Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, September 30, 2013

ROBERTO MANCINI HUYOO UTURUKI..KUIFUNDISHA GALATASARAY


Kocha wa zamani wa Manchester City ,Roberto Mancini anazungumza na mabingwa wa Uturuki Galatasaray kuhusu nafasi iliyo wazi ya kocha wa klabu hiyo.

Klabu hiyo ya mjini Istanbul ilithibitisha katika mtandao wa Twitter kwamba Mancini amekutana na wakurugenzi wa klabu hiyo na kupigwa picha na mkurugenzi mkuu , Lutfi Aribogan.
Mtaliana huyo anatarajiwa kushika nafasi ya Fatih Terim, ambae alipigwa kalamu wiki iliyopita baada ya kushindwa kukubaliana mkataba mpya.
Manchester City ilimfuta Mancini mnamo mwezi wa Mei mwaka mmoja baada ya kuongoza hadi kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya England.


Galatasaray imeanza vibaya msimu wa soka Uturuki ikishinda mechi moja tu kati ya michuano mitano ya kwanza .
Katika michuano ya klabu bingwa ya Ulaya ilicharazwa na Real Madrid,kwa mabao 6-1.
Terim, mwenye umri wa miaka 60, aliongoza Galatasary kushinda mara 6 ubingwa wa Uturuki pamoja na kombe la UEFA mwaka 2000 baada ya kuichezea kwa kipindi cha miaka 11.
Mancini ameshinda ubingwa wa Italia mara tatu akiwa na Inter Milan ya Utaliana kabla ya kunyakua kombe la FA na ubingwa wa ligi na Manchester City.

Kocha: Fatih Terim aliyekula kona Galatasaray
Roberto Mancini

RATIBA YA KLABU BINGWA ULAYA (UEFA CHAMPIONS LEAGUE) KESHO NA JUMATANO


Mechi za Makundi-Raundi ya Pili:
Mechi zote Saa 3 Dakika 45 Usiku
Jumanne 1 Oktoba 2013
FC Basel 1893 v FC Schalke 04
FC Steaua Bucureşti v Chelsea FC
Borussia Dortmund v Olympique de Marseille
Arsenal FC v SSC Napoli
Football Club Zenit v FK Austria Wien
FC Porto Club v Atlético de Madrid
AFC Ajax v AC Milan
Celtic FC v FC Barcelona

Jumatano 2 Oktoba 2013
FC Shakhtar Donetsk v Manchester United FC
Bayer 04 Leverkusen v Real Sociedad de Fútbol
Juventus v Galatasaray A.Ş.
Real Madrid CF FC København
Paris Saint-Germain v SL Benfica
RSC Anderlecht v Olympiacos FC
Manchester City FC v FC Bayern München
PFC CSKA Moskva v FC Viktoria Plzeň
*Jumanne Oktoba 1 na Jumatano Oktoba 2 Mashindano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, UCL, ambayo sasa yapo hatua za Makundi yakiwa na Makundi 8 ya Timu 4 kila moja ambako Timu 2 za juu husonga na kuingia Raundi ya Mtoano ya Timu 32, yataingia Mechi zake za pili baada ya kuanza hapo Septemba 17.









WALIOPASWA KUMRITHI FERGIE BADALA YA MOYES


KITABU cha maisha ya Jose Mourinho, kimesema kuwa kocha huyo wa Chelsea, alimwaga machozi baada ya David Moyes, kupewa jukumu la kurithi mikoba ya Sir Alex Ferguson.
Mwishoni mwa wiki Manchester United walipata kipigo cha pili mfululizo katika Ligi Kuu England.
Kwa wale waliokuwa wakiamini kocha huyo wa zamani wa Everton, Moyes, atafanya vizuri mwishoni mwa msimu akiwa Old Trafford, wameanza kujiuliza kuhusiana na hali hiyo itachukua muda gani, baada ya Manchester Unite kupata kipigo cha pili mfululizo kwenye Ligi Kuu England, tena wakiwa nyumbani dhidi ya West Bromwich Albion.
Hivyo imeonyesha wazi kuwa Moyes, ameshindwa kuimudu timu, baada ya mwenyewe kukiri kuwa amerithi mikoba ya kocha mkubwa na matokeo mabaya huenda yakawandama zaidi.
Makocha watano ambao wangepaswa kumrithi Ferguson, badala ya Moyes ndani ya Old Trafford.
 
5- Carlo Ancelotti
Kocha Carlo Ancelotti, aliweka wazi kuwa ataondoka Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu uliopita na klabu pekee iliyoonyesha dalili ya kumnyemelea ilikuwa ni Real Madrid.
Ancelotti, ambaye ana historia nzuri ya kuongoza klabu kubwa, ingawa aliwahi kuinoa Chelsea, lakini upendo wake kwa Blues usingeweza kumfanya akatae ofa ya kuinoa klabu hiyo ya Old Trafford.
Ukiangalia jinsi alivyokuwa akifanya kazi AC Milan na PSG, alikuwa akijenga mawasiliano mazuri na wachezaji wenye majina makubwa, ambao angeweza kuwanasa kwa urahisi akiwa Manchester United.
 
4- Jurgen Klopp
Ni mtu ambaye alikuwa kwenye orodha ya makocha wanaowaniwa kumrithi Fergie, lakini hakuna mazungumzo yaliyofanyika.
Klopp, amejijengea jina kubwa kwenye soka kwa kupata mafanikio makubwa, baada ya kuwabadilisha chipukizi wa Borussia Dortmund na kuwa timu yenye uwezo wa kuleta ushindani na vikosi vikubwa.
Ni Mjerumani mwenye macho ya kugundua vipaji na kuvitumia uwanjani, jambo ambalo limeweza kumpa heshima Ulaya na itashangaza kama hakuna klabu hata moja kubwa ambayo itakayojaribu kumnasa.
United walikuwa na nafasi hiyo ya kumpa mikoba ya Fergie kocha huyo, ili apate changamoto za Ligi Kuu England, lakini wenyewe waliamua kumpa jukumu hilo Moyes.
Uhusiano wa Klopp na wachezaji, lazima wachezaji kadhaa wangemfuta kocha hyo England.
 
