Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, July 7, 2017

MAELFU WAJITOKEZA KUMZIKA MWANAMUZIKI SHABAN DEDE WA MSONDO NGOMA

MWANAMUZIKI gwiji wa uimbaji na utunzi wa nyimbo za dansi nchini, Shaban Dede amezikwa leo katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
Hatutamwona tena Dede wala hatutaisikia tena sauti yake tamu na murua, ikighani mashairi ya nyimbo mbalimbali za muziki wa dansi.
Dede alifariki dunia jana, saa mbili asubuhi, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, ambako alikuwa amelazwa kwa wiki mbili akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.
Kabla ya mauti wake Dede alishazushiwa kifo wiki iliyopita, kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii lakini uongozi wa msondo ulikanusha habari hizo
Kifo cha Dede kikuwa ni mwendelezo wa vifo vya wanamuziki kwani hivi karibuni alikuwa
Dede alianza kuimba akiwa bendi ya Msongo Ngoma, enzi hizo ikiitwa Juwata Jazz, DDC Mlimani Park, Bima Lee na baadaye kurejea Msondo Ngoma miaka minne iliyopita na alikuwa mmoja wa watunzi mahiri wa nyimbo, hasa alipokuwa bendi ya Mlimani Park, ambapo inasemekana alitunga nyimbo zaidi ya 100, akiwa anashika nafasi ya pili nyuma ya Hassan Rehani Bitchuka.

Pia, alikuwa chachu ya ushindani wa kimuziki uliokuwepo kati ya Msondo Ngoma na Mlimani Park, ambapo alikuwa karata muhimu ya ushindi katika kila bendi. Alikuwa anajua nini cha kufanya ili kuwafurahisha mashabiki na kuwapa ile burudani wanayoihitaji.
Kifo cha Dede sio pigo tu kwa familia yake, bali pia wanamuziki wenzake na  wengi wamemuelezea bado alikuwa akihitajika kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kutunga na kuimba nyimbo zenye mvuto.
“Ninamfahamu Dede kwa kipindi kirefu kwani alikuwa mtunzi mzuri na mtu mwenye mchango mkubwa katika tasnia ya muziki. Nimesikitishwa sana na kifo chake na pengo lake halitazibika kwa urahisi,” alisema Bichuka, alipozungumza
Kiongozi wa sasa wa Mlimani Park, Abdalah Hemba, amekiri kuwa Dede ndiye aliyeibua kipaji chake, ambacho kwa sasa kimemfanya awe mwimbaji mahiri na kiongozi wa bendi hiyo kongwe nchini.
Hemba alisema Dede ndiye aliyemsaidia kuingia katika bendi hiyo na kujulikana kupitia sanaa ya muziki na alikuwa mtambuzi mzuri wa vipaji vya wanamuziki baada ya kuwa nao kwa muda mfupi.
Miongoni mwa nyimbo za Dede, ambazo zinapendwa na wadau wa muziki wa dansi ni Fumanizi, Kelele za paka hazimzuii mwenye nyumba kulala, Mshenga, Baba mkwe, Amina, Talaka rejea na Kizabinazabina.
Nyimbo hizo na nyinginezo kadhaa, alizitunga wakati akiwa katika bendi ya DDC Mlimani Park kwa muda wa miaka 27, kabla hajarudi katika bendi yake ya zamani ya Msondo Ngoma, mwaka 2014.
Mbali na wimbo wake wa ‘Suluhu’, ambao ulikuwa wa kwanza kuutunga baada ya kurejea Msondo Ngoma, mwanamuziki huyo pia aliitungia bendi hiyo nyimbo kedekede, ikiwemo Fatuma, Umbea umenichosha, Julekha, Jane, Kuruthumu na Amba ambazo zilimjengea umaarufu na kujikuta akipachikwa jina la ‘Kamchape’
Dede alilazimika kurejea Msondo Ngoma kutokana na bendi hiyo kuyumba baada ya kuondokewa na waimbaji wake waliokuwa tegemeo mfululizo, akianza Suleiman Mbwembwe, Othmani Momba, Ally Muhoja Kishiwa ‘TX Moshi’ na Joseph Maina.
Vifo vya waimbaji hao vilisababisha bendi hiyo kongwe kubakiwa na mwimbaji mmoja pekee  marehemu Maalimu Gurumo, hivyo uongozi uliona kuna kila sababu ya kumrejesha Dede ili kuongeza nguvu akisaidiana na Eddo Sanga, Juma Katundu na Hassan Moshi.
Uwezo wake wa kutunga na kuimba haukuishia kwa bendi hizo mahasimu kwani alipotua Bima Lee, mwaka 1983, aliwika kwa nyimbo kama Kipepeo, Bilionea wa mapenzi, Shangwe ya harusi, Zenaba, Kununanuna na Dunia duara.
Dede pia aliwahi kung'ara katika bendi ya Orchestra Safari Sound, ambako alivuma kwa nyimbo kama Nyumba ya mgumba haina matanga, Habari imeota mbawa, Titi na Mariam, kabla ya kurejea DDC Mlimani Park.