Uongozi wa klabu ya Simba umewaondoa kwenye kikosi cha timu hiyo
kinachoshiriki mashindano ya kombe la mapinduzi, Juma Kaseja aliyeomba
kupumzika na Mrisho Ngasa kutokana na kuwa majeruhi.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala,
amesema kuwa wamewatoa wachezaji hao kwenye mashindano haya kutokana na
kuwa majeruhi.
"Kaseja na Ngasa hawatakuwepo kabisa kwenye mashindano ya Mapinduzi
kwa sababu ni majeruhi na pia Kaseja aliomba kupumzika na uongozi
umeliangalia hilo na kuamua kuwaondoa kikosini," .
Aidha, amesema kuwa benchi la ufundi limekubaliana na maamuzi hayo
ya kuwaondoa kwenye kikosi kinachoshiriki mashindano ya Kombe la
Mapinduzi yaliyoanza wiki hii mjini Zanzibar.
Awali, Kaseja aliuandikia barua uongozi wa timu hiyo kuomba kupewa
miezi mitatu ya kupumzika kutokana na kucheza michezo mingi mfululizo
akiwa na klabu yake hiyo pamoja na kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa
Stars'.
Simba kwa sasa inashiriki mashindano ya Mapinduzi ambapo Meneja wa
timu hiyo, Jamhuri Kihwelo alisema kuwa mashindano yataisaidia timu yake kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa
mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara.
Alisema kuwa Simba ina wachezaji wengi chipukizi hivyo michuano hiyo
ya kombe la mapinduzi itawapa nafasi kuonyesha uwezo wao.
Awali kulikuwa na taarifa kuwa kikosi cha timu hiyo kitaenda kuweka
kambi nchini Oman kujiandaa na mzunguko wa pili lakini ushiriki wao
katika michuano hiyo ya kombe la Mapinduzi ni wazi huenda safari hiyo
isiwepo kwa kuwa mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara umepangwa
kuanza Januari 19 mwaka huu.
Wakati Simba wakishiriki katika michuano hiyo, watani wao, Yanga
wenyewe wapo nchini Uturuki walipokwenda kuweka kambi kujiandaa na
mzunguko wa pili wa ligi kuu.
No comments:
Post a Comment