3- Laurent Blanc
Blanc alikuwa United kama mchezaji na sasa amepewa jukumu la kumrithi Carlo Ancelotti katika klabu ya Paris Saint-Germain, hivyo angekuwa mtu sasa kutua Old Trafford.
Kocha huyo wa Ufaransa, alifanya kazi nzuri alipokabidhiwa kikosi cha Bordeaux na angeweza kupewa jukumu la kuinoa United.
Blanc, mwenye umri mdogo wa kuweza kuingoza klabu hiyo ya Old Trafford kwa muda mrefu, huku akiwa uwezo wa kuiongoza timu kwenye hali yoyote.
 
2- Pep Guardiola
Wakati Moyes anapewa jukumu la kuinoa United, tayari Pep Guardiola alikuwa ameshamwaga wino kwenye klabu ya Bayern Munich.
Lakini, kama United wangefikiria kumfuata mapema ili aweze kumrithi Sir Alex, wangeweza kumshawishi na Ligi Kuu England ndio alikuwa akiitaka, ili kujijengea heshima.
Kocha huyo mwenye malengo, alifanikiwa  kuifanya klabu ya Barcelona iliyokuwa na vipaji na kuifanya iweke historia kubwa kwenye soka.
 
1- Jose Mourinho
Huenda Mourinho amelia au hakulia kwa kuchaguliwa Moyes badala yake, lakini  kuinoa United ni kibarua alichokuwa akikitaka kwa muda mrefu.
Special One ni kocha ambaye anapenda mambo yaende anavyotaka yeye na ana njia zake, lakini jambo la kufurahisha ni kwamba anakuwa na uhakika wa mafanikio na mataji.
United walipashwa kumpa kumpa kocha huyo wa Ureno kibarua hicho.
Aba uzoefu wa kunyakua mataji kwenye ligi mbalimbali duniani, ikiwemo Ligi Kuu England, Serie A, La Liga na Ureno.
Klabu hiyo ya Old Trafford kama ingemchukua Mourinho, ungekuwa ni uamuzi sahihi wa kumrithi Ferguson.

