa kutosha juu ya mambo ya soka na kutokuijua katiba ya TFF.
Mkwarulo alishindwa kujibu hata swali la mipango yake ya baadaye endapo atashinda kiti cha Rais wa TFF, ambapo alitoa majibu ya kushangaza kwani alisema ataanzisha mashindano ya soka ambayo yatakwenda mpaka Malawi na watu wenye mabasi ndio watakao peleka wachezaji, jambo ambalo liliishangaza kamati yake, hivyo kamati imeona kuna udhaifu mkubwa wa upeo wake katika masuala ya soka na katiba ya TFF.

Kwa upande wa rufaa aliyokatiwa Jamali Emily Malinzi, ni mwamba Malinzi amekosa sifa ya uzoefu katika uongozi wa kujishughulisha na mambo ya soka kwa kipindi mfululizo cha miaka 5 kwa mujibu wa kifungu cha 9(3) , licha ya kwamba kuna ushahidi kuwa alikuwa katibu wa Yanga kutoka 2003 mpaka 2006 mwenyekiti wake alikuwa Fransis Kifukwe, lakini hajatimiza miaka 5.

Ushahidi mwingine ni kuwa yeye kama mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Kagera nafasi ambayo aliipata mwaka jana bado hajatimiza miaka 5 na pia hakuna ushahidi mwingine wowote ulionyesha kuwa amekuwa kiongozi wa michezo sehemu nyingine yoyote.
Pili katika suala la uadilifu kuna taarifa kuwa Malinzi alipinga kuunga mkono maamuzi na maagizo ya shirikisho la soka duniani FIFA ambayo yanawataka wanachama wake ikiwemo TFF kufanya mabadiliko katika katiba zao kwa kuundwa kamati mbalimbali ndani kama vile kamati ya rufaa ya uchaguzi, jambo ambalo lilikuwa ni maagizo ya FIFA, Malinzi akiwa kiongozi wa soka wa mkoa wa Kagera ambao ni wanachama wa TFF alipingana na mabadiloko hayo ambapo aliwaita waandishi wa habari kuelezea juu ya pingamizi hilo.

Kwa mujibu wa Mtinginjola amesema kamati yake iliona kuwa hatua hiyo ya Malinzi endapo atachaguliwa kuwa Rais atarejesha nyuma TFF katika kipindi ambacho FIFA ilitaka kuifungia TFF kwa sababu za kukinzana na maamuzi yake jambo ambalo Malinzi kama mgombea anakosa sifa chini ya ibara 9(3) cha katiba ya TFF.

 Malinzi amekosa sifa chini ya vifungu mbalimbali ikiwa ni pamoja vifungu vya uchaguzi 9(3) kifungu namba 29, 39(3), 12(b)(d) na kwamba vifungu hivyo vimevunjwa, hivyo rufaa dhidi yake iliyokatwa na Agape Fueyake imeshinda.

Rufaa dhidi ya Athumani Nyamlani imeshindwa kutokana na mrufani kushindwa kutoa ushahidi na maelezo ya kina juu ya kile alichokuwa anakipinga dhidi ya Athumani Jumanne Nyamlani.
Medard Justinian alikata rufaa dhidi ya Nyamlani kwa madai ya kutokuwa muadilifu kwani Nyamlani aliisababishia hasara TFF kwa kuisababisha mamlaka ya mapato Tanzania TRA kuipiga faini ya TFF jambo ambalo Medard alishindwa kulithibitisha mbele ya kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF kwa kutoa hoja na vielelezo juu ya madai yake hayo.

 Shauri la pili dhidi ya Nyamlani ilikuwa ni mrufani kuona kwamba Nyamlani ni mtumishi wa serikali kama hakimu hivyo haitakuwa sahihi kwa Nyamlani kuitumikia TFF wakati huohuo akiwa pia ni mtumishi wa serikali kama hakimu akihoji ikiwa Nyamlani atahamishwa kituo cha kazi na kupelekwa nje ya mkoa wa Dar es Salaam itakuwaje, jambo ambalo limepigwa kumbo na kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF, kwani kwasasa bado Nyamlani ni makamu mwenyekiti wa TFF nafasi ambayo ameitumikia akiwa ni hakimu na hakuna malalamiko yoyote yaliokuja kwamba ameshindwa kazi zake akiwa hakimu na akiwa makamu wa mwenyekiti wa TFF, hivyo kamati ya rufaa ya TFF imeitupilia mbali rufaa hiyo dhidi ya Athumani Jumanne Nyamlani.

No comments:

Post a Comment