Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, January 24, 2017

ADHABU ZA WAAMUZI, KAMISHNA, MAKOCHA NA WACHEZAJI KWA LIGI DARAJA LA KWANZA NA LA PILI



LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 34 (Pamba vs Friends Rangers). Kamishna wa mechi hiyo Mnenge Suluja amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo cha timu ya Pamba kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 35 (Kiluvya United vs Lipuli). Timu ya Lipuli imepewa Onyo Kali kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Pia mshabiki wa Kiluvya United, Bw. Athuman Mzongela anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi na kutaka kuwapiga wakati wa mapumziko. Hata baada ya mchezo aliendelea kuwatolea lugha chafu waamuzi na Msimamizi wa Kituo.
Mechi namba 36 (African Sports vs Ashanti United). Daktari wa Ashanti United, Andrea Mbuguni amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa kuondolewa kwenye benchi baada ya kumtolea lugha chafu Mwamuzi Msaidizi namba moja.
Mechi namba 38 (Lipuli vs Mshikamano FC). Kocha wa Mshikamano FC, Hamisi Kinonda amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga muda wa nyongeza wa dakika tano, na kumtolea lugha ya matusi Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Wachezaji wa Mshikamano FC, John Mbise jezi namba 9, Abdallah Makuburi (5), Ally Mangosongo (12) na kipa Steven Peter (1) wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumshambulia Mwamuzi Bryson A. Msuya.
Lakini pia Mwamuzi Bryson A. Msuya amefungiwa mwaka mmoja kwa kutozingatia sheria ipasavyo wakati akitoa penalti dhidi ya timu ya Mshikamano FC, na ripoti yake kufanana na ile ya Kamishna.
Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Makongo Katuma amefutwa katika orodha ya waamuzi wanaotambuliwa na TFF kwa kuwapiga vichwa wachezaji wawili wa Mshikamano FC wakati Mwamuzi wa Kati alipokuwa akishambuliwa na wachezaji wa timu hiyo wakati wakipinga adhabu ya penalti dhidi yao.
Adhabu hizo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1) na 38(1c) na (1e) za Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. Mwamuzi Katuma pia alipata alama za chini ambazo zisingemruhusu kuendelea kuchezesha Ligi Daraja la Kwanza.
Naye Mwamuzi wa Akiba, Hashim Mgimba ameondolewa kwenye ratiba kwa kuonyesha muda wa nyongeza (added time) tofauti na ule alioelekezwa na Mwamuzi. Adhabu dhidi ya Mgimba imezingatia Kanuni ya 38(1d) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Kamishna wa mechi hiyo Fidelis Ndenga wa Njombe ameondolewa kwenye ratiba ya makamishna kwa taarifa yake kufanana na ile ya Mwamuzi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Makamishna.
Pia Kamati imetoa mwito kwa vyombo vya usalama (askari polisi) kutumia nguvu za wastani katika kutuliza ghasia viwanjani, hasa pale wanapotaka kushughulikia eneo linalohusu wachezaji.
Uwanja wa Kichangani umeondolewa kutumika kwa mechi za Ligi, hivyo klabu za Iringa sasa timu zao zitatumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini humo kwa mechi zao la Ligi. Uwanja huo ulikuwa kwenye matengenezo ambayo tayari yamekamilika.
Mechi namba 39 (Polisi Dar vs Pamba FC). Klabu ya Pamba imepewa Onyo Kali kwa kutofika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 33 (KMC vs JKT Mlale). Kocha wa JKT Mlale, Edgar Msabila amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi (orderd off) kwa kutoa lugha chafu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 38 (Kimondo FC vs Njombe Mji). Kocha wa Njombe Mji, Abdul Banyai amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumtolea Mwamuzi lugha ya matusi, na kulazimisha wachezaji wake wajiangushe ili kupoteza muda.
Mechi namba 40 (Coastal Union vs Kurugenzi). Wachezaji wawili wa Kurugenzi; Kipa Hamza Mpatula na Optatus Lupekenya wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kosa la kupigana wakiwa uwanjani baada ya mechi kumalizika. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
Mechi namba 36 (Rhino Rangers vs Polisi Mara). Klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 20. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 38 (Mgambo Shooting vs Rhino Rangers FC). Kocha wa Mgambo, Moka Shabani amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi wakati timu zikielekea vyumbani baada ya kumalizika kipindi cha kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.

LIGI DARAJA LA PILI
Mechi namba 17 (Abajalo vs Burkina Faso). Klabu ya Burkina Faso imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 18 (Cosmopolitan vs Changanyikeni). Klabu ya Changanyikeni FC imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya filimbi ya mwisho. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 19 (Kariakoo vs Cosmopolitan). Klabu ya Kariakoo imepewa Onyo Kali kwa timu yake kutokuwa na daktari katika mechi hiyo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3).
Mechi namba 16 (Sabasaba vs Namungo). Klabu ya Sabasaba imepewa Onyo Kali kutokana na washabiki wake kuwazonga waamuzi wakati wakielekea vyumbani baada ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kumalizika. Uamuzi huo umezingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi namba 17 (Mawezi Market vs Mkamba Rangers). Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting), na pia kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 35. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi namba 19 (Namungo vs Mighty Elephant). Mighty Elephant imepigwa faini ya sh. 100,000 kutokana na wachezaji wa akiba na viongozi wake kuingia uwanjani kushangilia bao la timu yao. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(7), na adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(47) ya Ligi Daraja la Pili.

No comments:

Post a Comment