SABABU ZA MAN UNITED KUFUNGWA NA MAN CITY 4-1



 
MANCHESTER, England
NAHODHA wa Manchester City, Vincent Kompany, ametoboa siri iliyoifanya timu yao ikaibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya mahasimu wao, Manchester United, akidai ni kujituma kwao.
Anasema, timu nzima ilijituma siku hiyo kwa vile kila mmoja aliuona ushindi kwa City ulikuwa muhimu na wenye maana zaidi kuliko ilivyokuwa kwa United.
Ni kweli, kujituma huko kulionekana kulipa na kama wasingefanya hivyo, wasingeweza kushinda mechi yao. Lakini kwa wale walioitazama mechi hiyo vizuri, watakiri kwamba City, inayonolewa na kocha Manuel Pellegrini pia iliizidi Man United kwa kila idara uwanjani.
United ilionekana kupwaya kwa sababu ilikuwa na pengo kwenye safu yake ya ushambuliaji, kutokana na kutokuwepo kwa Robin Van Persie. Hata hivyo hiyo inaweza isiwe sababu kwani Man City ya Jumapili, ilikuwa sawa sawa.
Kabla ya mechi hiyo, City ya Pellegrini, haikuwa imewahi kuonyesha uzuri wowote na hakuna mtu ambaye angetegemea matokeo kama hayo, lakini kwa uchezaji ule, ilionekana kuwa ni timu iliyojipanga vizuri zaidi kushinda vigogo wote msimu huu.
Nahodha wake, Vincent Kompany na kiungo Yaya Toure walionekana kuwa wao ndio nyota wa mchezo kwa siku hiyo, baada ya kutawala safu ya ulinzi na dimba la kati kiasi cha kuwadhibiti kabisa United.
Kompany alimficha kabisa, Wayne Rooney kwa zaidi ya dakika 60, wakati Toure alikuwa kinara katika kupandisha mashambulizi yote ya City katikati ya dimba na kuifanya Man United kupoteana mara kwa mara.
Kiukweli, vita katika idara ya katikati ilikuwa kubwa lakini, Toure alionekana kuimudu vilivyo.
Toure amekuwa akitumiwa na Pellegrini kama kiungo mkabaji na kwa waliomuona siku hiyo watakubali uwezo wake. Alikuwa akizuia mashambulizi yote yasifike kwao na akatawala kwa kuudhibiti mpira usiende kwa maadui huku akipanda kuongeza nguvu.
Alifanya hivyo kwa dakika zote tisini, na matunda yake ya kupanda mbele yalionekana baada ya kwenda kufunga bao moja kati ya manne.
Uhuru wake wa kupanda na kushuka huku akisaidiana na Fernandinho, uliwafanya waonekane wameitimiza kazi yao ipasavyo, huku wakiwazidi Marouane Fellaini na Michael Carrick.
Pellegrini anaitaka timu yake icheze kwa kumiliki mpira muda mrefu na kwa kumtumia Toure, wamepata mchezaji sahihi wa kuwasaidia.
Alipiga pasi nyingi kuliko mchezaji yeyote wa timu yake, ambapo idadi inaonyesha kuwa aliwazidi kwa pasi 52 sahihi katika mchezo mzima na hadi hivi sasa anaongoza kwa wachezaji wote wa Ligi Kuu ya England.
Kabla ya mechi, ilidhaniwa kuwa winga wa City, Jesus Navas, angeweza kuwa 'sumu' dhidi ya beki wa kushoto wa United, Patrice Evra, ambaye alifikiriwa kuwa ndiye angekuwa mwiba wa kuanzisha mashambulizi.
Vile vile wengi walitarajia kuwa winga wa United, Antonio Valencia angeweza kuwa hatari kwa wapinzani wao hao kutokana na kucheza upande wa beki, Aleksandar Kolarov, ambaye hakabi sana.
Ukweli ukawa kwamba, katika upande huo, Valencia alifunikwa na badala yake Kolarov ndiye aliyeonekana kung'ara zaidi. Uchezaji wa pasi za haraka wa City ulikuwa hatari kwa Man United pande za pembeni, ambapo mabeki walikuwa wakipanda na kushuka muda wote, Kolarov akiongoza.
Bao la kwanza la City, lilikuwa ni mfano mzuri wa aina hiyo ya uchezaji.
Navas aliiba mpira na kuurudisha kwa kipa wake, Joe Hart. Baada ya kipa huyo kuondoa hatari, ulikwenda moja kwa moja kupigwa kichwa na Rio Ferdinand na kunaswa na Samir Nasri.
Nasri aliuchukua haraka na kumpasia Kolarov ambaye alikuwa akipanda kwa kasi, huku Valencia akishindwa kumkaba. Valencia alionekana mvivu kupita kiasi, pengine kutokana na kuzidiwa na akamuachia kazi Chris Smalling ya kuwadhibiti watu wawili, jambo ambalo hakuliweza na kusababisha kufungwa bao.
Sehemu nyingine ya sababu ni kwamba, Toure hakuwa na kazi kubwa ya kupasua katikati na hakuwa na hofu yoyote ya kuzuiwa na watu kama Fellaini au Carrick, hata kama wote wawili wangemfukuza nyuma yake.
Fellaini na Carrick walikuwa wakichunga zaidi pindi Toure alipokuwa akiwafuata na wakasahau kwamba walikuwa wanaachia mwanya kwa wachezaji wengine kuidhuru timu yao.
Haikutarajiwa kama Carrick angeweza kupanda mbele na hata Fellaini alipojaribu kufanya hivyo hakuweza kuleta madhara yoyote zaidi ya kile alichokifanya dakika ya 53 tu.
Toure na Fernandinho walimudu kucheza kama viungo huru, kwa sababu timu yao ilijipanga sawasawa katika idara hiyo na walikuwa na watu wa kazi upande wa ushambuliaji, kotekote kuanzia upande wa pembeni au katikati.
United haikufanya shambulizi lolote kutokea pembeni hadi City ilipokuwa mbele kwa mabao 4-0, ndipo waliposhtuka.
Katika dakika zote 45 za kipindi cha kwanza, Fellaini alionekana kujaribu kukaba tu, Danny Welbeck akawa kama mtoto yatima mbele peke yake na United haikuweza kuwa na madhara yoyote.
Ni kama vile Man United haikujua ni kwanini imeamua kumnunua mtu kama Fellaini na kumchezesha nafasi ya ukabaji wakati anapaswa kuwa kwenye nafasi ya ushambuliaji.
Katika mechi hiyo, United walipaswa kumtumia mbele badala ya ukabaji ili asaidie kupeleka mashambulizi kwa timu pinzani na hilo alilidhihirisha kipindi cha pili (dakika ya 68), alipoweza kupanda mbele na kumpa kipa wa City, Hart usumbufu wa kuokoa hatari yake ya kwanza kubwa.
Baada ya mechi kumalizika, takwimu zinaonyesha kuwa alikuwa miongoni mwa wachezaji waliomudu kugusa mpira mara nyingi zaidi hata alipohamia mbele kwenye eneo la wapinzani.
Lakini kwa upande wa ukabaji, alionekana kupotea na kushindwa kugusa baadhi ya mipira iliyokuwa ikiingia kwenye eneo lao na alifanya kosa la kumpoteza, Toure kwenye kona na kusababisha wafungwe bao la pili.
Pia analazimika kubeba lawama kwa kushindwa kuwasiliana na wenzake na kumruhusu, Sergio Aguero kumtoka na kufunga bao la tatu.
Uchezaji wa Rooney siku hiyo ulionekana kumkuna kocha wake, David Moyes ambaye alimsifia lakini, kwa kipindi hiki ambacho, Van Persie amekosa mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya England tangu atue Old Trafford mwaka 2011, tunaweza kuona ni jinsi gani Mholanzi huyo ana umuhimu kwenye kikosi cha Mashetani hao Wekundu.
Ni sawa na alivyo Kompany kwa upande wa Man City; haiwezi kuwa nzuri bila ya yeye kuwepo katika safu ya ulinzi.
Lakini swali ambalo mashabiki wanaweza kuendelea kujiuliza kuhusu Man United baada ya mechi chache za mwanzo msimu huu ni kwamba je, baadhi ya wachezaji wake wana uzuri kama unaofikiriwa? Kama mwedo wao utaendelea hivyo, hatutegemei iwapo timu hiyo itatwaa ubingwa.
Mabadiliko ambayo Moyes aliyafanya wakati timu yake ikiwa nyuma kwa mabao 4-0 kumuingiza Tom Cleverley badala ya Ashley Young, ilidhihirisha ni jinsi gani ina uhaba wa viungo wa ukweli kuweza kukabiliana na timu ngumu.
