Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, July 11, 2017

GOR MAHIA YAWASILI, EVERTON KESHO MAO






MWAMUZI wa Tanzania Israel Nkongo anatarajiwa kuchezesha mchezo wa kihistoria wa kirafiki kati ya Everton ya England dhidi ya Gor Mahia kutoka Kenya utakaofanyika keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Nkongo ambaye ana beji ya FIFA, atasaidiwa na Ferdinand Chacha, Frank Komba na mezani atakuwa ni Hery Sasii na Kamishna wa mchezo ni Michael Wambura.
Akizungumza na wandishi wa habari jana Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa ambao ndio waratibu wa mchezo huo Abass Tarimba alisema maandalizi ya mechi yamekamilika na kinachosubiriwa ni timu hizo kuwasili.
“Maandalizi yamekamilika hivyo niwaombe mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwaona wachezaji wanasifika kwenye Ligi Kuu ya England kwani Rooney atakuja na amekuwa na hamu ya kufika baada ya kusikia magwiji kandaa wametembelea Tanzania,” alisema Tarimba.
Naye Meneja Miradi wa Selcom ambao ndio wanauza tiketi za mchezo huo Gallus Runyeta alisema zoezi la uuzaji tiketi linaendelea na mtu asiye na kadi anaweza kuwahi mapema siku ya mchezo kwani zitakuwepo uwanjani.
“Mtu mmoja anaweza kununua tiketi yake na kumnunulia mtu mwingine ambaye ana kadi hivyo nawaomba mashabiki wajinunulie tiketi mapema,” alisema Runyeta.
Naye Ofisa Usalama wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), Inspekta Hashim Abdallah amewataka mashabiki watakaojitokeza kwenye mchezo huo kuachana na mahaba kwa wachezaji ikiwemo kwenda kuwakumbatia kwani hawataruhusiwa kufanya.
“Mshambuliaji Wayne Rooney atakuwepo kwenye msafara huo, kuna watu watataka kwenda kumkubatia hawataruhusiwa kwani itasababisha usumbufu,” alisema Hashim.
Viingilio katika mchezo huo ni shilingi 8000 kwa VIP B na C na mzunguko ni sh 3000 wakati VIP A itakuwa maalum kwa watu mashuhuri.
Gor Mahia ambayo kwa sasa inanolewa na Dylan Kerraliyewahi kufundisha Simba waliwasili jana mchana na Everton wanatarajiwa kuwasili leo asubuhi na baada ya kuwasili watafanya shughuli mbalimbali za kijamii.
Baada ya kuwasili Everton itafanya kliniki ya soka na kuzuru sehemu mbalimbali kuanzia saa 5:30 hadi saa 11:00 kwani wataanza kutoa huduma shule ya msingi ya Uhuru Kariakoo, klabu ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Sea Cliff na Gymkana
Kwa upande wa Gor Mahia saa 9:00 alasiri mpaka saa 10:00 jioni watakuwa Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mkutano na wandishi wa habari baadae watakuwa Uwanja wa Uhuru wakifanya mazoezi hadi saa 12:00 jioni.
Everton watafanya mkutano na waandishi wa habari saa 10:30 jioni mpaka 11:00 jioni Uwanja wa Taifa na saa 11:00 jioni mpaka saa 1:30 usiku watafanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa.
Keshokutwa kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana wawakilishi wa timu zote watatembelea hospitali ya Pugu Kajiungeni na watazuru Maasai Cultural Center kujionea tamaduni mbalimbali za kabila hilo.
Mchezo utaanza kuchezwa saa 11:00 jioni na milango ya uwanjani itaanza kufunguliwa kuanzia saa nne asubuhi ili kutoa fursa ya watu kuingia kwa muda muafaka bila bughudha.

No comments:

Post a Comment