Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, June 20, 2017

BMT YABARIKI UCHAGUZI WA TFF KUFANYIKABARAZA la Michezo Tanzania (BMT), limebariki kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambao unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mkoani Dodoma.
Akizungumza na wandishi wa habari leo Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas alisema BMT wameitakia uchaguzi mwema wenye amani, upendo na utulivu lakini TFF wameagizwa kupitia sheria za Baraza la Michezo, Kanuni za Baraza na kanuni za Usajili, hususani kanuni ya 8 (1) na (2). 
“BMT wameitakia TFF uchaguzi mwema wenye amani, upendo na utulivu lakini pia wameagiza TFF kuwaeleza wagombea wote utii wa sheria na kuepuka kushika nyadhifa mbili kwa wakati mmoja,” alisema Lucas.
Pia BMT imesema Kanuni  ya 8 (1) na (2), inaagiza kuwa endapo wagombea wote watakaoshinda nafasi wanazowania kwa sasa ndani ya TFF, hawana budi kuachia nafasi mojawapo katika uongozi wa mpira kwa miguu katika ngazi ya wilaya au mkoa aliyoshinda awali.
Katika barua yake iliyoandikwa Juni 19, mwaka huu na kusainiwa na Katibu Mkuu wa BMT, Mohammed Kiganja, Baraza hilo limesema: “Uchaguzi huu usivuruge amani iliyopo nchini na wagombea wakumbuke kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.”
Aidha Baraza limesisitiza kuwepo na haki katika mchakato mzima kuelekea kwenye uchaguzi na mchakato wake uwe huru na amani na usiwe ni kichocheo cha uvunjifu wa amani.
“Baada ya viongozi kupatikana, watakula kiapo cha utii, na kujaza fomu Namba 5 ya BMT ya utekelezaji majukumu yao kama Kanuni ya 8 (4) inavyoeleza,” alisema Kiganja.
Kadhalika, mara baada ya uchaguzi, Baraza limeagiza kuhusisha baadhi ya vifungu vya sheria ya Baraza ili viendane na katiba za TFF na wadau pamoja na kanuni zao.