@ Ingekuwa vipi Ligi Kuu England bila ya Wenger?
LEO Jumatatu kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, anafikisha miaka 17 ndani ya klabu hiyo ya Emirates.
Lakini mwishoni mwa wiki alisheherekea kufikisha miaka hiyo 17, tangu atue kwenye klabu hiyo mwaka 1996 kwa kuichapa Swanasea City mabao 2-1.
Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, ambaye ni mchambuzi wa mtandao wa Daily Mail, aliandika kuhusiana na Wenger akisema: “Wote tunapaswa kuwa mashabiki wa Arsenal.”
Mawazo hayo hayawezi kukubaliwa na mashabiki wa White Hart Lane wala wale wa Stamford Bridge, Manchester hata wa Merseyside. Lakini msimu huu wote tunapaswa tuwe mashabiki wa Arsenal, aliandika Carragher.
Aliendelea kusema kuwa kama Arsenal watafanikiwa, basi hiyo ina maanisha Wenger atabaki Ligi Kuu England na ukweli ni kwamba anahitajika kubaki.
Filosofia ya Wenger imeleta mambo makubwa katika soka la England na soka lingekuwa bofu kama sio yeye.
Ligi ya England isingekuwaje kama kama sio Wenger? Klabu zisingefikiria kutafuta makocha wakigeni kwa haraka kama asingefanya lolote.
Mafanikio yake yamefungua milango kwa makocha wengine kutua England, tangu kuwasili kwake Arsenal mwaka 1996,  makocha 47 kutoka sehemu wameajiriwa kwenye klabu kubwa, ukilinganisha na makocha 120 wa England. Hiyo ni idadi ya ajabu.
Hakuna ubishi kwamba bila ya Wenger, kusingekuwepo na Jose Mourinho, Rafa Benitez, Roberto Mancini au Carlo Ancelotti.
Bila ya Wenger, isingewezekana kumuona Thierry Henry, Cesc Fabregas na Robert Pires na wachezaji wengine wengi kutoka nje, ambao wameweza kubadilisha soka la England.
Beki huyo wa Reds, alisema kuwa Wenger, ndiye aliyemtia hofu na kumfanya aongeze kiwango chake cha soka, wakati huyo akicheza mpira kabla ya kustaafu.
Arsenal alifanikiwa kutwaa mataji mbalimbali  kutoka mwaka 2002-2004, ambapo kikosi chake kilifanikiwa kuitwa kikosi kilisichofungika, baada ya kumaliza msimu bila ya kufungwa hata mechi moja.
Wachezaji wenye kiwango kizuri na wenye uwezo wa kukimbia — walikuwa na kila kitu. Hata wachezaji wa upinzi waliposimama nao kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, walianza kuogopa kabla ya mechi.
Walikuwa wachezaji wazuri na kuwa na timu ambayo ilikuwa ya kiufundi na nguvu kidogo. Ilikuwa ni timu ambayo imeungana pamoja kuanzia mlinda mlango hadi washambuliaji.
Wachezaji walikuwa wamejengeka kimwili na kama utajaribu kuwasukuma unaweza kuanguka mwenyewe.
Ikiwa unacheza beki wa kulia kwa timu pinzani, halafu ukakutana na Arsenal ya wakati huo, utakuwa na kazi ngumu, kutokana na kuwepo na wachezaji kama Henry, Ashley Cole na Pires.
Wachezaji hao walikuwa na uwezo wa kukufanya kitu kibaya kutokana na uwezo wao wa kukokota mpira kwa kazi  na kumfanya beki akose muda wa kufikiria cha kufanya.
Heshima ya Wenger ilikuwa juu, akiwa ameshinda taji la Ligi Kuu England, mataji mawili ya Kombe la FA na mengine mawili ya Ngao ya Jamii katika muda wa misimu mitatu.
Lakini kwa sasa anaweza kuonekana kituko kwa watu kwa kushindwa kunyakua hata taji moja katika miaka tisa.
Arsenal wameshindwa kushindana na Manchester City na Chelsea, kutokana na matumizi mabaya ya fedha, huku wengine wakiiga mfumo wa Wenger kununua chipukizi kutokana nje.
Ijumaa iliyopita kulikuwa na kauli ya kumuunga mkono kocha huyo, kutoka kwa tajiri mwenye hisa nyingi kwenye klabu hiyo, Stan Kroenke.
Lakini, huu si wakati wa kuanza kumsifia Wenger, bali mashabiki na wadau wanapaswa kusubiri hadi majira ya Krismasi. Kwa sasa ni mapema sana kusema kitu kwa Arsenal, ingawa wanaongoza Ligi Kuu England.
Bila ya shaka wana mambo mengi ya kuwathibitishia na wana kikosi cha ukweli kuweza kuvaana na Manchester City, Manchester United na Chelsea.
Ushindi mmoja walioupata dhidi ya mahasimu wao Tottenham, kikosi pekee chenye  upinzani ambacho Arsenal wamekutanana nacho, hautoshi kuwapima Gunners.
Wakiwa chini ya Wenger, wamefanikiwa kufuzu kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa muda wote wa miaka 16, lakini wameshindwa kunyakua Kombe la FA ama la ligi, pamoja na kuwepo ‘top four’, kutokana na kutokuwa wazuri.
Wengi wa mashabiki wanaweza kuwa wamechoshwa na Wenger kwa kuwa wanaijua klabu yao, lakini mara nyingi wale ambao wamekuwa wakimkasirikia pale timu inapovurunda ila ikifanya vizuri wamekuwa wakigeuka na kucheka baada ya kuona mazuri.
Mwanzoni mwa msimu, baada ya Arsenal kuchaowa mabao 3-1 dhidi ya Aston Villa, mashabiki wengi walianza kumzodoa kocha huyo. Wengi wakisema hakuna jipya, wanaonekana kuwa wadhaifu.
Lakini, kuwasili kwa Mesut Ozil, kumewasaidia kufanya vizuri na kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho.
Ozil ni mchezaji pekee mwenye kiwango kizuri, ambaye amewasili Arsenal siku kabla ya dirisha la usajili kufungwa na kuifanya timu hiyo kuwa ya kuvutia katika wiki za mwanzoni, lakini mambo yanaweza yakawa magumu wiki hii kwa kukutana na Napoli hapo kesho.
Lakini kuna maeneo muhimu ambayo yanatakiwa yawekwe vizuri kwenye kikosi hicho. Watakuwa kwenye matatizo kama mshambuliaji wao Olivier Giroud atapata majeruhi, lakini pia wanapaswa watoe ofa kwa ajili ya mlinda mlango wa Real Madrid, Iker Casillas au Victor Valdes wa Barcelona kwa ajili ya kuwasajili Januari mwakani, ili wawe na mlinda mlango mwenye kiwango wanaemhitaji.
Wanaweza wakamaliza wakiwa ‘top four’ tena. Lakini tumtarajie kumuona Wenger kuingia sokoni dirisha la usajili la January na kusajili wachezaji wengine wenye kiwango, ili waweze kupambana na kuweza kuwania taji.
Carrangha, alimaliza kwa kusema kuwa tunamtaka abaki, ili tupata kuona soka zuri zaidi la Arsenal na wachezaji atakaowazalisha.
Tunapaswa kuwaunga mkono Arsenal msimu huu. Wenger anahitaji kipindi kingine cha kunyakua mataji na wote tunapaswa kumtakia mafanikio mema, ili soka la England lipate kufanikiwa kutoka kwake.
Miaka ya Wenger, Arsenal
1996-97:  Nafasi ya tatu Ligi Kuu England
1997-98: Mabingwa wa li, Kombe la FA
1998-99: Mshindi wa pili wa ligi
1999-00: Mshindi wa pili wa Kombe Uefa na mshindi wa pili Ligi Kuu England
2000-01: Mshindi wa pili wa ligi na Kombe la FA
2001-02: Mabingwa wa li na Kombe la FA
2002-03: Kombe la FA na washindi wa pili wa ligi
2003-04: Mabingwa wa ligi
2004-05: Washindi wa pili wa ligi na Kombe la FA
2005-06: Washindi wa pili wa ligi
2006-07: Nafasi ya nne ya ligi na nafasi ya pili wa Kombe la Ligi
2007-08: Nafasi ya tatu  Ligi Kuu England
2008-09: Nafasi ya nne Ligi Kuu England
2009-10: Nafasi ya tatu  Ligi Kuu England
2010-11: Nafasi ya nne Ligi Kuu England, washindi wa pili wa Kombe la Ligi
2011-12: Nafasi ya tatu  Ligi Kuu England
2012-13: Nafasi ya nne Ligi Kuu England

