Simba
imeanza vyema msimu mpya wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara kwa kutwaa Ngao ya
Jamii kwa kuichapa Yanga kwa penalti 5-4 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Alikuwa mshambuliaji
Mohammed Ibrahim Mo aliyeamsha shangwe, vifijo na nderemo za mashabiki wa
Simba kwa bao la ushindi.
Mo alifunga penalti ya tano kwa Simba na
kuhitimisha upigaji penalti ulioiacha Yanga ikiishia kupata penalti nne.
Pamoja na kuanza kupiga penalti huku Simba
ikimalizia, Yanga ilikosa fursa ya kubeba ngao hiyo baada ya mshambualiji wao,
Mahadhi kukosa penalti ya sita kabla ya Mo kufunga.
Hatua ya kupigiana
penalti ilikuja baada ya timu hizo kucheza dakika 90 za kawaida na kutoka suluhu,
licha ya kosa kosa kadhaa kila upande.
Ushindi huo wa Simba
umeifanya itwae kwa mara ya pili Ngao ya Jamii. Kinara ni Yanga mwenye ngao nne
za jamii na Azam moja.
Kabla ya Mo kufunga
penalti ya mwisho, Mahadhi alikosa kwa Yanga na kumaliza matumaini ya Yanga
kuweka historia nyingine.
Wengine waliopata
penalti hizo kwa upande wa Simba ni Method Mwanjali, Emmanuel Okwi, Haruna
Niyonzima na Shiza Kichuya.
Mohammed Hussein
'Tshabalala' ndiye peke yake alikosa penalti kwa Simba baada ya kipa wa Yanga,
Youthe Rostand kupangua shuti lake.
Kwa upande wa Yanga,
Kelvin Yondani na Juma Mahadhi walikosa. Shuti la Yondani lilidakwa na kipa
Aishi Manula huku Mahadhi akipaisha mpira kutokana na wasiwasi wake.
Waliopata penalti kwa
Yanga ni Kabamba Tshitshimbi, Thaban Kamusoko, Ibrahim Ajibu na Donald Ngoma.
Timu hizo ziliendelea
kupigiana penalti zaidi baada ya kipa wa Yanga kupangua penalti ya Tshabalala
na kufufua matumaini ya kushinda lakini bila mafanikio.
Awali katika muda wa
kawaida, timu zote zilicheza kwa spidi huku zikishambuliana kwa zamu.
Kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Yanga alikuwa
Tshitshimbi ambaye alicheza mechi yake ya kwanza Yanga tangu asajiliwe akitokea
Mbabane Swallows ya Swaziland.
Ubora na kiwango
alichoonesha kiliwakosha mashabiki wa Yanga na kufanya muda wote wamsifu kwa
nyimbo kutokana na kuokoa mipira mingi ya hatari langoni mwa Yanga.
Timu zote
zilitengeneza nafasi kadhaa za kufunga ndani ya dakika 90 bila mafanikio
kutokana na wafungaji kutokuwa makini.
Waliotengeneza nafasi
nzuri za kufunga ni Mavugo, Niyonzima, Luizio na Okwi kwa upande wa Simba.
Upande wa Yanga ni Ajibu, Tshitshimbi, Martin na Kamusoko.
Yanga ilifanya
mabadiliko kadhaa ya wachezaji hasa kipindi cha pili kwa kuwatoa Raphael Daud,
Juma Abdul na kuwaingiza Juma Mahadhi na Hassan Kessy, lakini haikuwasaidia.
Simba iliwatoa Laudit
Mavugo, Mzamiru Yasini na Erasto Nyoni na kuwaingiza Juma Luizio, Mohamed
Ibrahim na Mohamed Hussein lakini mabadiliko hayo hayakuisaidia kufunga mabao.
Ilibidi Simba isubiri
hadi katika upigaji penalti kuwapa furaha mashabiki kwa ushindi huo.
Mechi ya Ngao ya
Jamii inatumika kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara
inayoanza keshokutwa.
Mechi hiyo
hukutanisha bingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita ambao ni Yanga na mshindi wa
Kombe la FA msimu uliopita ambao ni Simba.
Kikosi cha Yanga:
Youthe Rostand, Kelvin Yondani, Vincent Endrew, Juma Abduli, Gadiel Michael,
Raphael Daud, Papy Tshishimbi Kabamba, Thaban Kamusoko, Emanuel Martin, Ibrahim
Ajibu na Donald Ngoma.
Kikosi cha Simba:
Aishi Manula, Erasto Nyoni, Ally Shomari, Method Mwanjale, Salim Mbonde,
Mzamiru Yasini, Haruna Niyonzima, James Kotei, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na
Laudit Mavugo.
No comments:
Post a Comment