Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Thursday, June 1, 2017

BARCELONA WALIVYOUJENGA NA KUUMZALIZA MSIMU WAO



 Image result for barcelona team
BARCELONA hawakuweza kukimbizana ipasavyo na Real Madrid msimu uliomalizika wa Ligi Kuu ya Hispania – La Liga, wakazimaliza mbio wakiwa katika nafasi ya pili nyuma ya mahasimu wao hao.
Wana Katalunya wakashindwa kulitetea taji lao kwa tofauti ya alama tatu tu, na laiti wangezifikisha na kufungana na Los Blancos hao, wangekuwa mabingwa kwa sababu ya idadi kubwa ya mabao ya kufungwa na machache ya kufungwa waliyo nayo.
Haikuwezekana, kilichopatikana ni nafasi ya pili, na wameichukua, lakini katika msimu mzima si kwamba wametoka kapa; kocha Luis Enrique anaondoka akiwa amewapa Super Copa ya Hispania na Copa del Rey – Kombe la Mfalme na sasa anakwenda kupumzika na kujitafakari.
Si siri, umekuwa msimu wenye mambo mengi, mvuto na msisimko kwenye matukio yaliyohusisha vijana hao wa Camp Nou na yapo mengi yatakayoangaliwa katika historia kwa msimu huu wa 2016/17 wanaoupa mgongo.
Kuna wachezaji waliokuwa wapya, waliojiongeza kwenye msimu huu ikilinganishwa na walivyokuwa kabla, lakini kuna waliochanua hasa na wale waliotokea kuwa magarasa tu na watatakiwa ama wakubali kukaa benchi au watafute timu nyingine.
Golikipa wa Barcelona, Marc-Andre ter Stegen alitoka kwenye nafasi ya kuwa kipa msaidizi hadi kushika namba moja hapo; kwa ujumla alifanya mambo mazuri msimu huu, japokuwa kwenye mechi nyingine, tena zilizodhaniwa zingekuwa na ushindani mdogo kwa Barca, hakuwa kwenye kiwango cha juu na Barca wakapoteza pointi kadhaa zisizokuwa za lazima.

Kadiri muda unavyokwenda anarekebisha makosa yake na hapana shaka atakuwa mzuri zaidi msimu ujao, ambapo mtindo wake wa kucheza pia unalandana vyema na wa timu.
Mchezaji aliyeonesha kipaji binafsi na kujituma zaidi hata kama timu ilikuwa imegawanyika au kushindwa kushikiwa pamoja ni Lionel Messi. Uwezo wake, kujituma na kutokata tama vinamfanya kuwa aliyejipeleka uzuri zaidi mchezoni.
Messi amefunga mabao mengi na mazuri, lakini tunapokuja kwenye bao tamu zaidi la msimu kutoka kwa watu hawa, naona ni lile la Rafinha, akitundika mpira kwenye kona ya juu ya goli dhidi ya Leganes, na hii ilikuwa mapema mwanzo wa msimu.
Ukitaka kuona jinsi Barca walivyojitahidi msimu huu, angalia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), walivyoweza kupindua kuwa nyuma kwa idadi kubwa ya mabao dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) wakaja kufuzu kwa nusu fainali walikoadhibika.
Alikuwa Sergi Roberto aliyefunga bao la mwisho na lililogeuza matokeo na kuwa 6-1 hapo Camp Nou hata kama baadhi ya watu walilalamika kwamba Barca walipendelewa. Unaweza kupendelewa lakini ukashindwa kutumia hata fursa hizo. Roberto ni mchezaji mzuri na wa kuangaliwa siku zijazo.
Ukweli ukisemwa, ni kwamba kuna wachezaji kadhaa wa Barca wasioonesha kuwa na ufanisi kiufundi, lakini inawezekana kwamba nyota wa klabu hiyo wanamulikwa mno zaidi, hata wakasifiwa kwa mabao wanayofunga kumbe yanatokana na jitihada za hawa wengine.
Watatu ndio wamekuwa wakitajwa zaidi, katika Messi, Neymar na Luis Suarez lakini kuna viungo, mabeki na kipa ambao wanaifanya kazi, ndiyo maana hawajafungwa mabao mengi na wanawazidi Real kwa njia chanya katika uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Rafinha ni mmoja wa wachezaji wasioonwa vya kutosha na hao waeneza habari; amekuwa na msimu mzuri wa kwanza kiungo huyu wa Brazil; anafanya kazi kwa kiwango kikubwa ikiwa ni pamoja na kuipata mipira, kutoa pasi kwa usahihi lakini pia kufunga mabao muhimu.
Msimu ule wa kiangazi Barca walitumia kiasi kikubwa cha fedha kujiimarisha kwenye usajili na kulikuwapo wachezaji kadhaa waliokuwa na msimu wa kwanza, kama beki wa kati, Samuel Umtiti, kinda huyu akionesha uwezo wake kiufundi lakini pia kifiziki. Bado tutarajie mengi na makubwa kutoka kwa Umtiti anayeonekana kujihisi Barcelona ni nyumbani, akifurahia.