KIKOSI CHA MAN UNITED CHAMTIA HOFU MOYES, MOURIHNO ALIA NA VERTONGHEN NA ARSENAL, LIVERPOOL ZAMNYATIA BALOTELLI



MANCHESTER, England
KOCHA wa Manchester United, David Moyes ameshikwa na ‘kitete’ juu ya ubora wa kikosi chake baada ya timu hiyo kupigwa mabao 2-1 na West Bromwich Albion, Old Trafford kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, juzi.
Man United imeweka rekodi mbaya zaidi ya mwanzo wa ligi katika kipindi cha miaka 24, kikosi cha Moyes kimefungwa mechi tatu kati ya sita na kufanikiwa kupata pointi saba tu mpaka sasa na hii ni rekodi mbovu zaidi ya United tangu msimu wa 1989-90, zama za mwanzo za Sir Alex Ferguson.
Moyes ameonyesha kuwa na hofu ya kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, kutokana na kikosi chake kukosa wachezaji wa kiwango cha dunia wa kutosha.
“Kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya, unahitaji wachezaji watano au sita wa kiwango cha dunia,” alisema Moyes.
“Angalia Bayern Munich, wanajaa. Angalia Barcelona, walikuwa nao siku za nyuma na Real Madrid, ambao wanaweza kuwa nao sasa. Hivyo ndivyo unatakiwa kuwa kama unataka kuchukua taji la Ulaya. Hatuna hilo bado, lakini tumejaza uzoefu.

“Nilipopewa kazi hii, ilikuwa lazima mabadiliko yafanyike na tukomae kadri siku zinavyozidi kusonga mbele.”
Moyes amekuwa na wiki ngumu baada ya Man United kufungwa mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu England na Manchester City na West Brom na kocha huyo wa United amekiri kwamba matokeo ya timu hiyo yanamtisha, hasa kutokana na timu hiyo kushindwa kufunga mabao ya ‘muvu’ kwenye ligi tangu baada ya mechi ya Swansea.

“Yalikuwa matokeo mabovu na kiwango kibovu,” alisema Moyes, “Hatukuonyesha mchezo mzuri. Tulimiliki mpira sana kipindi cha kwanza, lakini nafasi hatukutengeneza. Na tulipozitengeneza hatukuzitumia. Walikuwa hatari zaidi kwenye mashambulizi ya kushtukiza katika kipindi cha kwanza na zaidi walitisha kipindi cha pili.
“Ndio ninahofu baada ya matokeo ya leo, lakini kwa sababu tu hatukucheza vizuri. Kuna mechi nyingi zinakuja, nitajaribu na kuweka mambo sawa kwenye mechi zijazo.”

Moyes aliongeza kwamba, kinachowaangusha ni kushindwa kutengeneza mabao ya muvu na siyo kwamba hawana washambuliaji au wameshindwa kuonyesha kiwango, anaamini kwamba wanahitaji kujituma zaidi.
Mskochi huyo alisema kwamba, kwenye mechi dhidi ya West Brom, wachezaji walikuwa hawana hamasa uwanjani na walistahili kufungwa kutokana na hilo.
United juzi ililala kwa mabao ya Morgan Amalfitano na Saido Berahino, huku bao pekee la Man United likifungwa na Wayne Rooney kwa njia ya adhabu.
@@@@
 
Mourinho alia na Vertonghen
LONDON, England
KOCHA wa Chelsea, Jose Mourinho amemuangushia zigo la lawama beki wa Tottenham Hotspur, Jan Vertonghen kwa kumtafutia kadi nyekundu straika wake, Fernando Torres.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, Mourinho anaamini kwamba, Vertonghen alimdanganya mwamuzi na kumtafutia Torres kadi ya pili ya njano na kusababisha straika huyo atolewe kwa kadi nyekundu.
“Timu yangu ilikuwa vizuri sana, mpaka mwamuzi alipofanya makosa, makosa makubwa ambayo yalichangia sana kusababisha matokeo yawe vile. Mwamuzi hana hatia, Mchezaji (Vertonghen) ndiye mwenye hatia. Alijidanganyisha kana kwamba ameguswa sana na Fernando (Torres) na mwamuzi akamuamini na kutoa kadi,” alisema Mourinho.
Mourinho anaamini kadi hiyo ya Torres aliyoipata zikiwa zimesalia dakika 10 mechi kuisha, kwa kiasi kikubwa iliinyima ushindi timu yake, ambayo ilikuwa ikishambulia kwa kasi wakati huo.
@@@@

