Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, January 14, 2017

JUMA KAMAYA: Mwandishi wa kitabu cha soka
“BORESHA na endeleza kipaji chako cha soka ni kitabu kinachofundisha mchezo wa mpira wa miguu kwa wachezaji wachanga kuanzia miaka 6-20.
Kitabu hiki nimekigawanya kwa kuzingatia umri wa wachezaji hivyo basi kitabu hiki kimefanya vipatikane vitabu vingine vitatu ambavyo vinabeba jina hilo la boresha na endeleza kipaji chako cha soka.
Kitabu cha kwanza ni cha wachezaji kuanzia umri wa miaka 6-14, kitabu cha pili ni cha wachezaji kuanzia umri wa miaka 14-17, kitabu cha tatu ni cha wachezaji kuanzia umri wa miaka 17 -20 huku kitabu chenyewe ambacho ndio kikubwa kitakuwa kwa wachezaji kuanzia umri wa miaka 6-20,” anasema Juma Kimaya ambaye ni mwandishi wa vitabu hivyo.

Juma ni nani?
Juma ni kijana wa kitanzania mwenye umri wa miaka 20, alizaliwa na kupata elimu ya msingi wilaya ya Nzega, Tabora lakini baadae alihamia Dar es Salaam. Alipata elimu ya sekondari kwenye shule ya sekondari ya Kibasila iliyopo Dar es Salaam na alihitimu  kidato cha nne mwaka 2014.
Alipokuwa na umri wa miaka mitano alianza kucheza soka katika timu za mitaani Tabora kabla ya kuhamia Dar es Salaam na kuendelea kucheza huku akiwa anasoma.
Mwaka 2010 akiwa kidato cha kwanza aliichezea Yanga B yenye maskani yake mitaa ya Jangwani na Twiga Dar es Salaam  lakini anakiri hakucheza kwa mafanikio ndio akapata wazo la kuandika kitabu kikiwa mwongozo wake katika kujifunza mchezo wa soka.
Baada ya kupata wazo hilo alimweleza kocha wake wa Yanga B, Anthony Chibasa ambaye alimshauri amuone aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni ambapo alionana naye na kumpatia alichokihitaji.
Baada ya kuhitimu kidato cha nne mwaka 2014 wakati akicheza soka aliumia goti na huo ndio ukawa mwisho wa kuacha kusakata kabumbu na kwenda Mwanza kuuguza goti.
Safari ya  kuandika kitabu inaanza
Anasema wakati akicheza soka aliandika muswada wa kumwongoza katika uandishi wa kitabu chake, lakini pia ulimsaidia kwenye kuboresha kiwango cha uchezaji japo ndoto ya kuwa mchezaji mahiri ilizimika baada ya kuumia goti.
Baada ya kuachana na soka akaanza kuuweka muswada wake usomeke na kueleweka kwa wachezaji wenzake kwani alitambua wachezaji wengi wa Tanzania hutumia vipaji pekee na kukosa elimu ya mchezo wa soka huku akitambua soka huleta uzalendo, hujenga afya na hutoa ajira kwa vijana.
Ili kufanikisha ndoto ya kuandika kitabu chake kwa ufasaha alilazimika kusoma kozi ya awali ya ukocha iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambayo iliendeshwa na Mkufunzi Michael Bundala.
Kimaya anasema kozi hiyo ilimsaidia kuboresha uandishi wa kitabu chake  baada ya kumalizika alimpa  Kayuni maswada ili amwandikie Dibaji.
Katika kuboresha muswada anasema alilazimika kuwatafuta wataalamu wa mchezo wa soka ili wapitie muswada wake kabla ya kuchapisha kitabu baada ya kuongea na  Kayuni.
Miongoni mwa wataalamu aliowaona ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF wa sasa, Salum Madadi na aliyekuwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga  ndio walimshauri kukigawa kitabu kwa kuzingatia umri.
Pia alipata maoni ya kocha  Bundala na Mkufunzi Dk Jonas Tiboroha wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao kila mmoja alimwandikia ujumbe ambao unapatikana kwenye kitabu. Mwisho alikwenda serikalini kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT)ambapo walimpongeza kwa kazi yake na Katibu Mkuu Mohamed Kiganja alimwandikia ujumbe.
“Hawa wote kwa namna moja au nyingine walichangia kitabu hiki kiwe bora kwa mchezaji,” anasema Kamaya.

