Wakati
zimebaki siku nne (4) kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili kwa msimu wa
2017/18, tunazikumbusha klabu 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL);
timu 24 za Ligi Daraja la Kwanza na 24 Ligi Daraja la Pili kukamilisha usajili
kwa Mfumo wa Mtandao wa TMS – Transfer Matching System.
Ikumbukwe kuwa
dirisha la usajili linafungwa Agosti 6, mwaka huu na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), linatoa angalizo kwamba hakuna klabu itakayoshiriki Ligi
Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kama haitapata leseni
ya klabu.
Baadhi ya
klabu hazijachukua hata fomu za leseni ya klabu wakati zile zilizochukua kuna
baadhi hazijarejesha na pamoja kwamba kuna zile ambazo zimerejesha, lakini baadhi
inaonekana hazikujazwa kwa usahihi.
Kikao cha Kamati
ya Leseni za Klabu, chini ya Msomi Wakili Lloyd Nchunga kinatarajiwa kuketi
Jumamosi Agosti 5, mwaka huu kwenye ofisi za TFF, Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume, Dar es Salaam ambako kitapitia fomu zilizorejeshwa kabla ya kufanya
uamuzi wa kutoa leseni kwa klabu zilizotimiza masharti.
Klabu ambayo
haitapata leseni kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), haitakuwa na
nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja
la Pili kwa msimu wa 2017/18.
Suala la leseni
linakwenda pia kwa wachezaji. Kama ilivyokwisha kutangazwa, hakuna mchezaji
atakayeshiriki Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la
Pili - michuano inayoendeshwa na kusimamiwa na TFF kama hakutimiza masharti ya
kupata leseni ya kumruhusu kucheza.
Kuna vigezo sita
(6) vya mchezaji kupata leseni ambavyo ni: -
1. Kujazwa fomu
ua utimamu wa afya (Medical Form).
2. Bima ya matibabu
kwa mchezaji.
3. Barua ya uhamisho
(Release Letter).
4. Hati ya
Uhamisho wa Kimataifa kwa wachezaji wa kigeni.
5. Mikataba ya
wachezaji iliyosajiliwa kwenye mfumo wa usajili TMS
6. Ada ya
wachezaji wa kigeni ambayo ni Sh 2,000,000 badala ya dola 2,000 za Marekani.
Wakati hayo
yakiagizwa, maandalizi ya ujio mpya wa msimu wa mashindano yanaendelea ambako
kwa kesho Alhamisi, Agosti 3, mwaka huu Kampuni ya Vodacom - inayoongoza kwa
kutoa huduma za mawasiliano nchini Tanzania itatoa vifaa vya mchezo kwa timu
zote 16 za Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuwa ndiyo Mdhamini Mkuu wa michuano hiyo yenye
ushindani mkali. Vodacom wanafanya hivyo kwa mujibu wa mkataba wa udhamini.
No comments:
Post a Comment