  
Arsenal, Liverpool zamnyatia Balotelli
LONDON, England
ARSENAL na Liverpool zinaangalia uwezekano wa kumsajili straika mtukutu wa AC Milan, Mario Balotelli wakati wa dirisha dogo la usajili la Januari.
Kumekuwa na taarifa nchini Italia kwamba, Balotelli ‘Mad Mario’ tangu alipoondoka Manchester City amekuwa na vipindi tofauti akiwa AC Milan.
Pia amekuwa akikutana na tatizo la ubaguzi wa rangi kila kukicha kwenye majukwaa ya soka ya Italia, hivyo wachambuzi wa mambo wameanza kuamini kwamba kunauwezekano wa straika huyo kuuzwa kwa dau la pauni milioni 12 na Arsenal na Liverpool zinaweza kumtupia ndoano.

BALE APATA MJENGO KARIBU NA RONALDO, GERRARD ATAMANI UKOCHA LIVERPOOL NA MESSI AIBEBA BARCA NA KUUMIA



 
MADRID, Hispania
WINGA wa zamani wa Tottenham Hotspur, Gareth Bale, aliyesajiliwa msimu huu katika kikosi cha Real Madrid kwa dau la rekodi ya dunia, amefanikiwa kupata nyumba mpya ya kupanga Madrid ambayo atakuwa akilipa kodi ya euro 10,000 (sh milioni 21.251) kwa mwezi.
Bale mwenye umri wa miaka 24, alisema kuwa anajisikia furaha kukaa katika Jumba hilo lililopo karibu na mjengo wa Cristiano Ronaldo, aliyevunja rekodi yake ya kusajiliwa.
“Wazazi wangu, Frank na Debora walikuja kunitembelea hapa wakiwa pamoja na mchumba wangu, Emma Rhys-Jones na mtoto wetu Alba, hii ni hatua nzuri kwangu na ninafurahia kuwa katika kikosi hiki,” alisema Gareth.
Mchezaji huyo ameingia mkataba wa miaka sita wenye thamani ya kitita cha euro milioni 100, baada ya kukamilika kwa mchakato mrefu wa usajili huo na kuongeza chachu ya safu ya ushambuliaji ya Santiago Bernabeu.
@@@@@@@@
 


Gerrard atamani ukocha Liverpool

LIVERPOOL, England
NAHODHA wa Liverpool, Steven Gerrard amesema kuwa amebakiza muda mfupi wa kuitumikia klabu hiyo uwanjani na sasa anatamani kuwa mmoja wa makocha wa klabu hiyo, mara baada ya kutundika daluga.
Gerrard (33), alisema kwamba anamapenzi makubwa na timu hiyo, hivyo amewaomba viongozi wake walifikirie suala hilo ili aendelee kuitumikia Liverpool katika maisha yake yote.
“Ndoto zangu ni kuwa kocha wa Liverpool mara nitakapostaafu soka. Kwangu ni fahari kubwa kuitumikia klabu hii ambayo nina mapenzi nayo ya dhati,” alisema Gerrard na kuongeza kuwa:
“Ukiona umefikia umri wa kutaka kustaafu soka, ni lazima uanze kufikiria mambo makubwa kwa ajili ya maisha ya baadaye, hivyo mikakati yangu ni kuwa meneja wa timu hii.”
@@@@@@@@@

 
Messi aibeba Barca, aumia mguu
BARCELONA, Hispania
STRAIKA wa Barcelona, Lionel Messi usiku wa kuamkia jana alifanikiwa kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Almeria, lakini alijikuta anashindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia mguu wake wa kulia.
Messi, ambaye Ijumaa iliyopita alitinga mahakamani kujibu mashitaka yanayohusiana na ukwepaji wa kodi, alifunga bao dakika ya 21 likiwa ni la 11 msimu huu katika mashindano yote.
Adriano Correia aliongeza bao la pili na la ushindi kwa timu hiyo. Kuumia kwa nyota huyo kumemsikitisha Kocha wake, Gerardo Marino kwa kile alichodai kuwa, mwanandinga huyo ni muhimu katika kikosi chake.
“Kuumia kwa Messi ni pigo kubwa kwetu kwa sababu ni muhimu sana katika timu hii na sasa nawaachia madaktari ambao watamfanyia vipimo ili kujua ameumia kwa kiasi gani ila kwa sasa siwezi kusema chochote,” alisema Marino.




BALE ALIMBANIA SIGURDSSON KUTUA SUNDERLAND, EVERTON YAPANIA KUMBAKIZA BARRY, FLETCHER KURUDI UWANJANI OCTOBA NA MUSTAKABALI WA TERRY MIKONONI MWA MOURIHNO



LONDON, England
STRAIKA wa Tottenham Hotspur, Gylfi Sigurdsson (24), alishindwa kutua Sunderland akitokea Spurs kutokana na sakata la uhamisho wa Gareth Bale kwenda Real Madrid, inasemekana Sigurdsson ambaye alifunga bao la Spurs kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Chelsea, alitakiwa na Sunderland na jamaa walikuwa tayari kutoa pauni milioni 10 kwa ajili yake, lakini kampuni yake ya uwakala ya Stellar Group ilikuwa imeelekeza nguvu zake zote kufanikisha uhamisho wa Bale na kumsahau yeye.
@@@@

Everton wapania kumbakiza Barry
LIVERPOOL, England
EVERTON wanataka kumpa mkataba wa kudumu, Gareth Barry (32), anayeichezea klabu hiyo kwa sasa kwa mkopo wa muda mrefu akitokea Manchester City, inasemekana kocha wa miamba hiyo ya Goodison Park, Roberto Martinez, ameridhishwa na kiwango cha nyota anayepokea kiasi cha pauni 120,000 (sh milioni 304.363) kwa wiki na anataka kumbakiza baada ya mkataba wake wa mkopo kuisha.
@@@@
 
