Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, January 8, 2017

MWAMBUSI ASEMA DHARAU ZILIWAPONZA



KOCHA Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema kipigo cha mabao 4-0 walichopata toka kwa Azam FC ni darasa kwa wachezaji kujua hawatakiwi kudharau mechi hata kama wamefuzu.
Akizungumza na gazeti hili Mwambusi alisema wachezaji walicheza wakijua wameshavuka kwenye hatua ya makundi na kustarehe na kuacha kuonyesha juhudi uwanjani na kuacha njia wazi.
“Wachezaji wetu walicheza huku kichwani wakijua tumeshavuka kwahiyo hakukuwa na haja ya kuweka nguvu zaidi lakini ni somo kwetu tunatakiwa tucheze mechi zetu kwa uangalifu kwa sababu tumepoteza hii mechi tunakubali matokeo,” amesema Mwambusi
Pia Mwambusi alisema wachezaji walistarehe na kuacha njia wazi Azam wakacheza kwa nguvu na kupata mabao manne na kudai ni masikitiko lakini watarekebisha makosa.
Naye kocha wa Azam FC, Idd Cheche alisema walitumia mbinu ya kukaba viungo wa Yanga ndio maana walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 4-0.
Akizungumza na gazeti hili, Idd Cheche alisema Yanga wanategemea mipira ya pembeni kushambulia hivyo mimi nikakaba wachezaji viungo wa Yanga wakashindwa kupata mpira.
 “Yanga wanategemea sana kushambulia kupitia mipira ya pembeni hivyo sisi tukaangalia wale wachezaji wachezaji ambao wanawachezesha tukakamata sehemu ya kiungo tukauwa lengo lao,” alisema Cheche
Bao la kwanza kwenye mchezo huo lilifungwa na nahodha John Bocco 'Adebayor' dakika ya pili kwa shuti la mguu wa kushoto kufuatia mpira uliopanguliwa na kipa Deo Munisha ambao ulipigwa na winga Joseph Mahundi bao lililodumu hadi mapumziko.
Azam FC walilishambulia lango la Yanga kila mara na dakika ya 54 Yahaya Mohammed aliipatia Azam bao la pili kwa kichwa baada ya kupokea krosi kutoka kwa Abubakar Salum 'Sure boy.
Mahundi alifunga bao la tatu dakika ya 80 kwa shuti kali akiwa nje ya eneo la 18 baada ya kupokea pasi nzuri toka kwa Gadiel Michael Dida kuchupa bila mafanikio.
Akitokea benchi Enock Atta Agyei alihitimisha karamu ya mabao baada ya kufunga bao nne dakika ya 84 akitumia vyema makosa ya Geofrey Mwashiuya aliyeshindwa kuokoa krosi iliyopigwa na Mahundi.
Kwa matokeo hayo Azam imeongoza kundi B ikiwa na pointi saba huku Yanga wakishika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia pointi sita.
Kwa matokeo hayo Azam FC imeifunga Yanga mabao 38 na Yanga imeifunga Azam FC mabao 37 tangu zianze kukutana Octoba 15, 2008 katika mechi za mashindano mbalimbali walikutana.
Ushindi wa mabao 4-0 wa Azam FC ni wa 10 sawa na Yanga ambao wameifunga 10 na kutoka sare mara nane na kuwa na rekodi ya kuwa ndio timu pekee Tanzania inayoizidi Yanga kwa matokeo.
Kabla ya mchezo Yanga walikuwa wameizidi Azam FC kwa ushindi mmoja na mabao matatu kwenye mashindano yote waliyokutana zikiwa zimelingana kila kitu.
Kwenye Ligi Kuu zimecheza mara 17, Yanga imeshinda mara tano na Aza mara tano zimetoka sare mara saba.

No comments:

Post a Comment