Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, June 20, 2017

WAGOMBEA 74 WACHUKUA FOMU UCHAGUZI WA TFF



 
WAGOMBEA 74 wamechukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
Hadi zoezi hilo linafungwa jana saa 10.00 jioni wagombea wote wamerejesha, kwenye nafasi ya urais, jumla ya wagombea 10 walijitokeza kuomba nafasi hiyo wakati kwenye makamu rais wamejitokeza sita.
Akizungumza na gazeti hili Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas alisema 58 wamejitokeza kuwania nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji katika Kanda mbalimbali.
“Zoezi la kuchukua na kurejesha fomu kwa mujibu wa Kanuni ya 10, limefanyika kwa siku tano kuanzia Juni 16, 2017 hadi Juni 20, mwaka huu na jumla  ya wagombea 74 wamechukua na kurudisha fomu,” alisema Lucas.
Siku ya kwanza kuanza kutolewa fomu, Jamal Malinzi alikuwa wa kwanza kuchukua fomu akifuatiwa na Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Athumani Nyamlani, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe.
Waliojitokeza kuwania Makamu wa Rais na kurejesha fomu ni Mulamu Ng’hambi, Michael Wambura, Geofrey Nyange, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa kufuata Kanda 13, Kagera na Geita wapo wanne, Mara na Mwanza wanne, Shinyanga na Simiyu watatu, Arusha na Manyara watatu, Kigoma na Tabora wanne.
Katavi na Rukwa wawili, Mbeya, Songwe na Iringa wanne, Njombe na Ruvuma wanne, Lindi na Mtwara wanne, Dodoma na Singida sita, Pwani na Morogoro wanne, Kilimanjaro na Tanga watatu na Dar es Salaam wapo 15.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, msomi Wakili Revocatus Kuuli alisema mchujo utaanza leo hadi Juni 23, kwa mujibu wa kanuni ya 11.1 ya Uchaguzi wa TFF na itafanywa na kamati ya Uchaguzi kwa wote waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali kama inavyojionesha hapo juu.
”Mchujo utafanyika (kesho) leo na wagombea na kuwaandikia barua za kuwajulisha juu mchujo wa awali na Juni 24-25 tutachapisha na kubandika orodha ya awali ya wagombea,” alisema Kuuli.
Kipindi cha kuweka pingamizi ni Juni 26-28 na pingamizi zinatakiwa kuwekwa na wagombea pekee na Juni 29 hadi Julai Mosi  kupitia pingamizi zote kufanya usaili wa wagombea.
Alisema kamati ya uchaguzi itatangaza matokeo ya awali ya usaili Julai 2-3 na sekretarieti itawasilisha masuala ya kimaadili kwenye kamati ya maadili Julai 4-6.
Wagombea watakuwa na fursa ya kukata rufaa kwa maamuzi ya masuala ya kimaadili kwenye kamati ya rufaa ya maadili ya TFF baada ya kamati ya maadaili kutangaza matokeo ya maamuzi ya kamati hiyo Julai 15-17.
Kipindi cha kusikilizwa na kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF, Julai 29 hadi Agosti 4 na orodha ya mwisho ya wagombea na kutangazwa Agosti 5-8 na kampeni kwa wagombea wote itaanza Agosti 7-11
Uchaguzi Mkuu wa TFF unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mkoani Dodoma.

No comments:

Post a Comment