Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungia kati ya
mechi tatu na nane wachezaji Juma Nyoso wa Mbeya City na Aggrey Morris wa Azam
kutokana na makosa ya kinidhamu waliyoyafanya wakiwa uwanjani.
Nyoso
ambaye alilalamikiwa na TFF kwa kumfanyia vitendo vya udhalilishaji mshambuliaji
Elias Maguri wa Simba amefungiwa mechi nane za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 57 na Ibara ya 11 (f) ya Kanuni
za Nidhamu za TFF Toleo la 2012.
Akiwa
mbele ya Kamati hiyo jana (Februari 5 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Nyoso
alikiri kufanya na kujutia kosa hilo, pia amemuomba radhi mchezaji Maguri kwa
kitendo hicho.
Akisoma
uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa alisema
kitendo kilichofanywa na Nyoso ni kosa kubwa, kudhalilisha utu wa mtu, na ni
mfano mbaya kwa watoto na jamii nzima ya mpira wa miguu.
Naye
Morris amefungiwa mechi tatu za VPL baada ya kutiwa hatiani kwa kumpiga mshambuliaji
Emmanuel Okwi wakati timu hizo zilipopambana kwenye mechi ya ligi iliyochezwa
Januari 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kabla ya
kusoma uamuzi, Wakili Msemwa alisema mlalamikiwa Morris alikiri kugongana na
Okwi, kwa maelezo kuwa aliingia kwenye 'reli' ndiyo ukatokea mgongano huo.
Kamati
baada ya kupitia malalamiko ya klabu ya Simba, ripoti za Brain CT scan kutoka
Besta Diagnostic Centre na nyingine kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI),
taarifa za madaktari zilionyesha Okwi aligongwa kichwani akiwa anacheza mpira
na kuzimia kwa dakika tano, pia mkanda wa video uliowasilishwa na TFF imeona
kulikuwa na kugongana kati ya wachezaji hao.
Hivyo,
Kamati ikamtia hatiani Morris kwa kutumia Ibara ya 48(1)(d) ya Kanuni za
Nidhamu za TFF Toleo la 2012 kwa kumfungia mechi hizo tatu na kumpa onyo kali.
Pia
Kamati hiyo imemfungia miezi sita na kumpiga faini ya sh. 200,000 Meneja Vifaa
(Kit Manager) wa timu ya Polisi Mara, Clement Kajeri kwa kuhamamisha vurugu na
kuwapiga waamuzi kwenye mechi dhidi ya Mwadui iliyochezwa Uwanja wa Karume
mjini Musoma. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 40(2) ya Ligi
Daraja la Kwanza.
Wachezaji
watatu wa Friends Rangers; Mahmoud Othman, Khalid Twahil na John Alexander
wamefungia miezi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kumpiga mwamuzi
kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Majimaji.
Licha ya
wachezaji hao kuitikia mwito wa Kamati, wachezaji hao walizuiwa na viongozi wa
kuingia ukumbini wakati malalamiko dhidi yao yalipoanza kusikilizwa. Hatua hiyo
iliifanya Kamati ifanye uamuzi baada ya kuusikiliza upande wa walalamikaji
pekee.
Shauri
dhidi ya mchezaji George Michael wa Ruvu Shooting kwa kumchezea ubabe Amisi
Tambwe wa Yanga, Kamati imeliahirisha baada ya mlalamikiwa kupata udhuru
uliosababisha asiwepo.
Pia Kamati
ya Nidhamu imeelekeza malalamiko ya timu ya Friends Rangers kupinga refa
kuchezesha mechi yao dhidi ya Majimaji kwenye mvua kubwa, kutoa maamuzi yasiyo
halali na kutokuwepo na ukweli kwenye ripoti ya Kamishna yakasikilizwe na Bodi
ya Ligi kwa vile si masuala ya kinidhamu.
No comments:
Post a Comment