Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, June 12, 2017

URAIS TFF NI SHILINGI 500,000

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, msomi Wakili Revocatus Kuuli (katikati) akitangaza uchaguzi na mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na nafasi zinazogombewa pamoja na wajumbe wenzake. Kushoto ni Jeremiah Wambura na Kulia ni Omar Hamimu. (Picha na Rahel Pallangyo)


ILI kuchukua fomu ya kugombea urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unatakiwa kuwa na shilingi 500,000 na uchaguzi utafanyika mkoani Dodoma Agosti 12 mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, msomi Wakili Revocatus Kuuli alipoongea na wandishi wa habari kusoma tangazo la uchaguzi na nafasi zinazogombewa.
“Anayegombea nafasi ya rais fomu itakuwa shilingi 500,000,  makamu wa rais sh. 300,000 na wajumbe wa kamati ya utendaji sh 200,000,” alisema Wakili Kuuli.
Pia Wakili Kuuli alisema sifa za mgombea wa nafasi ya urais na makamu wa rais anatakiwa kuwa na kiwango cha elimu isiyopungua shahada moja, mwenye utu na uwezo wa kuiwakilisha TFF ndani na nje ya nchi.
Aidha sifa zingine za jumla anatakiwa kuwa mtanzania, elimu ya kidato cha nne, uzoefu katika uendeshaji wa soka kwa miaka mitano, awe na umri angalau miaka 25.
Asiwe na hatia yoyote ya kosa la jinai au kifungo kisicho na mbadala wa faini, awe amewahi kuwa mchezaji wa soka, kocha, refa  au kushiriki katika uendeshaji wa mpira wa miguu katika ngazi ya mkoa au daraja la kwanza.
Wakili Kuuli alisema nafasi zinazogombewa ni rais, makamu wa rais na wajumbe 13 wanaowakilisha kanda 13 na mchakato wa uchaguzi utabandikwa kwenye mbao za matangazo kuanzia kesho.
“Fomu za kuomba uongozi zitaanza kutolewa Juni 16 na mwisho wa kurudisha ni Juni 20 na zitakuwa zinapatikana kwenye Ofisi za TFF, Ilala na katika tovuti ambayo ni www.tff.or.tz,” alisema Wakili Kuuli.
Wakili Kuuli alisema Juni 21-23 kutafanyika kikao cha mchujo wa awali wa wagombea na kuwaandikia barua za kuwajulisha juu mchujo wa awali kabla ya Juni 24-25 kuchapisha na kubandika orodha ya awali ya wagombea.
Kipindi cha kuweka pingamizi ni Juni 26-28 na pingamizi zinatakiwa kuwekwa na wagombea pekee na Juni 29 hadi Julai Mosi  kupitia pingamizi zote kufanya usaili wa wagombea.
Alisema kamati ya uchaguzi itatangaza matokeo ya awali ya usaili Julai 2-3 na sekretarieti itawasilisha masuala ya kimaadili kwenye kamati ya maadili Julai 4-6.
Wagombea watakuwa na fursa ya kukata rufaa kwa maamuzi ya masuala ya kimaadili kwenye kamati ya rufaa ya maadili ya TFF baada ya kamati ya maadaili kutangaza matokeo ya maamuzi ya kamati hiyo Julai 15-17.
Kipindi cha kusikilizwa na kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF, Julai 29 hadi Agosti 4 na orodha ya mwisho ya wagombea na kutangazwa Agosti 5-8 na kampeni kwa wagombea wote itaanza Agosti 7-11.
Wakili Kuuli alisema watashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuzuia na kudhibiti vitendo vya rushwa kwa wagombea na ikithibitika mgombea ametoa rushwa watamfikisha katika vyombo vya sheria.