Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, January 14, 2017

Tusijivune kulegeza bukta Afcon 2017
FAINALI za 31 za mashindano ya Mataifa ya Afrika, yaani Afcon zinaanza leo nchini Gabon na kushirikisha nchi 16 ikiwemo mwenyeji Gabon iliyofuzu kutokana na uenyeji wake.
Ukiondoa mwenyeji Gabon, timu zingine zote 15 ikiwemo Ivory Coast ambaye ni bingwa mtetezi, zilianzia katika hatua ya kufuzu ili kusaka nafasi ya kushiriki katika fainali hizo.
Ni fainali za 31 na Tanzania ilishiriki mara moja tu mwaka 1980 nchini Nigeria, ambapo mashindano hayo yalishirikisha timu nane, ambazo ziligawanywa katika makundi mawili ya timu nne kila moja.
Kwa sasa kuna jumla ya timu 16, ambazo zinagawanywa katika makundi manne yenye timu nne kila moja.
Fainali hizo zinafanyika huku Tanzania ikiendelea kutokuwepo katika fainali hizo kwa mara nyingine tena baada ya kushindwa kufuzu baada ya timu ya Taifa Stars kuchemka.
Kuanzia leo tutashuhudia mipambano ya aina yake kutoka kwa nyota wa soka wanaocheza soka Ulaya, China, Marekani na Afrika ambao wamejaa vipaji.
Wachezaji wa timu za Tanzania ziwe za klabu au za taifa wana kitu cha kujifunza kutoka katika mashindano hayo makubwa kabisa ya taifa barani Afrika.
Mashindano hayo yana wachezaji nyota kama vile akina Riyad Mahrez, Islam Sliman na Daniel Amertey, ambao wanacheza soka katika klabu ya England ya Leicester City ya England.
Hao ni wachache kwani kuna wachezaji wengi zaidi nyota ambao watashiriki katika mashindano hayo ya Mataifa ya Afrika.
Kikubwa wachezaji wa Tanzania wanatakiwa kujifunza kitu kutoka kwa wachezaji na timu za taifa zinazoshiriki mashindano hayo ya Afcon.
Lakini cha ajabu utashangaa kuona wachezaji wa Tanzania badala ya kujifunza mbinu za uchezaji kutoka kwa wenzao wa Afcon, badala yake wataiga unyowaji wa nywele na ulegezaji bukta utakaofanywa na baadhi ya wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo.
Katika Afcon kutakuwa na mbinu kibao za uchezaji soka, ambazo ndizo zinatakiwa kuigwa na wachezaji wetu ili watuoneshe ufundi katika Ligi Kuu Tanzania Bara na wale waliopo katika Taifa Stars.
Watanzania hawataki kuoneshwa mitindo ya ulegezaji bukta au kunyoa viduku, kuweka tatuu na badala yake wanataka kuona mitindo ya soka la kisasa.
Wachezaji wa Tanzania tuache kuiaga ujinga na badala yake muige vitu vya msingi, ambavyo vitawasaidia kuboresha au kunoa viwango vyenu vya mchezo na sio kulegeza bukta.
Wachezaji wetu ni mahiri sana kuiga vitu vya kijinga, ambavyo wanavipatia kweli, lakini linapokuja suala la kiwango cha mchezo wanashindwa kuiga wenzao wanavyofanya vizuri.
Baada ya kukosa mwakilishi katika Afcon, lakini sasa Watanzania watafarijika kwa msanii wao Diamond kutumbuiza katika ufunguzi wa Afcon 2017.