Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, March 19, 2016

SIMBA YAVUNJA MWIKO WA TANGA NA KUENDELEA KUKAA KILELENI LIGI KUU




KASI ya Simba katika mbio za Ligi Kuu Tanzania Bara hivi sasa inatisha na haizuiliki.
Pengine ndivyo inavyoweza kuzungumzia matokeo ya mchezo wa jana wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Coastal Union uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani Tanga na kumalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Matokeo hayo yameifanya Simba iendelee kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 57 ikiwa ni tofauti ya pointi saba na timu zinazoifuatia ambazo ni Yanga na Azam zote zikiwa na pointi 50, zikitofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hata hivyo Simba ipo mbele michezo mitatu ikiwa tayari imecheza michezo 24, wakati Yanga na Azam zenyewe zimecheza michezo 21.
Lakini ushindi wa jana licha ya kuwahakikishia kuendelea kukaa kileleni, lakini pia ni furaha kubwa kwa Simba kuifunga timu ambayo katika uwanja huo ilionekana mwiba kwa Yanga na Azam.
Coastal iliifunga Yanga mabao 2-0 katika uwanja huohuo na kisha kuifunga Azam FC bao 1-0 pia katika uwnaja huohuo. Kabla ya hapo Yanga na Azam zilikuwa hazijapoteza mchezo katika ligi hiyo.
Katika mchezo wa jana, Simba ilipata bao la kwanza dakika ya 39 mfungaji akiwa Danny Lyanga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Mohammed Hussein Tshabalala.
Bao la pili la Simba lilifungwa na Hamisi Kiiza dakika ya 52 kwa kichwa akiunganisha krosi ya beki Emery Nimubona.
Bao hilo lilikuwa la 19 kwa Kiiza msimu huu akiongoza katika orodha ya wafungaji.
 Pia kwa bao hilo, Kiiza ameifikia rekodi iliyowekwa na mshambuliaji  Amis Tambwe wa Yanga msimu wa mwaka 2013/2014 wakati akichezea Simba, ambapo alifunga mabao 19 na kuibuka mfungaji bora.
Coastal Union licha ya kupoteza mchezo huo ilijaribu kucheza kwa uelewano hasa kipindi cha kwanza, lakini ilishindwa kutumia nafasi ilizopata.
Kwa matokeo hayo Coastal Union inaendelea kuburuza mkia ikiwa na pointi 19 baada ya kushuka dimbani mara 24 na hivyo kuwa bado katika hatari ya kushuka daraja.
Simba; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohamed Hussein, Juuko Murshid, Novarty Lufunga, Justice Majabvi, Jonas Mkude, Said Ndemla/Awadh Juma, Mwinyi Kazimoto/Mgosi, Hamisi Kiiza na Daniel Lyanga.

Coastal Union; Fikirini Bakari, Hamad Juma, Adeyum Saleh, Hamisi Mbwana, Yusuph Sabo, Yusuph Chuma, Juma Mahadhi, Abdulhalim Humud, Ismail Mohamed/Abasarim Chidiebele, Ally Ahmed Shiboli/Said Jeillan  na Ibrahim Twaha Messi/Ayoub Yahya.

No comments:

Post a Comment