Kwa upande mwingine wa kipimio kuna mtu anaitwa Andre Gomes ambaye kama ni msimu mbaya kwake ni huu, tena baada ya kusajiliwa kwa pesa ndefu kutoka Valencia. Amekuwa akipewa nafasi lakini anachokifanya ni kupoozesha mpira mara kwa mara na kudhaifisha timu, ikizingatiwa kwamba Enrique amekuwa akitaka mpira uwafikie pacha wale watatu niliowataja kule mbele mapema iwezekabavyo.
Haikuwa, hadi wiki za mwisho alipoanza kuipandisha mipira hiyo, lakini tayari Barca walishajeruhiwa na majaliwa ya ubingwa hayakuwa tena mikononi mwao. Kiulinzi pia Gomes ni dhaifu, akionekana kuwa sayari tofauti kabisa na Sergio Busquets.
Kuna wachezaji kadhaa wa Barca ambao wapo kwa mkopo kwenye klabu nyingine, na Munir ni mmoja wao – akiwa amefanya kazi kubwa sana akiwa na Valencia – akifunga mabao manane akiwa ni winga. Aliwasaidia kwa sababu jamaa hao wanaojulikana kama Los Che walikuwa katika hali mbaya kwa muda mwingi wa mwaka, kama si miaka michache iliyopita.
Kwingineko kuna mtu anayeitwaCristian Tello aliyekuwa na kawaida ya kuchezeshwa na kufanya vyema akiwa na Fiorentina wakati Douglas alicheza muda mwingi wa msimu akiwa na Sporting Gijon walioshushwa. Si yeye aliyesababisha washuke, bali alikuwa mmoja wa waliojitahidi kuwanusuru. Ni kusubiri kuona iwapo wachezaji hawa watarejeshwa nyumbani, watabaki huko kwa mkopo au watauzwa kimoja.
Vipi kuhusu wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukingoni katika kipindi cha miezi 14 hivi ijayo? Wapo na Messi ni mmoja wao. Ni wazi kwamba kwa kazi anayofanya, Messi anastahili kupewa dili jipya la mkataba na matarajio ni kwamba atausaini.
Mwingine ni kijana mwenye umri wa miaka 19, Carles Alena, aliyeingia kikosi cha kwanza msimu huu, akianzia kwenye benchi mechi zaidi ya 10 za La Liga na kuingia mara kadhaa, kisha akafunga bao kwa mara ya kwanza akiwa na wakubwa wakati wa mechi ya Copa del Rey.
Kiungo huyu anacheza soka ya moja kwa moja, miguu yake ni myepesi na anaifanya kazi haraka na mzuri katika kumaizi pasi – vitu ambavyo Barca wanajitaji na muhimu kutunza hazina kama hiyo. Aprili ilidaiwa kwamba angesainishwa mkataba mpya, lakini bado hakuna taarifa rasmi juu yake.
Kwa ujumla ni sahihi kusema kwamba kikosi cha kwanza cha Barca msimu huu kimekuwa ni timu inayopata matokeo mazuri lakini wakati mwingine pia kikiishia kutibuliwa – na ni moja ya maeneo madogo madogo waliyokwama msimu huu na ukweli ni kwamba hawana wachezaji wengi wa kuziba mapengo, tofauti na Real Madrid.
Hata hivyo, kwenye eneo hilo la viraka kuna mtu anaitwa Lucho ambaye amefanikisha sana kazi, lakini pia mshambuliaji  yupo Paco Alcacer, aliyewafungia wana Katalunya mabao mawili na usaidizi kwa mengine mawili katika dakika zake 376 alizocheza, zote akitokea benchi.
Yupo Denis Suarez ambaye ni kiungo aliyefunga bao moja na usaidizi kwa mawili, ambapo akiwa ni kiungo wa kati si kazi mbaya. Nimalizie kwa kusema kwamba kwenye ulinzi wa kati Gerard Pique yupo vizuri sana lakini pia Marlon na huwezi kuacha kumtaja mtu kama Javier Mascherano.

No comments:

Post a Comment