Fletcher kurudi uwanjani Oktoba
MANCHESTER, England
KIUNGO wa Manchester United, Darren Fletcher (29) anatarajiwa kurudi uwanjani Oktoba, mwaka huu baada ya kukaa benchi kwa muda mrefu akisumbuliwa na majeruhi, bado haijafahamika siku rasmi ambayo Fletcher atarudi uwanjani, lakini madaktari wa Man Utd wanaamini itakuwa Oktoba, hii ni baada ya kukaa benchi tangu Januari, huku katika kipindi cha miaka miwili akicheza mechi saba tu, kutokana na matatizo ya kiafya.
@@@@

Mustakabali wa Terry mikononi kwa Mourinho
LONDON, England
MUSTAKABALI wa John Terry (32), katika klabu ya Chelsea, uko mikononi kwa kocha wake, Jose Mourinho, ambaye ndiye ameshika rungu la kuamua kumuongeza mkataba au kumuacha aende zake pindi mkataba wake wa sasa utakapomalizika. Zamani Mkurugenzi wa Ufundi, Michael Emenalo na Bodi ya klabu ndiyo walikuwa na sauti ya kuamua, lakini sasa hivi Mourinho ndiye mwenye sauti ya mwisho kwenye ishu ya Terry na Frank Lampard.

SMS YA MESSI ILIMTIMUA IBRAHIMOVIC CAMP NOU, KAGAWA NJIA PANDA MAN U NA WENGER AHAMIA KWA LARS BENDER


BARCELONA, Hispania
IMEFAHAMIKA kwamba, meseji ya Lionel Messi kwa kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola, ndiyo iliyomfukuzisha Zlatan Ibrahimovic Camp Nou.
Katika kitabu cha El Misterio de Messi (Upande wa pili wa Messi), waandishi Sebastian Fest na Alexandre Juillard wametoboa siri za tabia mbovu za Messi.
Sehemu ya kwanza ya kitabu hicho iliyopewa jina la El Shock, imeeleza jinsi Messi alivyochangia kumuondoa Ibra, Camp Nou, inasemekana baada ya Ibra kusajiliwa mwaka 2009, Messi aliamua kumuandikia sms Guardiola ambayo ilikuwa inasema: “Sawa bwana, ninaona kwamba sina umuhimu tena kwenye timu, hivyo…..”
Sms hiyo ya Messi inasemakana kumfanya Guardiola ambaye alilazimisha uhamisho wa Ibra kuanza kutaka kumtumia pembeni Ibra, lakini Msweden huyo aligoma na kuamua kuondoka msimu uliofuata.
@@@@
 
Kagawa njia panda Man Utd
MANCHESTER, England
MUSTAKABALI wa Shinji Kagawa, Manchester United unaonekana kuwa njia panda, kutokana na staa huyo wa Kijapan kutolewa wakati wa mapumziko kwenye mechi dhidi ya West Brom ambayo United ililala kwa mabao 2-1, lakini David Moyes mwenyewe anadai kuwa alimtoa Kagawa kutokana na sababu za kiufundi, na kusisitiza kwamba Mjapan huyo yupo kwenye mipango yake ya baadaye.
@@@\
 
Wenger ahamia kwa Lars Bender
LONDON, England
KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger anaonekana kuanza kunogewa na wachezaji wa Kijerumani, baada ya kumsajili Mesut Ozil na sasa chaguo lake la kwanza kwenye usajili wa wakati wa Januari ni kiungo wa Bayer Leverkusen, Lars Bender na Wenger yuko tayari kuweka mezani pauni milioni 20 (sh bilioni 50.727).
Wenger tayari alishaweka mezani pauni milioni 18.5 (sh bilioni 45.654), kwa ajili ya kiungo huyo ambaye anatazamiwa kuja kurithi mikoba ya Mikael Arteta, huku kukiwa na taarifa kwamba Ozil ndiye aliyempigia debe Mjerumani mwenzake huyo.

AARON RAMSEY AFURAHIA KUFUNGA BAO WAKATI WANAIBWAGA SWANSEA CITY BAO 2-1.


Mchezaji kiungo wa Wales na Arsenal Aaron Ramsey anasema alifurahia kufunga katika ushindi wa Arsenal 2-1 dhidi ya klabu Swansea kwenye uwanja wa Liberty hapo jana.
Mchezaji huyo aliyeichezea watani wa Swansea, Cardiff City alizomewa kupitia kiupindi chote cha mchuano na mashabiki wa Swansea.
Bao la Ramsey lilipatikana katika dakika ya 62 kuipa klabu yake ya Arsenal mabao mawili kuthibitisha mwendo wao wa kushinda.
Ushindi wa Arsenal umeizidishia klabu hiyo rekodi ya kushinda ugenini kutimiza mechi 12 ikiwa ni sawa na rekodi yao ya mechi nane katika Ligi ya Premier iliyowekwa katika msimu wa mwaka 2001-02. 

Katika ushindi wa jumamosi, Ramsey, aliyejiunga na Arsenal mwaka 2008 akiwa kija na mwenye umri wa miaka 17 na baada ya hapo kukumbwa na jeraha lililomueka nje ya mchezo ka kipindi kirefu na baada ya hapo kushindwa kufikia viwango na kukemewa na mashabiki hapo jana alikua chachu ya ushindi dhidi ya Swansea.

