Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, December 13, 2013

SIMBA YANASA SAINI YA BEKI WA KATI WA GOR MAHIA

Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
SIMBA SC jana ilifanikiwa kumsainisha Mkataba wa miaka miwili, beki wa kati wa klabu ya Gor Mahia ya Kenya, Donald Mosoti Omwanwa, ambaye ni pendekezo la kocha wa timu hiyo, Mcroatia, Zdravko Logarusic pamoja na kipa Ivo Mapunda.
Katibu wa Simba SC, Wakili Evodius Mtawala alitua jana usiku Nairobi na leo mchana akamsainisha Mkataba wa miaka miwili mchezaji huyo, mbele ya mchumba wake, Lilian Atieno.
Kifaa kipya; Beki wa Gor Mahia ya Kenya, Donald Mosoto Omwanwa akisaini Mkataba wa kuichezea Simba SC pembeni ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Wakili Evodius Mtawala mchana wa leo mjini Nairobi, Kenya.

Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya kusaini Mkataba huo, beki huyo mrefu alisema kwamba anashukuru kujiunga na Simba SC, kwani ni klabu kubwa na ya kihistoria Afrika Mashariki.
“Nimefurahi kusaini Simba SC, hii ni klabu kubwa na ya kihistoria ukanda huu wa Afrika Mashariki, nataka kufuata nyayo za Wakenya wengine waliochezea klabu hii kwa mafanikio kama Mark Sirengo, Hillary Echesa na Mike Barasa,”alisema.
Mchezaji huyo anayetarajiwa kuondoka kesho kwenda Dar es Salaam kujiunga na wenzake, alisema kwamba amefurahi pia kwenda kufanya kazi tena chini ya kocha Logarusic, ambaye alikuwa mwalimu wake Gor Mahia.





“Mimi binafsi kama mchezaji ni faraja kwenda kufanya tena kazi na Loga, ni kocha mzuri na aliifanya Gor iwe na heshima hapa (Kenya) na hata Simba SC wajue wamepata kocha mzuri,”alisema.
Donald Mosoti Omanwa alizaliwa Julai 14, mwaka 1981 kijiji cha Kisii, Nyanza nchini na Kenya na alipata elimu yake ya Msingi na sekondari huko huko Kisii.
Kisoka, baada ya mpira wa shule, beki huyo alianzia klabu ya World Hope ya Nairobi mwaka 2005 kabla ya kuhamia Nairobi City Stars mwaka 2008 ambako alicheza hadi mwaka 2011 alipojiunga na Gor Mahia.
Omwanwa alisema Mkataba wake wa sasa na Gor Mahia unamalizika Februari 31, mwakani lakini ameruhusiwa kusaini Simba SC kwa kuwa Ligi ya Kenya inaanza Machi mwakani.
“Hakuna tatizo, Simba watapatiwa ITC (Hati ya Uhamisho wa Kimataifa) na nitacheza Tanzania,”alisema beki huyo aliyewahi kuichezea Kenya, Harambee Stars mechi moja tu dhidi ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ ya kirafiki ya kimataifa iliyokuwa katika kalenda ya FIFA.       
Baada ya kumsaini beki huyo, Simba SC iko katika hatua za mwisho za kumalizana na Ivo Mapunda, aliyemaliza Mkataba wake Gor Mahia.

No comments:

Post a Comment