Yaliyomo kwenye kitabu
Kitabu kimesheheni mawazo mbalimbali ya wadau wa soka hivyo kitaongeza kasi ya kukua kwa soka la Tanzania.
Kwa kifupi kitabu kina sura zifuatazo ambazo zitamsaidia mchezaji kuwa bora kiuchezaji sasa na baadae.
Sura mojawapo ni maana ya mchezo wa mpira wa miguu na mambo yote muhimu ambayo ni lazima mchezaji awe nayo kabla ya kuingia uwanjani.
Sura hii imeeleza vitu muhimu ambavyo vi vema mchezaji akaviweka sawa kabla hajaingia uwanjaini kama akili timamu na nidhamu, afya ya mwili, umbile, lishe bora na usafi wa mavazi na mwili bila kusahau kupumzika.
Pia kuna sura inayoeleza mazoezi ya mwili na mpira, sura hii mchezaji atajifunza mazoezi ya mwili  ambayo yatamfanya kuwa na utimamu wa mwili, hapa mchezaji atajifunza mazoezi ya pumzi, mazoezi ya ukakamavu, mazoezi ya wepesi wa mwili, mazoezi ya kukimbia kwa kasi na mazoezi ya viungo vya mwili.
Mazoezi ya mpira mchezaji atajifunza kutumia miguu yake  kwani ni muhimu ili aweze kukabili tukio la kimchezo na mguu husika kwa wakati muafaka, atajifunza namna ya kufunga mabao kwenye magoli madogo na makubwa na kucheza mazoezi kwenye eneo dogo na uwanja mzima.
Sura nyingine mchezaji atajifunza mazoezi ya mwili na mpira wa miguu kwa pamoja, sehemu za mpira wa miguu, sheria za mpira wa miguu na majukumu yake ndani ya uwanja.
Pia kuna sura inayoitwa utulivu katika mchezo wa soka ambayo hupatikana kwenye nguzo nne ambazo ni utazamaji, kujiamini, umakini na ukimbiaji na sura nyingine ni historia fupi ya mpira wa miguu duniani.
Kwenye kitabu hiki mchezaji atakutana na maelezo yaliyojitosheleza na michoro inayovutia yenye kumpa mifano inayofanyika kwa vitendo na mwisho kuna vifupi vya maneno ambayo itamsaidia mchezaji kutambua maana ya maneno yaliyotumika ndani ya kitabu.

Ushauri wa mwandishi kwa wasomaji
Anasema siyo wachezaji tu wanaweza kukitumia kitabu chake bali pia walimu wa  soka wanaweza kukitumia kwa kuwapatia mafunzo wachezaji wachanga kulingana na umri kwani wana uelewa tofauti katika kupokea mafunzo. Ili mchezaji aweze kufikia kiwango bora ni vizuri akapitia katika malezi yafuatayo kwasababu inachukua muda si chini ya miaka 10 na saa 10,000 kwa mchezaji chipukizi kuwa mkomavu.
Anasema wazazi wana mchango mkubwa wa kuwafanya watoto kuwa wachezaji wazuri kwa kuwajumuisha kushiriki mazoezi ya mpira wakiwa na umri mdogo.
Uwepo wa vyuo vya michezo utasaidia kuibua vipaji vya wachezaji na kuviendeleza kwa kuwapatia mafunzo ya mpira wa miguu na elimu.
Pia taasisi za michezo zenye dhamana zinahusika kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya mpira wa miguu kwa kuanzisha mipango ya maendeleo ya wachezaji wakiwa na umri mdogo.
“Michezo ikisimamiwa na kuendeshwa vizuri katika shule husaidia kuibua vipaji vyenye uelewa mzuri wa mpira wa miguu na elimu kwani kipaji hakijitokezi tu bali hugunduliwa na ni njia ndefu kufikiwa,” anasema.
Mwandishi huyo anamaliza kwa kunukuu maandiko ya Dk Tiboroha: “Wazee wetu wa zamani walikuwa sahihi kusema kwamba busara ya mtu haipimwi kwa umri au elimu”.
Pia ananukuu ya Katibu Mkuu wa BMT: “Tanzania yetu tutaijenga wenyewe”. Nukuu hizi ni zinapatika kwenye kitabu hiki ambacho kimechukua miaka kumi kukamilika.
Wito
Anatoa wito kwa wadau kuungana naye ili elimu iwafikie wachezaji wote waliopo ndani ya nchi na nje. “Naomba wadau wanisaidie kuchapisha kitabu hiki ili kiweze kusambazwa kwani lengo langu ni kuwafikia wachezaji na watu wote wanaopenda soka ila sina fedha”.
Anasema kwa anayehitaji kushirikiana naye anapatikana kwenye namba 0717100042 au barua pepe jumakimaya3@gmail.com

Shukrani
Kimaya anawashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha kuandika kitabu chake kwa namna yoyote. Kipekee anaishukuru BMT, TFF, Kayuni, Katibu Mkuu wa Chama cha Makocha (TAFCA) Bundala, Mkufunzi wa elimu ya viungo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Tiboroha na Kanali mstaafu na mmiliki wa shule ya michezo Lord Barden, Idd Kipingu.
Pia wazazi wake Eva Kachala na Mohamed Rashid kwa malezi bora na elimu waliyompatia na hatimaye kuweza kuandika kitabu ambacho leo kitasaidia kukuza soka la Tanzania.