Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Thursday, June 1, 2017

MCHEZAJI WA ZAMANI WA EVERTON, OSMAN ATEMBELEA TANZANIA, AKUTANA NA WACHEZAJI CHIPUKIZI
SERIKALI imesema kuna kila sababu kwa Klabu za Tanzania kujifunza mbinu, nidhamu na  mafanikio ya  klabu ya  Everton ya Ligi Kuu England  mara itakapokuja nchini mwezi ujao.
Everton na baadhi ya mashabiki wake inatarajia kufanya ziara nchini ambapo Julai 13, mwaka huu itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya bingwa atakayepatikana katika michuano ya Kombe la Sportpesa.
Akizungumzia ziara hiyo jana kwenye utambulisho  wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Everton Robert Elston, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe alisema ujio wa timu hiyo kongwe yenye umri wa miaka 140, ni fursa kwa klabu mbalimbali kuona na  kujifunza namna ya kuendelea.
“Nimepokea kwa furaha kubwa ujio  wa Everton nikiamini utatusaidia kujifunza badala ya kupigana ngumi kila siku. Klabu, wachezaji na hata viongozi kwa pamoja wajifunze wafanye nini kuendeleza soka la Tanzania, ufahari uwekwe pembeni,”alisema.
 Dk. Mwakyembe alisema tayari mgeni wao Elston ametazama uwanja wa Taifa utakaotumika kwa mchezo wa Everton dhidi ya bingwa wa Sportpesa na kusema hakina tatizo kubwa zaidi kinahitaji kubadilishwa nyasi kwa kuwa zilizopo zimekaa kwa muda mrefu.
Mbali na kutarajiwa kucheza Soka Waziri huyo alihimiza klabu hiyo ya kimataifa kutembelea vivutio vya Tanzania ikiwemo Mlima Kilimanjaro na mbuga za wanyama.
Kwa upande wake, Elston aliyeongozana na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo Leon Osman alisema timu ya kwanza ya England kuja kucheza Tanzania itakuwa ni sehemu muhimu ya maandalizi ya msimu mpya ujao.
“Tunafuraha kuja Tanzania, tunafungua milango mipya, hatuna shaka kwamba tutapa marafiki na kuongeza mashabiki wetu kimataifa,”alisema.
Alisema Kocha wao Ronald Koeman na wachezaji wanajiandaa kuja kucheza mechi nzuri dhidi ya moja ya klabu bora Afrika Mashariki.
Mkurugenzi wa Utawala wa Sportpesa Abbas Tarimba alisema ziara hiyo iliyoko chini ya Kampuni hiyo ya bahati nasibu itafanyika sambamba na kutoa elimu kwa makocha na viongozi wa soka nchini.
Michuano ya sportpesa inatarajiwa kuanza wiki ijayo ikishirikisha timu nane za Tanzania na Kenya ambapo bingwa mmoja atacheza na Everton.
Timu zitakazocheza ni Yanga, Simba, Singida United na Jang’ombe zote za Tanzania,  Tusker, Gor Mahia, Nakuru All Stars na AFC Leopards za Kenya.