Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, April 24, 2017

SIMBA YAPOKWA POINTI TATU



KAMATI ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeipokonya Simba ushindi wa mezani waliopewa baada ya kufungwa na Kagera Sugar 2-1 Aprili 2, mwaka huu Uwanja wa Kaitaba, Kagera.
Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 iliipa Simba SC ushindi wa mabao matatu na pointi tatu baada ya kujiridhisha, beki Mohammed Fakhi aliichezea timu ya Kagera Sugar akiwa ana kadi tatu za njano.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jioni hii ofisi kwake, Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam, Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa amesema kwamba Kamati imegundua makosa kadhaa katika maamuzi ya Simba kupewa ushindi wa mezani.
Alisema kwanza malalamiko ya Simba hayakuwasilishwa ndani ya wakati kwa mujibu wa kanuni ya 20 kifungu cha kwanza cha kanuni za Ligi Kuu toleo la mwaka 2006 inayotaka malalamiko yote yawasilishwe kwa maandishi Bodi ya Ligi siyo zaidi ya saa 72 baada ya mchezo kumalizika kwa mchezo.
Akasema pili malalamiko hayo hayakulipiwa ada kwa mujibu wa kanuni ya 20 kifungu cha nne kinachosema ada ya malalamiko ni Sh. 300,000 na kwamba malalamiko yatakayowasilishwa bila kulipiwa ada au baada ya muda uliowekwa hayatasikilizwa.
Sababu ya tatu aliyoitaja Mwesigwa ni kwamba kikao cha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kilikosa uhalali baada ya kuwashirikisha Wajumbe waalikwa ambao siyo sehemu ya Kamati hiyo.
“Kwa maana hiyo matokeo ya mchezo kati ya Kagera Sugar na Simba Sports Club yanabaki kama yalivyokuwa awali, vile vile Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji inamuagiza Katibu Mkuu wa TFF kuwapeleka katika kamati za kinidhamu na Maadili baadhi ya watendaji wa bodi ya ligi kwa kutokuwajibika katika nafasi zao na kuipotosha Kamati ya Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72,”amesema Mwesigwa.
Kuhusu Fakhi, Mwesigwa kama alikuwa ana kadi za njano ataitumikia katika mchezo ujao wa timu yake.
Ikumbukwe Kamati ya Saa 72 iliipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu baada ya kujiridhisha beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi aliichezea timu hiyo dhidi Wekundu wa Msimbazi Aprili 2, mwaka huu akiwa ana kadi tatu za njano, ambayo ni kinyume cha kanuni.
Lakini siku mbili baadaye, Kagera Sugar wakapinga maamuzi hayo na kuomba suala hilo lisikilizwe upya kwa kuwa mchezaji wao hakuwa na kadi tatu za njano siku wanaifunga Simba 2-0 Uwanja wa Kaitaba.
Ndipo TFF ikaliwasilisha Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ambayo leo imemaliza sakata hilo kwa kuirudishia Kagera Sugar pointi zake.
Pamoja na hayo, Simba inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 59 baada ya kucheza mechi 27, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 za mechi 25.

No comments:

Post a Comment