|
Msemaji wa Simba Ezekiel Kamwaga. |
26/12/2012
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KHERI ya Krismas na Mwaka mpya kwenu nyote.
Uongozi wa klabu ya Simba leo unapenda kutoa taarifa ifuatayo kwenu.
- Mkutano
wa Wanachama uliopangwa kufanyika Desemba 30 mwaka huu.
UONGOZI umepata taarifa kuwa kuna kundi la wanalojiita
wanachama wa Simba waliopanga kufanya mkutano wa wanachama siku ya tarehe 30
Desemba mwaka huu (Jumapili hii) kwa lengo la kujadili mambo ya klabu.
Mkutano huo, kwa mujibu wa Katiba ya Simba ni batili.
Ubatili huo unatokana na ukweli kwamba wale walioutisha mkutano huo hawana Locus Standi (nguvu au mamlaka) ya
kufanya hivyo. Katiba ya Simba iko wazi kuwa mtu anayeitisha mkutano wa
wanachama ni MWENYEKITI wa klabu pekee na si vinginevyo.
Mkutano huo wa wanachama haujaitishwa na Mwenyekiti wa klabu
na hivyo hauna uhalali wowote wa kisheria.
Uchunguzi uliofanywa na klabu umebaini kwamba zaidi ya nusu
ya walioitisha mkutano huo pia si wanachama halali wa Simba. Wengine hawajawahi
kulipa ada zao za uanachama katika kipindi cha hadi miaka 10 iliyopita !
Matendo yanayofanywa na kundi hili yanaashiria watu
wanaotaka tu kuleta vurugu klabuni. Kundi hili linafanya hivi wakati Rais
Jakaya Kikwete ametoka kutoa kauli kuhusiana na namna vurugu zinavyosababisha
kushuka kwa michezo hapa nchini.
Kundi hili linaandaa vurugu katika kipindi ambacho uongozi
upo katika mikakati kabambe ya kuiboresha timu ikiwamo kuipeleka nje ya nchi
kufanya mazoezi, jambo ambalo halijawahi kufanyika katika kipindi cha miaka 20
iliyopita.
Linaandaa vurugu katika kipindi ambacho Simba ndiyo bingwa
mtetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania
na ikiwa imeongoza ligi katika msimu huu kuanzia mechi ya kwanza hadi ya 11
katika mechi 13 za kwanza.
Klabu inaomba wapenzi na wanachama wake kukaa mbali na kundi
hili la waleta vurugu. Huu ni wakati ambapo tunatakiwa kuwa pamoja kwa vile
klabu inatakiwa kutetea ubingwa wake na pia kuliwakilisha taifa katika michuano
ya kimataifa mapema mwakani.
Huu ni wakati wa wanachama, wapenzi na uongozi kuwa kitu
kimoja. Uongozi uko tayari kukosolewa wakati wowote ule lakini haukubaliani na
waleta vurugu.
Uongozi unapenda kusisitiza lifuatalo, Mkutano wa Desemba 30
ni batili na wale wote wenye mapenzi mema na klabu wanatakiwa kukaa mbali nao
na kutojihusisha kwa chochote na wanaopanga vurugu.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
No comments:
Post a Comment