LIVERPOOL ILIVYOICHAPA SUNDELAND 3-1 KWENYE ENGLISH PREMIER LEAGUE, KOCHA MPYA WA SUNDERLAND AKARIBISWA KWA KICHAPO



Kocha wa Liverpool Brendan Rodgers (kushoto) akisalimiana na kocha mpya wa Sunderland  Kevin Ball kabla ya MtanangeDaniel Sturridge ndiye aliyeanza kuifungia bao Liverpool dakika ya 28 kipindi cha kwanza, bao safi la kiaina kwa kutupia kwa kichwa.Daniel Sturridge akishangilia bao lake la 7 kwa msimu huu.
Daniel Sturridge akiwaamusha mashabiki ugenini..
Luis Suarez nae akifurahia bao lake la pili kwa msimu huu baada ya kurudi tangu kufungiwa kwake mechi 10 na hapa aliifungia bao Liverpool dakika ya 36 kipindi cha kwanza baada ya kupewa krosi safi kama kona na kuteleza na mpira hadi nyavuni.Dakika ya 89 Luis Suarez akaongeza bao la tatu na la mwisho huku likiwa bao lake la pili kwenye mtanange huu. Ushindi huu wa Majogoo Liverpool unawapandisha juu kwenye msimamo hadi nafasi ya pili chini ya Arsenal wakiwa na Pointi 13 na Arsenal 15, Wao Sunderland ambao wamechapwa tena leo hii wamezidi kukandamizwa mkiani wakiwa na pointi 1 tu na madeni ya mabao yakiongezeka, hakika Kocha mpya anakazi ya ziada. Kesho Jumatatu usiku saa 4:00 ni Everton na Newcastle United.

FRANSIC MIYEYUSHO AMTWANGA SADIK MOMBA KWA POINTI JANA


Bondia Sadiki Momba kushoto akioneshana umwamba wa kutupiana makonde na Fransic Miyeyusho wakati wa mpambano wao usiokuwa wa ubingwa uliofanyika siku ya jumapili katika ukumbi wa  Friends Coner  Manzese Dar es salaam Miyeyusho alishinda kwa pointi
Bondia Sadiki Momba kushoto akioneshana umwamba wa kutupiana makonde na Fransic Miyeyusho wakati wa mpambano wao usiokuwa wa ubingwa uliofanyika siku ya jumapili katika ukumbi wa  Friends Coner  Manzese Dar es salaam Miyeyusho alishinda kwa pointi
refarii Sako Mtlya akimnyoosha mkono juu bondia  Fransic Miyeyusho baada ya kumgalagaza Bondia Sadiki Momba wakati wa mpambano wao
Bondia Mussa Sunga kushoto akipambana na Fahiri Awadhi wakati wa mpambano wao uliofganyika jumapili Awadhi alishinda kwa Pointi

SIMBA YAZIDI KUJIIMARISHA KILELENI YAICHAPA JKT RUVU 2-0






SIMBA imeendelea kuchanja mbuga baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-0, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyochezwa jana, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Simba imezidi kuwaacha watani wao wa jadi Yanga kwa tofauti ya pointi tano, huku ikiendelea kukaa kileleni kutokana na pointi 14, huku ikiwa haijafungwa zaidi ya kutoka sare mechi mbili na kushinda  mechi nne. 

JKT Ruvu iliyoanza ikiongoza katika msimamo wa ligi hiyo kabla ya Simba, imeshuka hadi nafasi ya saba  kutokana na pointi tisa sawa na Yanga inayoshika nafasi ya tano huku Azam FC ikipanda hadi nafasi ya nne kutokana na sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons jana na kuifanya timu hiyo kufikisha pointi 10 sawa na Coastal Union inayoshika nafasi ya tatu huku Kagera Sugar inaifuatia Simba, baada ya kujikusanyia pointi 11 na Ruvu Shooting ikiwa nafasi ya sita kutokana na pointi tisa, huku timu zote zikiwa zimecheza mechi sita kila moja.

Katika mechi ya jana, Simba ilikuwa ya kwanza kulifikia lango la JKT Ruvu ikiwa ni dakika ya saba, baada ya Amis Tambwe kupiga shuti kali akitumia krosi ya Amri Kiemba, lakini alitokea Shaban Dihile na kuokoa hatari hiyo.

Dakika ya 17, Abdulhalim Humud alioneshwa kadi ya njano kutokana na kumchezea rafu mshambuliaji wa JKT Ruvu, Salum Machaku.
Hata hivyo, JKT Ruvu ilipoteza nafasi ya kufunga katika dakika ya 21, baada ya beki wa timu hiyo, Stanley Nkomola kupiga krosi iliyomkuta Damas Makwaya na kupiga shuti ambalo liliokolewa na Kipa wa Simba, Abel Dhaira.

Mechi hiyo iliyochezeshwa na Mwamuzi, Antony Kayombo kutoka Rukwa, alitoa penalti kwa Simba dakika ya 24, iliyoonwa na mwamuzi wa pembeni, John Kanyenye, baada ya beki wa JKT Ruvu, Jamal Said kunawa mpira katika eneo la hatari iliyofungwa na Tambwe na kumfanya akifikishe mabao saba.
Katika dakika ya 43, Makwaya aliwatoka mabeki wa Simba na kuachia shuti kali, lakini kutokana na ushupavu wa Kipa, Abel  Dhaira aliondoa hatari hiyo.

Simba ilipata bao la pili kupitia kwa Ramadhan Singano ‘Messi’ aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Kiemba, aliyefunga bao la moja kwa moja baada ya kuunganisha krosi ya Humud.
JKT Ruvu walipoteza nafasi ya kufunga baada ya Emmanuel Pius kupiga shuti kali katika dakika ya 80, lakini Kipa wa Simba, Dhaira aliweza kupangua shuti hilo.

Simba iliwakilishwa na wachezaji, Abel Dhaira, Haruna Shamte, Adeyoun Seif, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Abdulhalim Humud, Amri Kiemba, Said Ndemla, Amis Tambwe, Betram Mombeki, na Haruna Chanongo.

JKT Ruvu: Shaban Dihile, Damas Makwaya, Stanley Nkomola, Omari Mtaki, Jamal Said, Nashon Naftal, Alhaji Zege, Emmanuel Swita/ Richard Msenya (dk 58), Bakari Kondo/Paul Ndauka (dk 78), Salum Mchaku na Emmanuel Pius.

Wakati huo huo, Azam FC imetoka sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Bao la Tanzania  Prisons lilifungwa na Peter Michael katika dakika ya 36 na, lilifungwa na Kipre Tchetche dakika ya 49.

Katika mechi nyingine iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam Ashanti United imetoka sare ya mabao 2-2 na Mtibwa Sugar.