Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, January 14, 2017

AZAM FC BINGWA WA MAPINDUZI



AZAM FC jana wametawazwa kuwa mabingwa wapya wa kombe la Mapinduzi kwa mara ya tatu baada ya kuifunga timu ya Simba bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Katika mchezo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk Ally Mohammed Shein alikuwa mgeni rasmi na ndiye aliyekabidhi zawadi ya kikombe kwa mabingwa hao waliowavua mabingwa wa mwaka jana URA ya Uganda.

Azam ilianza michuano hiyo kwa kusuasua katika hatua za makundi lakini kadiri mashindano yalivyokuwa yakiendelea ndivyo walizidi kucheza vizuri huku mlinda mlango wake Aishi Manula akiwa hajafungwa hata bao moja.

Himid Mao aliipatia Azam bao la kwanza kwa shuti kali la mguu wa kulia nje kidogo ya 18 dakika ya 13 baada ya wachezaji wa Simba kushindwa kumdhibiti huku wakidhani angetoa pasi kwa wenzie.

Licha ya kufungwa bao hilo Simba waliendelea kutawala mchezo na kufika zaidi langoni mwa wapinzani lakini safu ya ulinzi ya Azam iliyokuwa chini ya Yakub Mohammed na Agrey Moris ilikuwa imara na kuwazidi ujanja vijana hao wa Msimbazi.

Kiungo Mwinyi Kazimoto ambaye hakuwa amecheza mechi yoyote ya michuano hiyo alizidiwa ujanja na viungo wa Azam hali iliyopelekea ashindwe kuisadia timu kiasi cha kocha Joseph Omog kuamua kumtoa dakika ya 41 na kumuingiza Laudit Mavugo.

Kipindi cha pili Simba walianza kwa kasi ya kutaka kurudisha bao hilo lakini wachezaji wa Azam walikuwa makini kuanzia kati ya uwanja hadi safu ya ulinzi huku wakiwaacha nahodha John Bocco na Yahaya Mohammed mbele ambao nao walikuwa wanarudi kusaidia kukaba.

Mwamuzi Mfaume Ally Nassor aliwaonya kwa kadi ya njano Aboubakar Salum 'Sure Boy' na Himid kwa Azam huku Abdi Banda akionywa kwa Simba.

Kwa ushindi huo Azam wamekabidhiwa kombe pamoja na fedha taslimu Sh 10 milioni ikiwa ni zawadi ya bingwa wa michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment